06/04/2012

Barua ya wazi kwa Joshua Nassari

Mbunge Mteule wa Arumeru Mashariki, Joshua NassariBARUA YA WAZI KWA Ndg. JOSHUA NASSARI, MBUNGE WA ARUMERU MASHARIKI
Ndugu Joshua,

Natumai umepata pongezi za kutosha juu ya kushinda kwako katika kinyang’anyiro cha Ubunge. Ushindi wako haukua lelemama. Nchi nzima iligeuzia macho na masikio yake Arumeru. Uliposhinda ndipo nilipogundua kuwa hukuwa chaguo la Wanaarumeru wala wapenzi wa Chadema. Kila niliyekutana naye alilitaja jina lako kwa furaha huku akishangilia kushindwa kwa CCM. Hapa Chuoni (UDSM), ushindi wako ulikuwa gumzo. Mtaani umejaa vinywani mwa watu. Kwa utafiti mdogo nilioufanya, wengi wamefurahia zaidi kuporomoka kwa ngome ya CCM.

Kwa ukubwa wa majukumu uliyopewa na matumaini uliyotwishwa, nadhani hata wewe unatishikatishika. Binafsi nachelea kukupongeza. Kila nikutazamapo naona nyuso za vikongwe, akina mama na wototo wenye njaa, waliodhoofu na wagonjwa. Nawaona vijana wasio na ajira na waliokata tama. Naona umbali mrefu watembeao akinamama kuteka maji. Nawaona yatima, wajane, n.k. Nawaona wanafunzi waliofukuzwa shule na vyuo kwa kukosa ada… Wamepoteza matumaini, wote wanakutazama wewe kama jibu la matatizo yao. Huo ni upande mmoja. Upande wa pili, naona watu wakipanga kugawana fedha za kodi na miradi ya maendeleo. Naona jinsi rasilimali za nchi hii zinavyoneemesha mataifa ya nje na vijibwa vyao vya hapa nchini. Na wewe upo katikati ukipiga makelele, kama kilivyo chama chako [kiitikadi?]. Je, ni silaha gani  utakazotumia kurejesha matumaini kwa wanyonge?

Tafakuri ilinipeleka mbali na kunifanya nikumbuke Januari 2009, nikiwa mwasisi wa Bunge Kivuli la Vijana wa Dar es Salaam (DSM Youth Shadow Parliament – DAYOSHPA). Hili lilikuwa jukwaa la aina yake ambalo liliwakutanisha vijana wa makundi mbalimbali ili kujadili namna ya kuboresha mfumo wa elimu hapa nchini. Hii ilikuwa ni baada ya mgomo mkubwa wa wanafunzi wa vyuo vikuu wakipinga mfumo wa madaraja ya mikopo uliopelekea kufungwa kwa vyuo vikuu vya umma takribani nane. Jukwaa hili halikuwa na mfadhili. Lilikuwa ni jukwaa la vijana na liliondeshwa kwa nguvu ya vijana bila kulipwa chochote.

Kuna mmoja wa wabunge mahiri katika kambi ya upinzani ‘aliyenikosesha raha’ katika kiti cha uspika nilichokuwa nimekikalia. Kila mara alinitumia ki-‘memo’ kunikumbusha kuwa nikimwita jina lake, mwishoni nitaje ‘Mbunge wa Arumeru Mashariki’, ilhali akijua kuwa wabunge wote wa bunge lile kivuli hawakuwa na majimbo! Walikuwa ni wabunge wa kitaifa. Mbunge huyo hakuwa mwingine bali ni wewe Joshua Nassari.

Hiyo ilikuwa ni mwaka 2009. Tayari ulikuwa na ndoto za kuwania ubunge wa Arumeru Mashariki. Mara kadhaa ulinishawishi kuwa lazima vijana tushike nafasi za uongozi ili tulete mabadiliko. Niliposema kushika nafasi za kisiasa sio sawa na kumkomboa myonge, ulinikosoa: ‘Wewe ‘political scientist’ (mwanasayansi wa siasa) gani usiyependa siasa?’ Nami nikakutahadharisha kutofautisha kati ya siasa na madaraka huku nikimnukuu Prof. Shivji: ‘[M]imi si mwanasiasa, ingawa ninapenda siasa. Wanasiasa huwa hawapendi siasa, wanapenda madaraka‘. 

Kwa kuwa tulikuwa tukiishi mtaa mmoja, aghalabu tulikutana kwa mama ntiliye na kuanza kutaniana. ‘Mheshimiwa Spika, hata wewe unakula kwa mama ntiliye?’ Ila tukajifariji: sisi ndio wawakilishi halisi wa wanyonge. Tunapanda nao daladala na tunakula nao kwa mama ntiliye. Na hatukufanya hivyo kwa kuigiza bali ndivyo maisha yalivyotulazimisha.

