04/05/2009

Rostam Aziz aendeleza Libeneke lake na Reginald Mengi

Mbunge wa Igunga (CCM), Rostam Aziz

VITA ya maneno inayohusisha mapambano dhidi ya ufisadi aliyoianzisha Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi wiki iliyopita, sasa imeanza kuibua masuala mapya.

Katika hali ambayo haikutarajiwa, mmoja wa wafanyabiashara watano ambao aliwatuhumu kwa kile alichokiita ufisadi papa, jana aliibuka hadharani na kutoa tuhuma nzito dhidi yake, akimhusisha na vitendo mbalimbali vya ufisadi alivyodai vimechangia katika kuwafanya Watanzania kuwa maskini zaidi.

Mfanyabiashara huyo wa kwanza kujitokeza hadharani kujibu tuhuma hizo za Mengi, ni Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), ambaye mbali ya kumshambulia Mengi akimhusisha na tuhuma za aina tofauti za ufisadi, alikanusha madai yote dhidi yake.

‘‘Kwanza nataka niweke wazi kwamba tuhuma zote zilizotolewa na Mengi dhidi yangu ni za uongo na ni upuuzi mtupu. Tuhuma hizo ni mwendelezo wa wimbo ule ule ambao amekuwa akiuimba kwa muda mrefu sasa, na tayari nilikwishazitolea kauli huko nyuma,” alisema Rostam ambaye baadaye alikana kuhusika kwa namna yoyote katika kashfa za EPA, Richmond na Dowans.

 Rostam ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, vikao vyenye nguvu kubwa ndani ya chama hicho, mbali ya kukanusha tuhuma hizo dhidi yake, aliwasilisha mlolongo wa kihistoria na vielelezo vinavyojumuisha barua za benki na za taasisi tofauti kueleza namna Mengi alivyojihusisha katika vitendo tofauti vya ufisadi vilivyolitafuna taifa.

Sambamba na hilo, Rostam ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Kibo katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, jijini Dar es Salaam alimuelezea pia Mengi kuwa kinara wa harakati za kumchafua yeye na watu wengine ambao ni washindani wake wakubwa wa kibiashara.

 

Rostam ambaye pia ni mfanyabiashara mwenye hisa katika kampuni za ujenzi, mawasiliano ya simu na habari, alitumia fursa hiyo kutamka hadharani kwamba alikuwa akikusudia kuwasilisha katika vyombo vya dola mlolongo wa tuhuma za ufisadi dhidi ya Mengi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi kabla ya hatua dhidi yake kuchukuliwa.

‘‘Nimetafakari kwa kina athari zinazoweza kulifikia taifa letu, ikiwa mwenendo wa watu kama Mengi wa kujipa haki ya kuchafua wale anaowaona kuwa ni washindani wake utaachiwa uendelee, na hasa kutokana na sumu mbaya iliyomo katika maelezo anayoyatoa na malengo anayoyakusudia kwa kutoa maelezo hayo,” alisema Rostam.

 

Huku akitaja tuhuma moja baada ya nyingine zinazomhusisha Mengi na ukopaji wa mabilioni ya fedha na aliyoshindwa kuyalipa kwa njia ya kuua kampuni alizotumia kukopa, Rostam aliielezea hatua hiyo ya mfanyabiashara huyo kuwa ni ufisadi mbaya.

Alipoanza kutaja tuhuma hizo, Rostam ambaye alionyesha kukerwa na kitendo cha Mengi kuwapachika yeye na wafanyabiashara wenzake jina la mafisadi papa, alikwenda mbele na kumuita mgomvi wake huyo ‘nyangumi wa ufisadi’.

‘‘Nimeamua kuitisha mkutano huu ili kuwaeleza, na kupitia kwenu kuwaelewesha Watanzania wamjue Reginald Abraham Mengi katika sura yake halisi na dhamira zake chafu na ovu, na kumtambua kwamba huyu ni nyangumi wa ufisadi,” alisema Rostam ambaye alidai Mengi alikuwa amejiteua mwenyewe kuwa msemaji wa wananchi pasipo kupigiwa kura na mtu yeyote.

