04/11/2009

Barua ya wazi kwa Mheshimiwa Mkapa

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa (kushoto) akiwa na Rais wa Finland, Tarja Halonen


Mwanasosholojia amefurahi kuisoma barua ya wazi ambayo Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Issa Shivji ameandika kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania, Mheshimiwa BenjaminWilliam Mkapa. Ni hii hapa...

Mheshimiwa Mkapa,

Assalam Alaykum.

Nakuamkia kwa heshima na taadhima. Natumai u mzima wa afya, wewe na familia yako. Nakuombea kila la heri na mapumziko mema, pamoja na majukumu yako mengi na mazito ya kimataifa.

Mheshemiwa, nimeshawishika kuandika barua hii baada ya kusoma kwenye tovuti (http://businessmirror.com.ph/home/opinion/14843-the-sudden-demise-of-neoliberal-economics.html) maoni yako ambayo yamenukuliwa na mwandishi wa habari Roberto Savio akiandika juu ya kifo cha uliberali mamboleo katika gazeti la Business Mirror la 19 Agosti 2009. Umenukuliwa ukisema:

“We privatized everything the state had. Everything was bought by foreign capital because we had no national capital to compete. The foreign companies almost always closed local businesses, which were not competitive, transforming them into distributors of foreign products and driving up unemployment. The experts of the World Bank and the IMF predicted that this would happen, but they told us: Now the influx of foreign investment will lead to the creation of new, competitive and technologically current businesses that will provide the foundations for a lasting, modern development. None of this happened for us.”

“Tulibinafsisha kila kitu kilichokuwa mikononi mwa dola. Kila kitu kilinunuliwa na wawekezaji kutoka nje kwa sababu hatukuwa na mtaji wa ndani wenye uwezo wa kushindana. Makampuni ya nje yakafunga mashirika ya ndani kwa sababu hayakuwa na tija na yakayageuza mashirika haya kuwa wachuuzi wa bidhaa kutoka nje na kwa hivyo kuongeza watu wasio na ajira. Wataalam wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa walitabiri kwamba hivyo ndivyo ingekuwa, lakini wakatuambia: Uwekezaji kutoka nje utazaa taasisi za kibiashara za kisasa, zenye uwezo wa kushindana, na teknologia ya kisasa, na kwa hivyo kujenga misingi ya kudumu ya maendeleo ya kisasa. Hakuna lolote kati ya hiyo lililotokea nchini mwetu”.

Mzee, unasononeka; kwa kiasi fulani, katika lugha yako ya kidiplomasia, unalalamika. Lakini hata baada ya maanguko ya mfumo wa uliberali mamboleo na utandawazi, ambao uliushabikia sana wakati wa utawala wako, hukuwa na ujasiri wa kuomba msamaha wa watu wako. Sikulaumu. Huwezi kulaumiwa. Ni hulka ya binadamu kutokuona au kukiri kosa lake. ‘Nyani haioni ngokoye.’ Katika hili huko peke yako. Katika mkutano wa kundi la nchi 20 (G20) zenye nguvu za kiuchumi ulioitishwa mjini London kuzungumzia hali mbaya ya uchumi mnamo Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu wa Uingereza, Bwana Gordon Brown, alikiri kwamba ‘Muafaka wa Washington umekufa’, alisema hivyo bila kuwaomba radhi watu wa ulimwengu, hasa wa nchi maskini, ambao waliathirika sana na “muafaka” huo wa nchi za kibeberu ambao nchi zetu zililazimishwa kuufuata.

Mheshemiwa Rais mstaafu: Ukweli ni kwamba haya yaliyotokea sasa si matokeo yaliyokuja kwa bahati mbaya au kwa miujiza tu. Wako viongozi na hasa wasomi (angalau wachache) walisema, tena kwa uchambuzi wa kina na yakinifu, kwamba mfumo huo hautufai, hautatuletea maendeleo, bali utauongeza tu unyonywaji wa watu wetu na uporwaji wa mali zetu. Mwalimu Nyerere alijitahidi sana kupinga masharti ya nchi za kibeberu, lakini hakufanikiwa. Mzee Mwinyi alifungua milango na wewe ukakumbatia, bila kuhoji mfumo huo, hasa masharti yale ya kubinafsisha mashiriki ya umma. Ni kweli mashirika mengine hayakuwa na tija, ni kweli pia mengine yalikuwa na menejimenti mbovu. Lakini je, tulijaribu kutafuta njia mbadala, licha ya hiyo ya kubinafsisha ‘kila kitu’? Wasomi wako wachache waliokosoa sera zako za kiuchumi uliwaita majina na kuwafananisha na ‘wavivu wa akili’. Ulipigia sana debe utandawazi kiasi kwamba jina lako litaingia katika historia kama mvumbuzi wa neno ‘utandawazi’ katika msamiati wa Kiswahili. Uliwafumbia macho viongozi wako wakati wakitumia vyeo vyao kujilimbikizia mali na utajiri wa kupindukia – au hili pia ilikuwa ni sera ya kujenga mabepari wa ndani?