Lakini sasa wewe si mbunge-kivuli tena. Ni mbunge wa ukweli. Hutalazimika kuazima koti na tai au kushangilia hotuba yako iliponukuliwa gazetini au sura yako kuonekana katika televisheni [kama tulivyokuwa tukifanya enzi zile]. Hivi sasa, ili magazeti yauze sharti yaandike habari zako, iwe za kweli ama za uongo. Nafasi yako inakurusha mbali kimaisha na watu waliokuchagua. Ukipanda daladala au kula kwa mama ntiliye, utafanya hivyo kwa kuigiza si kwa kulazimishwa na hali ya kipato chako. Mwisho wa mwezi huu, bila shaka, akaunti yako itakua na salio lisilopungua milioni kumi! Tena utaongezewa zingine milioni tisini kwa ajili ya gari. Hayo ndio maisha mapya ya uwakilishi wa wananchi. Sina hakika kama dhana ya uwakilishi inaleta maana hapa.


Ningependa kukukumbusha sehemu ya hotuba yako katika Bunge Kivuli mwaka 2009. Kila mmoja alikereketwa kwa utamu wa hotuba zako zenye mrengo wa kimapinduzi na zilizofanyiwa tafiti. Iwapo umepoteza mkanda wa Bunge lile, nitakusaidia kunukuu sehemu ya hotuba yako kuhusu nini kifanyike ili kuiokoa elimu yetu:
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba elimu yetu ni kivuli hafifu cha elimu ya kikoloni: imekosa ubora uliokuwa ndani ya elimu ya kikoloni ya wakati ule na pia imekosa maudhui ya kiukombozi kwa sababu haionekani kuwa na malengo thabiti yanayoangalia mustakabali wa nchi yetu. Katika vigoda hivi viwili, elimu yetu imedondoka sakafuni.
Mheshimiwa Spika, tumekataa kukubali kwamba mfumo mzima wa elimu yetu umevurugika baada ya kukubali kwamba turudi katika chumba cha usanifu na kuuchora mfumo huo upya. Tumehangaika kujenga vyumba vingi zaidi na kuelezea ujinga kwa gharama kubwa.
Mheshimiwa Spika, kinachohitajika katika mfumo wa elimu yetu si jambo jingine bali ni mapinduzi ya elimu ambayo yataandamana na elimu ya mapinduzi itakayozagaa katika sekta zote muhimu. Hii ni kwa sababu, tukatae tusikatae, sekta kadhaa muhimu nazo zina taswira ileile tunayoiona katika sekta ya elimu. Napenda kuchukua fursa hii kuangazia nini kifanyike ili kuhakikisha kuwa serikali inatoa elimu bora na si bora elimu. Katika hili, nisingependa kuwa nyuma kuunga mkono baadhi ya mitazamo ya wanafalsafa walioweza kuitoa kuhakikisha kuwa sekta ya elimu nchini inaboreshwa. Mitazamo hii ni pamoja na ifuatayo:-
*      Kuwatendea haki walio wengi ambao tunajua kuwa hawataingia katika vyuo vya elimu ya juu. Hali inaonyesha kuwa ni sehemu ndogo tu ya watoto wanaoingia shule za msingi ndio wanaopata nafasi ya kuendelea hadi Chuo Kikuu.  Tujenge mifumo ya elimu na mitaala itakayowafanya watoto wa nchi hii wawe na manufaa kwa jamii zao; watoto wa wakulima wafundishwe kilimo bora, watoto wa wafugaji wajifunze ufugaji bora, n.k.
*      Tuwekeze kwa dhati kwa kutenga rasilimali za kutosha na kuwekeza katika tafakuri ya pamoja katika shule za umma na kuzifanya ziwe na ubora wa hali ya juu kiasi kwamba isiwepo haja ya wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi, ambazo ni za gharama kubwa zaidi.               
*      Shule ifundishe sayansi, hisabati na lugha. Lakini pia ifundishe maadili mema ili kujenga raia wema. Sayansi, teknolojia, hisabati na lugha ni nyenzo muhimu katika makuzi ya kijana. Lakini iwapo nyenzo hizo hazitaambatana na mafunzo na malezi ya uungwana ipo hatari watazitumia nyenzo hizo katika uhalifu.
*      Watoto wafundishwe na watiwe shime ya kufanya tafakuri ya kiudodosi (‘critical thinking’). Aidha, vijana wa Tanzania wafundishwe kujiamini, kutafakari na kusema kwa sauti kile wanachokiamini. Pamoja na maadili, watoto pia wafundishwe kupenda vitu vizuri ikiwa ni pamoja na umaridadi, michezo na sanaa ikiwa ni pamoja na muziki na ushairi kama sehemu ya ujenzi wa jamii ya watu wanaopenda mazingira wanayoishi maisha ya siha na furaha. Elimu inayomfunza mtoto hisabati lakini haimfundishi namna ya kuvaa vizuri, kula kwa staha na kuongea kwa ufasaha katika lugha anayoheshimu hadhira inaunda roboti na si binadamu.
*      Suala la ubora wa elimu ya walimu liwe nambari moja kwa sababu bila walimu bora, yote mengine tunayoyafanya, kama vile ujenzi wa majumba, n.k. ni upuuzi. Walimu watokane na wahitimu wenye ubora wa juu kuliko wengine, watambulike kwa uwezo wao mkubwa katika masomo yao, waandaliwe vema, walipwe mishahara mizuri na wapewe marupurupu wanayostahili…
Hebu itazame nukuu ya hotuba yako hapo juu. Hayo yalikuwa ni mawazo yako katika Bunge Kivuli miaka miwili iliyopita. Sina hakika ni wangapi hutoa mawazo ya aina hiyo katika Bunge uingialo ambalo ajenda yake kuu ni ‘mipasho na miposho’. Ulitaka tujitazame kama jamii, tusiangalie tulipoangukia bali tuchunguze tulipojikwaa. Ulisisitiza kuwa maendeleo hayapimwi kwa vitu bali ubora wa maisha ya watu. Ulitaka tufanye tafakuri ya kina kama jamii na kufikia mwafaka wa jamii tuitakayo. Ulisisitiza tufanye mabadiliko ya kimfumo yatakayojenga taasisi zenye kujali maslahi ya wengi.