Katika madai yake hayo, Rostam aliihusisha iliyokuwa Kampuni ya Anche Mwedu ambayo Mengi alikuwa ana hisa, kuwa mfano wa kampuni ambazo mfanyabiashara huyo alizitumia kukopea mabilioni katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na akashindwa kuzirejesha kwa njia ya kuiua kampuni hiyo.

‘‘Hivi ndivyo Mengi alivyochangia kuifilisi NBC, benki ya wananchi maskini wa Tanzania. Fedha hizi zilizochukuliwa shilingi bilioni 28 zinaweza kujenga shule za sekodari 100,” alisema.

Hakuishia hapo, alizitaja kampuni nyingine kadhaa alizosema pia zilikuwa ni za Mengi ambaye aliamua kuziua kwa sababu hizo hizo za ama kukataa kulipa madeni, kukwepa kulipa kodi na wakati mwingine kushindwa kuziendesha.

Katika orodha ya kampuni hizo, alizitaja Anche Mwedu Ltd, Tanpack, Tissue Industries Ltd, Chemical Industries, Bodycare Ltd na Medicare Ltd.

‘‘Hebu tujiulize ni kwa nini Mengi anaua kampuni zake halafu anatafuta mchawi kwa wale waliofanikiwa? Bila shaka ameziua kampuni hizo kwa lengo la kukwepa kulipa kodi na kulipa madeni, mambo ambayo ni ufisadi mkubwa. Binafsi sina mchezo wa aina hiyo,” alisema Rostam.

Mbali ya hilo, alimhusisha Mengi na tuhuma za kutolipa madeni ya fedha za wafadhili zilizotolewa katika mpango maalum wa kuwasaidia wafanyabiashara kuagiza biadhaa nje kwa fedha za mkopo (Commodity Import Support).

Katika hili, Rostam alifikia hatua ya kumhusisha Mengi na tuhuma za kushirikiana na ofisa mmoja wa Wizara ya Fedha ili kumwandalia barua inayoonyesha alikwishalipa deni hilo, kinyume na ulivyo ukweli halisi.

Rostam aliyekiri kwamba naye alikopa fedha hizo na kuwa anaendelea kuzilipa, alisema hatua ya kampuni zinazohusishwa na Mengi kutolipa madeni ni ya kuwaongezea Watanzania umaskini ambao siku zote amekuwa akidai kuwapigania.

Nje ya tuhuma hizo za ufisadi, aligeukia kile alichokiita tabia ya Mengi kupenda kuendekeza ugomvi dhidi ya watu mbalimbali kwa lengo tu la kulinda maslahi yake.

Katika hili alitoa mifano mingine 11 tofauti ya kihistoria akionyesha namna Mengi alivyojenga tabia ya kukabiliana kwa namna ya ugomvi na watu au taasisi kwa malengo hayo hayo binafsi.

Katika hili, Rostam alirejea mizozo iliyopata kumhusisha mfanyabiashara huyo kwanza na wamiliki wa televisheni ya DTV, aliyekuwa Waziri wa Nchi (Utawala Bora), Wilson Masilingi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Shamim Khan na kisha aliyekuwa Waziri wa Nchi (Mazingira), Edward Lowassa wote wakati wa serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa.

Huku akifafanua ugomvi wa kila mmoja wa watu hao na Mengi, aliendelea kueleza namna mfanyabiashara mwenzake huyo alivyogombana na aliyekuwa Waziri wa Fedha enzi hizo hizo, Basil Mramba, wamiliki wa zamani wa Kampuni ya Habari Corporation, Mbunge wa Mkurunga, Adam Malima na baadaye Tanil Somaiya.

Katika orodha hiyo hiyo ya mlolongo wa ugomvi wa Mengi na watu mbalimbali, Rostam akawataja pia mfanyabiashara Yussuf Manji, Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kabla hajamrukia yeye mwenyewe.

Rostam alirejea tena wito wake wa kuwataka wale wenye ushahidi wa tuhuma za ufisadi dhidi yake kuufikisha mbele ya vyombo vya dola badala ya kuendelea kumchafua mitaani.