Mbaya zaidi, mheshimiwa, chini ya uongozi wako tukakubali kutoa uhuru kwa taasisi za kifedha, na kukubali soko huria katika biashara ya fedha, (na kutokudhibiti akaunti ya mtaji (capital account)) bila udhibiti na usimamazi wowote wa dola. Hili ndilo hasa lilikuwa chanzo cha chumi zetu kuathirika kupita kiasi pale anguko la mfumo wa fedha wa kimataifa lilipotokea.

Nchi ambazo zilikataa soko huria katika mambo ya fedha, kama China na Malaysia, hazikuathirika kama nchi zingine. Naomba nisiendelee. Wananchi wetu, pamoja na kutokuwa na usomi au ustaarabu wako au wangu, wanahisi moyoni mwao udhaifu wa mfumo wa utandawazi na binamu yake uliberali mamboleo. Ndio maana wakati wa kuadhimisha miaka kumi tangu kifo cha Mwalimu, wakalilia sana Azimio la Arusha.

Mwalimu hakuwa malaika, alikuwa kiongozi wa kisiasa. Alikuwa na mapungufu yake lakini alijali watu wa chini, watu ambao walisahaulika kabisa katika awamu ya tatu na wanaendelea kupuuzwa katika awamu ya nne. Kila mlalahoi aliyetoa maoni yake alikuwa na maneno haya tu: Mwalimu alitujali; Azimio la Arusha lilitujali sisi wanyonge. Azimio lilitoa matumaini. Uliberali mamboleo na utandawazi ulitoa matumaini yapi kwa matabaka ya chini, zaidi ya kuwa njia ya viongozi kujilimbikizia mali bila aibu!

Mheshemiwa Rais mstaafu, sio nia yangu kurudia yale yaliyotokea. Lakini, utakubaliana nami kwamba historia ni muhimu. Kujifunza kutokana na historia yetu na ya wengine ni hatua ya kwanza katika safari ndefu ya kujikomboa na kujiletea maendeleo halisi. Kama kweli umejifunza na umeyaona madhara ya sera ulizozikumbatia wakati ukiwa madarakani, je, huoni kwamba una wajibu wa kumsaidia mrithi wako, na hasa kutusaidia sisi wananchi, ili tujifunze kutokana na makosa ya serikali yako? Je, kweli, bado unanadi na kutunasihi kwamba utandawazi hauepukiki? Je, bado unatushauri kwamba msukumo wa maendeleo ni uwekezaji kutoka nje, uwekezaji ambao umejidhihirisha wazi ni uporaji wa maliasili yetu? Je, huoni kwamba unao wajibu, kwa upande wako, wa kufanya kila iwezekanayo – na wewe sio mtu mdogo katika nchi hii – kutusaidia kuzindua mjadala wa kitaifa juu ya hatma ya nchi yetu na bara letu?

Wasalaam,

Issa Shivji

Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Okotoba 24, 2009

25/10/2009

Kuna Asiyependa Kwao?

Leo nikiwa njiani narudi nyumbani, hapa uwanja wa ndege wa Cork nimepata hamu ya ghafla ya kutunga tungo mbili tatu za kuelezea nyumbani. Pamoja na safari yangu ughaibuni kunichukua kama wiki mbili tu, nilikumiss nyumbani!


Nyumbani ni nyumbani jamani, hata kuwe kwa namna gani
Wahenga hawakuwa punguwani, kuliweka wazi barazani
Hata usafiri kote duniani, utarudi nyumbani mwishoni
Kuna anayesema asilani, Hapendi kwao jamani?


Nimekaa na kuwaza vilivyo, pasingekuwepo nyumbani
Kila kitu kingekuwa hovyo, tungekosa raha duniani
Tungetangatanga visivyo, bila kuwa na maskani
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?


Wasanii nao wanaimba, nyumbani kwako ni nyumbani
Kwa zao tungo wanatamba, luningani na redioni
Ni nyumbani wanakuimba, kumwaga sifaze jamani
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?


Pamoja na umuhimuwe, kuna wengine wakubeza!
Wamejawa na kiwewe, na maisha ya kuigiza
Hawataki kwao kamwe, wanaranda wakibangaiza
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?


Hawa wamejisahau, kutukuza ugenini
Wanasahau nahau, kujiweka utumwani
Kwenda kwao walau, hawawazi akilini
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?


Mwenzenu napenda kwetu, hata nipewe nini,
Siwezi utupa utu, kwa kupenda ugenini
Kwetu kunabaki kwetu, nakupenda kama nini
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?

18/10/2009

Wahi Nakala yako ya Chemchemi

Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Issa Shivji

Kigoda cha Kitaaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu Dar es Salaam kimetoa toleo la pili la Chemchemi lililozinduliwa rasmi na Makamu Mkuu wa Chuo mwezi huu. Toleo hili ni la Kiswahili.