Naamini utajinoa zaidi kinadharia ili usiwe mbwabwaja maneno kwa kuchukulia matatizo yanayozalishwa na mfumo wa kinyonyaji tulioukumbatia, kuwa mtaji wako wa kisiasa. Naamini utakinoa chama chako ili kijitaje kinadharia na kivitendo, je, umma kinaoupigania ni umma gani? Je, umma huo utakombolewa na itikadi/dira gani? Je, umma huo utakombolewa na nani? Je, ni miiko ipi inapaswa kutawala maisha ya viongozi na wanachama?

Ngoja nikutolee mfano: TANU na CCM ya mwalimu Nyerere ilichagua umma wa wanyonge [wakulima na wafanyakazi] huku itikadi yake ya ukombozi ikiwa Ujamaa. Pamoja na mapungufu kadhaa ya utekelezaji wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, wananchi wetu bado wanalikumbuka Azimio la Arusha na kusema: ‘Azimio lilitujali!’ Hata juzi machinga walipofukuzwa katika eneo la Ubungo, ambapo huuza bidhaa zao wakati wa jioni, waliimba: ‘Kama sio juhudi zako Nyerere, na amani ingetoka wapi?’ Wanatambua kwamba amani ni tunda la haki; amani hupatikana kwa kujenga mfumo unaojali maslahi ya wengi. Ndivyo alivyofanya Mwalimu.

CCM ya sasa pia ina umma wake –  wawekezaji-papa na wafadhili – na itikadi yake ni uliberali mambo-leo [soko huria]. Machinga, wakulima wadogo, wachimbaji wadogo, mama ntiliye n.k. sio umma wa CCM. Wao ni uchafu, sio injini ya maendeleo katika soko huria. Ndio maana hunyang’anywa ajira zao, hunyanyaswa na kusukumwasukumwa ovyo. Huporwa hata kile kidogo walicho nacho. Hivyo haishangazi, wakati wananchi wakilalamika kwa hali ngumu ya maisha,  watawala huwashangaa huku wakisema, ‘huko nje tunasifiwa’.

Najua unajiandaa na sherehe ya kuapishwa. Naomba nikugawie kipande cha keki niliyopewa na Prof. Shivji wakati nikihitimu shahada ya kwanza mwaka 2011. Ni keki isiyoisha, isiyooza, isiyopungua utamu:

Maisha sio porojo
Za siasa na Abunuwasi.
Maisha sio uhondo
Wa dhahabu na almasi
Maisha sio uhongo
Wa ufisadi na uchoyo
Wa mali na madaraka.
Maisha ni kuishi
Kuishi uhai wa walalahoi.

Maisha ni kujitolea
Mhanga wa ukombozi
Ukombozi wa kitabaka
Tabaka la wanyonywaji
Tabaka la wanyanyaswaji.
Nakutakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yako.

Wasalaam,
Sabatho Nyamsenda,
Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
6/4/2012.


No comments:

Post a Comment