Mfanyabiashara huyo alisema muda mrefu, kabla ya tukio la wiki iliyopita la Mengi kuwaita yeye, Tanil Somaiya, Jeetu Patel, Shubash Patel na Yussuf Manji kuwa mafisadi papa, tayari alikuwa ameshaanza kuwa na hisia za kumhusisha mfanyabiashara huyo na kile alichokiita kampeni chafu za kuwachafua baadhi ya watu akiwamo yeye.

‘‘Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita nilipata taarifa kwamba ni Mengi ndiye aliyekuwa akiendesha na kusimamia kampeni ya kunisakama kwa kupika na kusambaza habari zote chafu zilizolenga kunichafua. Nilipoonana naye kumueleza juu ya taarifa hizo, si tu aliruka sana, bali pia aliapa kwa jina la mama, mke na mtoto wake kwamba hahusiki kabisa na kampeni hizo na kwamba hata yeye anakerwa,” alisema Rostam.

Chanzo cha habari hii kilipowasiliana na Mengi ili kupata maoni yake kutokana na hatua hiyo ya Rostam kuelekeza tuhuma nzito za ufisadi dhidi yake, hakuwa tayari kusema kwa urefu zaidi ya kusema alikuwa na ujumbe mfupi wa maandishi uliokuwa na majibu yake.

Chanzo hiki kilifanya juhudi za kumfikia Mengi na kupata taarifa yake hiyo fupi ambayo ilisainiwa na yeye mwenyewe kwa saini inayofanana na ile iliyoko katika baadhi ya nyaraka zilizowasilishwa na Rostam kama ushahidi wa tuhuma dhidi yake.

‘‘Mafisadi papa wana uwezo mkubwa sana, sio tu wa kuiba mali za umma, bali hata wa kutunga uongo kama alivyofanya Rostam Aziz leo (jana Jumapili),” alisema Mengi ambaye alipotakiwa kufafanua alisema ulikuwa ukijibu kila alichokisema mbunge huyo.

Badala yake, Mengi alisema anampa Rostam ushauri wa bure wa kwenda mahakamani kwa lengo la kuondokana na shutuma za ufisadi anazokabiliana nazo.

Alihitimisha majibu yake kwa kusema: ‘‘Hata baada ya kukutana na waandishi wa habari leo, hoja ya kushutumiwa kama fisadi papa inabaki pale pale. Watanzania wanasubiri kwa hamu kubwa kusikia kwamba Rostam amekwenda mahakamani kwa sababu wengi, hasa wanyonge wana hasira nyingi dhidi ya ufisadi.”


Wadau, mpaka hapa nani msafi na nani fisadi? Nini hatima ya libeneke hili na lina faida yoyote kwa watanzania, hasa wale masikini wanaoishi bila uhakika wa kuifikia kesho?

1 comment:

  1. Kusema ukweli ni kwamba shutuma za mengi zina maana sana kwangu mimi, kwa kuwa Bwana Mengi ni mpambanaji na kama ni mpambanaji ni lazima awe msafi kwanza,na ili ndo jambo ambalo Bw.Rostam ambalo alikuwa analionesha siku ya jumapili, ila swali ni kwamba alikuwa wapi? na kwa nini sasa?.Kusema ukweli ni kwamba ameamua kumchafua mwanzake sasa kwa kuwa Bw.Mengi kamchafua. Ila kama kuna uwezekano wa Bw.Mengi kuhusika kwa namna moja au nyingine katika shutuma zilizotolewa na mbunge wa igunga ni lazima ashutumiwe. Ndugu zangu kuna mambo mengi ambayo ni lazima tujiulize sisi wabongo,ila kwa leo nauliza maswali mawili tu serikali ya KIkwete ni chafu kama serikali ya mkapa na hii ni hadi viongozi wake, ni kwanini Bw.mengi anazidi kumsifia Jk kwamba ni kiongozi bora,wakati uzembe wake umesababisha nchi kuingia katika kiza cha buzwagi na richmond? na kwa nini Bw.Mengi amekuwa sabuni ya ikulu ya Dar es salaam?,ndugu zangu naomba mnisaidie hapo.

    ReplyDelete