Bodi ya uhariri ya Jarida hilo inabainisha kuwa ndani ya toleo hili mna makala mbalimbali kama vile; Haja na Namna ya Kutoa Elimu ya Uraia Tanzania (Bashiru Ally) Tafsiri na Muhtasari wa Kijitabu cha Hamidu Ismail Majamba Kiitwacho 'Uwezekano na Mantiki ya Kuanzisha Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara (Aldin Mutembei), Edward Moringe Sokoine na Mapinduzi Vijijini (Issa Shivji) na kadhalika. Pia kuna makala ya Dkt. Mwami juu ya Ulimbikizaji wa Mtaji kwa Unyang'anyi Chini ya Ubeberu Nchini Tanzania (kwa taarifa ya ziada: Dkt. Mwami anakaribia kumaliza tafsiri ya Das Kapita kwa Kiswahili!)

Vile vile toleo hili lina mazungumzo marefu kati ya Shivji na Kingunge Ngombale Mwiru yaliyoandaliwa na Jacquiline Mgumia. Katika mazungumzo haya Ndugu Ngombale Mwiru anazungumzia maisha yake ya kisiasa tokea alivyojiunga na TANU miaka ya 1950, jinsi alivyokwenda kusoma Liberia na kwanini alikimbia Liberia na kwenda kusoma Dakar, Senegal na kadhalika. Shivji anamdodosa Ngombale jinsi CCM ilivyotoa Mwongozo wa mwaka 1981 wenye uchambuzi wa kitabaka chini ya Mwalimu Nyerere ilhali Mwalimu alikuwa hakubaliani na mtizamo wa kitabaka. Na je, Ndugu Ngombale anateteaje "Azimio la Zanzibar" wakati yeye bado ni muumini wa Ujamaa?

Mazungumzo mengine ni juu ya Muungano wa Tanzania kati ya Shivji na Ismail Jussa (CUF), Bakari Mohamed (Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala CKD), Ng'wanza Kamata (Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala CKD, Chris Peter (Shule ya Sheria), Bernadetha Killian (Shule ya Uandishi wa Habari) na Adolf Mkenda. Mambo makuu mawili yanajadiliwa, chimbuko la muungano na muundo wa muungano.

Pia kuna mapitio ya kitabu cha Mohamed Said (kilichotafsiriwa na A.S. Mkangwa). Kitabu hiki kinaitwa "Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924-1968): Historia Iliyofichwa Kuhusu Harakati za Wailsam Dhidi ya Ukoloni wa Waingereza Katika Tanganyika" Mpitiaji wa kitabu Adolf Mkenda.

Toleo hili lina pia CD ya wimbo wa kusisimua wa Karola Kinasha- wimbo alioutunga mahsusi kwa ajili ya Wiki ya Tamasha la Kitaaluma la Mwalimu Nyerere na kuuimba kwa mara ya kwanza kabisa pale Nkrumah. Waliokuwepo pale Nkrumah watakumbuka jinsi wimbo huu ulivyoshangiliwa na kusisimua. Karola amekubali CD hii iambatane na kila toleo la Chemchemi bila kudai malipo yeyote.

Mwisho, toleo hili lina pia kumbukizi ya Haroub Othman iliyoandikwa na Chris Peter na shairi lililotungwa na Shivji. Beti kadhaa za shairi la Mwalimu Nyerere pia zimechapishwa. Baadhi ya beti hizo ni hizi hapa;


1.Tanzania yetu ina

Watu aina aina:

Inao hao Wapemba

Watochomewa majumba,

Sera hii ikipita

Bila ya kupigwa vita.


2.Lakini ina Wahaya,

Na Wasumbwa na Wakwaya,

Ina Waha na Wamwera,

Na Wakwavi, na Wakara.


3.Ina Anna ina Juma,

Ina Asha ina Toma,

Kadhaka ina Pateli,

Na wengine mbali mbali.


4.Uhasama ukipamba

Mkafukuza Wapemba,

Anajua ni Manani

Mbele kuna mwisho gani.


Jipatie nakala yako kutoka kwa Walter Luanda (0754 281 837)

Taarifa hii ni kwa hisani ya Dkt. Adolf Mkenda wa idara ya uchumi, Chuo Kikuu Dar es Salaam

17/10/2009

Unapokutana na Mdau Ughaibuni


Mwanasosholojia amepata bahati ya kukutana na mdau rafiki yake wa siku nyingi Nyangusi Ndukai, wakati wa mkutano wa kimataifa wa Sustainable Global Development unaoendelea kufanyika chuo kikuu cha Limerick, Ireland. Nyangusi kwa sasa amehitimu shahada yake ya Uzamili katika fani ya Maendeleo ya Jamii katika chuo cha Kimmage Manor. Kwa pamoja wanahudhuria mkutano huo unaowakutanisha washiriki kutoka sehemu mbalimbali duniani wakijadiliana mambo yahusuyo maendeleo. Mwanasosholojia yeye aliwasilisha mada yake jana.

02/10/2009

Jibu la Kitendawili cha Mroki

Nimepata walau kadakika kamoja ka kumjibu Kamarade Mroki kwa tungo mbili tatu kufuatia swali lake juu ya mwenye mamlaka kati ya kondakta na dereva.

Mroki malenga wetu, salamuzo nimepata

Nakujibu mwanakwetu, nipo safi pasi tata

Ulichokiuliza kwetu, jibu lake utalipata

Mwenye mamlaka dereva, kondakta ni msaidizi


Kondakta ni msaidizi, mwenyewe umeonesha

Wala hafanyi ajizi, vituoni kutushusha

Hata kupiga uluzi, dereva kumgutusha

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi


Dereva ndiye mwamuzi, gari kulisimamisha

Anaviruka vihunzi, abiria kuwafikisha

Kumsikiliza msaidizi, ukweli si kubadilisha

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi


Anashika usukani, gari kuliongoza

Anapokuwa barabarani, kulipoza na kukoleza

Breki zi miguuni, aweza kuzichokoza

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi


Hakuna ubishi malenga, anayo mamlaka

Anaweza kukutenga, asisimame Malampaka

Matusi ukimlenga, atakuvukisha mpaka

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi


Nilipata walau dakika, Kamarade nimjibu

Naweza tena andika, kwa sababu ni wajibu

Ila ninayo hakika, ataridhishwa na jibu

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi

01/10/2009

Mroki na Kitendawili cha Dereva na Konda!


Kamarade Mroki amerusha swali kupitia tungo. Anauliza juu ya mwenye mamlaka kati ya dereva na kondakta. Maswali yake yanatiririka namna hii;

Wabilahi tawafiki, nyote nawasalimuni,
Nyote msio na chuki, habarari za nyumbani,
Sibagui marafiki, na mlio ofisini,
Kondakita na dereva, nani mwenye mamlaka.


Nani mwenye mamlaka, dereva na kondakita,
Mtu akitaka shuka, tamtafuta kondakta,
Dereva utamruka,mlango utaufata,
Kondakta na dereva, nani mwenye mamlaka.


Breki ipo kwa dereva, unaanza muita konda
We konda shusha Kizava, njiapana kihonda,
Kazi hiyo ya dereva, vipi wamuita konda,
Kondakita na dereva, nani mwenye mamlaka.


Yamkini upo mbele, siti karibu na suka,
Inakutoka kelele,eti unatakashuka,
Ukae kiti cha mbele,kituo muite suka,
Kondakita na dereva, nani mwenye mamlaka.


Konda atakuitika, kisha tamjuza suka,
Shusha mmoja kafika,siunge mwambia suka,
Breki huzifinga suka, kituoni ukifika,
Kondakita na dereva, nani mwenye mamlaka.


Konda hukusanya fedha, ndo yake kazi muhimu,
Hujiongezea adha, na wingi wa majukumu,
Kuwaita abiria, askari kwa walimu,
Kondakta hastahili, kulisimamisha gari.


Dereva anastahili, kulisimamisha gari,
Hata matuta mawili,suka talizima gari,
Yupo makini kwahili,muonapo msafiri,
Kondakta hastahili, kulisimamisha gari.


Mwisho ninamalizia, kituoni nimefika,
Kitini sikusinzia,siokwamba sijachoka,
Jibu nasikilizia,sote weze faidika,
Kondakta hastahili, kulisimamisha gari.



Mtunzi: Mroki Mroki (Father Kidevu)
"Bepari wa Kikamba"
Box 9033, Dar es Salaam
Email. mrokim@gmail.com
+255 7171 002303
Tanzania.


Haya wadau, mwenye majibu anakaribishwa, nafikiria fikiria kumjibu huyu mtunzi

Kwa Wapendao kwenda Marekani

Kaka Makulilo mdogo (Jr) amepata chansi ya kuliona tangazo linalonadi bahati nasibu ya kwenda Marekani na kulirusha kwa Mwanasosholojia. Linasomeka hivi kwa kimombo;

2011 Diversity Visa Lottery Program (GREEN CARD) Starts 2nd October, 2009

The Department of State announces the opening of the registration period for the DV-2011 Diversity Visa lottery. Entries for the DV-2011 Diversity Visa lottery must be submitted electronically between noon, Eastern Daylight Time (EDT) (GMT-4), Friday, October 2, 2009, and noon, Eastern Standard Time (EST) (GMT-5), Monday, November 30, 2009. Applicants may access the electronic Diversity Visa entry form (E-DV) at www.dvlottery.state.gov during the registration period. Paper entries will not be accepted. Applicants are strongly encouraged not to wait until the last week of the registration period to enter. Heavy demand may result in website delays. No entries will be accepted after noon EST on November 30, 2009.

Important Notice

No fee is charged for the electronic lottery entry in the annual DV program. The U.S. Government employs no outside consultants or private services to operate the DV program. Any intermediaries or others who offer assistance to prepare DV entries do so without the authority or consent of the U.S. Government. Use of any outside intermediary or assistance to prepare a DV entry is entirely at the entrant’s discretion.
FOR DETAILS ON GREEN CARD AND SCHOLARSHIPS - VISIT
MAKULILO, Jr.
San Diego, CA

Haya tena wadau mnaopenda kwenda Marekani, changamkieni pande hili!

22/09/2009

Eti hizi ni Sababu 37 za Mwanaume Kuamua Kuoa!


Hutokea mtu kujiuliza sababu hasa zinazopelekea kuamua kuoa/ kuolewa, hususani kwa wale wanaofuatilia mijadala ya ndoa, na hata wale walioamua kukata shauri kuishi maisha ya kikapera. Wachambuzi wa mambo ya mahusiano na ndoa wanasema kuwa kuna sababu zisizopungua 37 zinazopelekea mwanaume kuamua kuoa. Haiwezekani ikawa ni sababu zote, la hasha! Ila wanasema miongoni mwa hizo 37 lazima kuna ambayo/ ambazo zinapelekea uamuzi wa kuoa.

1. Kuwa na mwenzi wa maisha
2. Amempata mpenzi wa kweli
3. Ni muda muafaka kuoa
4. Umri unakimbia...anaukimbilia uzee
5. Ana nyumba kubwa na yupo peke yake
6. Ana watoto aliozaa na mke wa awali na hana msaidizi wa kuwatunza
7. Anahitaji msaidizi wa kazi za ndani wa kudumu
8. Ana pesa nyingi na muda
9. Amechoshwa na mke/ wake alionao
10. Dini inamruhusu kuoa

11. Anahitaji mtu wa kumzalia watoto
12. Mkewe wa awali ni tasa
13. Amekuwa mkubwa na anahitaji mwenye umbo la umama ili amtunze
14. Anahitaji kuridhishwa kimapenzi
15. Wazazi wake wamemlazimisha kuoa
16. Anaona wenzake wa rika moja wanamwacha nyuma kwa kuoa...anawakimbilia
17. Hawezi kupika, anakula hotelini na kwa mama ntilie...anahitaji mpishi nyumbani
18. Hawezi kusema hapana kwa kuwa mama wa mchumba wake ameshaanza kufanya maandalizi, amelipia ukumbi na kuwaarifu ndugu, jamaa na marafiki wote
19. Mchumba ni tajiri sana
20. Baba wa mchumba ni tajiri sana

21. Baba wa mchumba anafanya biashara na anayetaka kuoa
22. Anataka kumjali kwa ukaribu anayemuoa maisha yake yote
23. Mchumba anampenda sana na anaweza kufa ikiwa hatamuoa
24. Anaoa ili wazazi wake waache kupiga makelele kumuhimiza
25. Anaoa kwa kuwa wazazi wake wanamsifia mchumba wake kuwa ni mrembo
26. Anaoa kwa kuwa amempa rafikiake ujauzito
27. Anaoa kwa kuwa anaogopa kuuawa na baba wa aliyempa ujauzito
28. Anaoa ili mchumbake apate uraia
29. Anaoa kwa kuwa ni rafikake wa toka udogoni
30. Anaoa kwa kuwa mwanamke ameapa kutomwacha maishani

31. Anaoa kwa kuwa muda mrefu amekuwa akitaka kuanzisha familia
32. Anaoa ili amalizie maisha yake yaliyobaki na yeye
33. Anaoa ili apate matunzo bora kutoka kwa anayemuoa
34. Anaoa ili mwanamke aweze kutoka kwao na afaidi uhuru

35. Anaoa kwa sababu tu anafikiri anampenda sana
36. Na kwamba anafikiri anapendwa sana
37. Anaoa kwa kuwa ni lazima apitie hatua ya kuoa


Wadau wababa na wakaka; kama hujaoa, sababu zipi kati ya hizo unafikiri zitakupelekea uoe? Kama umeoa, ni zipi zimekupelekea uoe?

Wadau wamama na wadada hali kadhalika, unafikiri utaolewa kwa sababu zipi kati ya hizi, au kuna ukweli kuwa umeolewa kwa sababu yoyote kati ya hizi?

21/09/2009

Wanazuoni changamkieni Tenda hii

Haya tena wanazuoni, jaribuni kutuma maoni katika hii chansi ya "feloshipu", tuendeleze libeneke.

Fellowship for Students from Ghana, Nigeria, South Africa, Tanzania, or Uganda

  • Applicants must be Africans residing and working in Ghana, Nigeria, South Africa, Tanzania, or Uganda.
  • Funding is available for dissertation completion and for postdoctoral research and writing.
  • Applicants for dissertation-completion fellowships should be in the final year of writing the dissertation at a university in Ghana, Nigeria, Tanzania, or Uganda (but not South Africa).
    • Applicants for postdoctoral research/writing fellowships must be working in Ghana, Nigeria, South Africa, Tanzania, or Uganda.
    • Projects must be in the humanities.
    • Projects must be carried out in Africa.

    Application forms and instructions are available on the ACLS website. Printed versions of forms and instructions may be obtained from the African Humanities Program through http://www.acls.org/programs/ahp. ACLS encourages the submission of applications via email; ahp@acls.org



13/09/2009

Kushikiwa bango Kanumba na Ung'eng'e Bongo

Msanii Steven Charles Kanumba

Kwanza napenda kuwataka radhi wadau kwa kimya cha Mwanasosholojia cha takribani miezi miwili. Nilikuwa huko ndani ndani wanakoishi ndugu zangu wadanganyika wenye nia, ambako teknolojia kama hii wanaisikia kwa "bomba" tu.

Baada ya kurudi jijini na kujipanga kuweka kimaandishi nilichokifuata huko udanganyikani, leo nimeona vyema kurudi barazani. Nimefurahishwa na mjadala uliovuma hivi punde juu ya uwezo wa wabongo, hususani wasanii wetu katika kutema ung'eng'e, hasa kufuatia mgeni mwalikwa katika jumba la "Bigibraza", msanii mwigizaji na mwimbaji Steven Kanumba kudaiwa "kuchemsha" katika kubonga ung'eng'e ndani ya jumba hilo.

Si tu vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti suala hili, bali hata wengi wetu tumepokea ujumbe kwa mfupi wa maneno katika simu zetu za viganjani, pengine ukiwa umeongezwa chumvi kwa njia ya kuchekesha (na hata wengine wanasema kudhalilisha) ukielezea jinsi mbongo mwenzetu Kanumba alivyokuwa anachapia kimombo jumbani.

Hapa kuna masuala kadhaa ya kujiuliza, kwa upande mmoja sisi kama watanzania tunapigia upatu Kiswahili kama lugha ya Taifa, na hata kuanza kufanya jitihada za kukitumia katika mikutano mbalimbali (nakumbuka hotuba za viongozi wetu wa juu katika mikutano ya Umoja wa Afrika), lakini kwa upande mwingine lugha ya kiingereza inaendelea kupeta kama lugha ya kimataifa inayotumika katika maeneo mengi.

Ukinzani huu wa ukweli unamlazimisha Mwanasosholojia kutamka kwamba tunapaswa kutukuza utamaduni wetu na kuweka mkazo katika kukuza lugha yetu ya Kiswahili, bila ya kuona aibu kwa wenzetu kwa nini tunatumia Kiswahili. Kutamka hivi kunatokana na ukweli kwamba, kama tunaogopa aibu kwa kuchapia kutumia lugha ya wenzetu tunaweza kufanya mambo mawili; kwanza ni kukomaa kuongea lugha yetu na inapobidi atafutwe mkalimani, pili kama tunaona aibu basi tujifungie na kujifunza kwa bidii huo ung'eng'e ili kutochapia na kuizoa aibu hata miongoni mwetu.

Mgeni anayetumia kimombo kwa mfano akiongea kiswahili cha kuchapia mara nyingi hadhihakiwi, zaidi huelekezwa usanifu wa lugha anayotumia, lakini mswahili akiongea kimombo cha kuchapia huchekwa na hata waswahili wenzake! Hii ni kasumba ambayo imejijenga kwa miongo mingi. Kama Mwanasosholojia alivyoweka bayana awali, hatuna haja ya kuendelea kuchekana na kudhihakiana wakati tuna lugha yetu inapotokea tunajiona hatuna uwezo wa kutumia lugha ya wenzetu. Inashangaza kuona mtu anakomaa kuchapia lugha ye wenzetu wakati anaijua fika ya kwake, labda ni kule kuona aibu kuwa utaonekana hujui kimombo, kwani kimbo si ni lugha tu pamoja na kwamba inakingiwa kifua kimataifa... huu ni utumwa wa kifikra ambao si vyema ukaendelea.

Mjadala huu wa Kanumba ulimpelekea Mwanasosholojia kutafuta undani wa msanii huyu. Yeye anamiliki tovuti, ukiipitia hata tovuti yake unagundua kuwa anatumia King'eng'e "chenye matege", jambo ambalo alipaswa kuliangalia kwa kuamua tu kutumia Kiswahili au kama alitaka aonekane wa kimataifa basi alichoandika alipaswa kumpatia mhariri mwenye ufahamu wa kimombo kilichonyooka, kabla ya kukitundika tovutini. Labda wadau nanyi mpate fursa ya kusoma angalau wasifu wa Msanii Kanumba aliouandika kwa kin'geng'e na kuupachika kwenye tovuti yake;

Steven Charles Kanumba is my name, i was born in a Christian family of 2 girls and i happen to be the last born and the only boy to Mr. & Mrs. Charles Meshark Kanumba. I was given birth on january 8th 1984. I originate from Shinyanga region in Tanzania. I am Sukuma by Tribe. I completed my Primary Education in Bugoyi Primary School in Shinyanga. After Completing my primary education i started my secondary education right away in Mwadui Seminary Secondary School in shinyanga where by i shifted to Dar-es-salaam Christian Seminary Secondary school here in Dar-es-salaam when i was still in form II and complete my O-Level Education there. Thereafter i moved to Jitegemee Sec. School to complete my A. Level Education.

Growing up, acting has always been something that i really liked to do. Apart from that i also liked singing and that made me grave to be an artist while i was still in teens, still in school ie. i started acting in church a lot of people told me i had a talent so i decided to join Kaole Sanaa Group which delt with Acting. After joining Kaole Sanaa Group i met different Teachers from Bagamoyo and other College who helped me to build up my career of Acting for a period of 1 year, after that i got a special Training from University of Dar es salaam Under Doctor Nyoni for about 3 months therefore i was sure to go to work and indulge myself in Soap Operas/Series. i then took acting as my career. Little by little i got to win peoples' attention which made me work even harder and become successful.

After all the hard work that i kept in series i decided to play a part in movies so i took a step forward and associate myself in film industry. i happen to do a lot of movies that did very well in the market and i'm still doing movies up today and it just get better day by day. in addition to this i archieved a lot through my hard work that is prestigious awards, travel across different countries, working with people from different part of the world meeting different people and learn new things and experiencing different life.

I also got to get to work with Nollywood in Nigeria where by i did more than five movies with famous actors from Nolllywood, it was the wonderfull experience. I also got a chance to Visit The United States of America and there is where i got the experience of a lifetime i got visit Hollywood, Warner Bros Pictures, Universal Studios and Disney Land, i learnt a lot i met people who work there so i got to ask alot of Quaestions and gained a lot of knowledge.

Speaking about me as Steven Kanumba i'm a very down to earthguy i like hanging out with my friends and i like to associates myself with people, i love children with all my life, i'm just a simple guy, i'm not outgoing a lot, i love going to movies and just be chilled out and relaxed places. I'm not married for the time being but i am in a commitment in the name of God i hope that one day we will get married.

I would like to end with my most sincerly appreciation, first and foremost i would like to thank God Almighty for giving and Blessing me a beautiful talent cause apart from acting being my Job, it also happen to be something i love doing and when i am at it i do it with passion. I would also like to thank my whole family but special appreciation goes to the most beautiful woman in the whole world that happened to be my mother (I Love you Mom) would also like to thank Game 1st Quality Tanzania Limited and again special thank to my brother, my executive Producer and my Advicer Mr. Mtitu G. Game and His Wife. I Would like to thank all the Artist, Producers and Directors i have worked with. Also my special Thanks to my sister Sharifa Kalala in USA and Sanura Hussein in Denmark. Most Importantly, i would lastly like to thank all my fans from different part of the world, thank you all very much for supporting me, I LOVE YOU all and God bless you.

Wadau mwaweza kumtembelea msanii wetu Kanumba tovutini kwake kupitia http://www.kanumba.com




14/07/2009

Slaa naye aendeleza Libeneke

Dk. Willibroad Slaa

MBUNGE wa Karatu, Dk Willibrod Slaa (Chadema), ambaye ni maarufu kwa kuanika uovu, jana aliulipua mradi mkubwa wa kusambaza maji kwa wananchi wanaoishi kwenye miji ya Shinyanga na Kahama uliogharimu takriban Sh252 bilioni za walipakodi, akidai kuwa una harufu ya ufisadi.

Dk Slaa alitoa kauli hiyo jana akiwa mchangiaji wa tatu katika hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2009/10.

Alidai kigogo mmoja wa Mamlaka ya Maji safi na Majitaka wa Shinyanga kuwa alifanya ufisadi mkubwa, akishinikiza wenzake wakubali kupitisha fedha ambazo haziko katika utaratibu mzuri huku akionekana kuwekewa ulinzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Dk Slaa alisema katika mradi, ambao unatoka ndani ya mradi mkubwa wa Ziwa Victoria, ameingia mdudu anayeonekana wazi, lakini wahusika hawaonyeshi kasi katika namna ya kumshughulikia.

“Ni lazima iundwe Takukuru nyingine kwa ajili ya kuichunguza Takukuru iliyopo hivi sasa, kwani inaonekana kuwa imeshindwa kabisa kutekeleza majukumu yake na inaingilia kazi ambazo zinaonekana wazi kuwa ni sehemu ya rushwa,” alisema.

Aliitaka serikali iunde taasisi nyingine ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa ajili ya kuichunguza Takukuru iliyoko hivi sasa.

Alisema sababu za kutaka kuundwa kwa taasisi hiyo mpya ni kutokana na kile alichokieleza kuwa, Takukuru imeshindwa kabisa kutekeleza majukumu yake.

Akiongea kwa hisia kali, siku moja baada ya Spika Samuel Sitta kuruhusu watu kuonyesha hisia zao, mbunge huyo ambaye ni katibu mkuu wa Chadema, alizungumza huku akionyesha baadhi ya vielelezo vyake.

Alisema: "Tarehe 13 Machi mwaka huu, kigogo huyo alikwenda katika Hoteli ya Karena na kuongea na mkurugenzi wa Trans Ocean Supply Ltd na kukubaliana mambo ambayo ni wazi yanaonyesha kuwa kuna mianya ya kifisadi.

“Kama haitoshi siku iliyofuata alikwenda tena mkurugenzi huyo na kumchukua mgeni wake bila ya kujua walikuwa wanazungumza kitu gani, lakini kwa kutumia gari la serikali aina ya (Toyota)Prado namba STJ 6463 alimbeba na kumpeleka kwenye Uwanja wa Ndege wa Shinyanga.”

Dk Slaa alifafanua kuwa siku chache baada ya kuondoka kwa mkurugenzi wa Trans Ocean Supply Ltd, Gulam aliwaita wenzake na kuwaeleza kuwa alikuwa na maagizo kutoka kwa wakubwa ili aweze kununua vifaa vya kufunga mitambo ya maji katika miji ya Shinyanga na Kahama.

Kwa mujibu wa Dk Slaa, mkurugenzi huyo alikataliwa na mkurugenzi wa fedha wa Shinyanga kwamba asingeweza kutoa fedha zozote kwa ajili ya manunuzi ambayo yalikuwa nje ya utaratibu, lakini alilazimishwa na kutishwa ili akubali kuidhinisha kiasi cha Sh 2.1 bilioni ambazo tayari zilikuwa zikidaiwa.

Mbunge huyo alifafanua zaidi kuwa, baadhi ya viongozi waliendelea kumtishia mkurugenzi wa fedha na hata kiasi cha kumwandikia barua ya kumsimamisha kazi huku Takukuru ikiingilia kati kwa kuwasaidia baadhi ya watu ili wambane mkurugenzi huyo wa fedha ambaye aliendelea kuweka msimamo na kugoma.

Aliongeza kuwa, mkurugenzi wa maji aliamua kutembeza karatasi kwa ajili ya kuwasainisha wajumbe wa bodi kwenye nyumba zao ili waidhinishe fedha hizo bila ya kufuata maoni ya mkurugenzi wa fedha.

Alisema wakati huo tayari mita 4,000 za maji zilishafika katika eneo hilo bila ya kujua tenda hiyo ilikuwa imepitishwa na nani na kwa muda gani.

Maelezo ya Dk Slaa yalisema kuwa, kutokana na msimamo wa mkurugenzi huyo, alipelekewa fedha katika bahasha na alipokana, aliitiwa watu wa Takukuru ambao walimchunguza na bila kupata kitu chochote, lakini waliendelea kumfuatilia bila ya kujua sababu zipi ziliwafanya wamfuatilie.

Pamoja na kuihusisha Takukuru katika masuala ya rushwa, Dk Slaa aliijia juu Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambayo alisema imeonyesha udhaifu katika mradi huo baada ya kutumia fedha nyingi huku ikitambua kuwa bado kuna matatizo makubwa katika eneo hilo.

Alisema kuwa, taasisi hiyo haikutenda haki katika jambo hili kutokana na kuhusika moja kwa moja katika masuala mazima ya kushughulikia jambo hilo kwa kuwa iliwaacha wahusika kamili na kumfuata mtu mwingine tena kwa vitisho.

Alisema tayari ameshamfikishia Waziri wa Maji na Umwagiliaji taarifa zote na orodha ndefu ya majina ili aweze kushughulikia, vinginevyo hakuna haki inayotendeka kwa watumishi wenye misimamo ya kweli ndani ya wizara hiyo.

Kwa upande wa Maji, Dk Slaa aliibebesha lawama kwa kusema ilitumia kiasi cha Sh 700 milioni katika mradi huo huku itambua kuwa kuna tatizo kubwa katika mgogoro wa uendeshaji shughuli zake na kwamba, fedha hizo hazikutumika ipasavyo.

Dk Slaa alisema Sh700 milioni zingeweza kutosha kugharamia mradi mzima wa kusambaza maji katika miji ya Shinyanga na Kahama na kwamba kuidhinisha Sh2 bilioni ni sehemu ya ufisadi mkubwa usio na huruma kwa wananchi wa Tanzania.

Katika hotuba ya makadirio ya matumizi, wizara hiyo iliomba Bunge lipitishe jumla ya Sh 264,933,617,000 ili ziweze kutumiwa katika miradi mbalimbali.

Chanzo cha habari hii; http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=13275

Mwanasosholojia anakupa heko Dk Slaa, endeleza libeneke mpaka kieleweke!

12/07/2009

Kwa nini Wabunge Wasifuate Mfano wa Mama Killango?

Mbunge wa Same Mashariki, Mama Anne Killango Malecela

Nimevutiwa sana na ujasiri ambao mbunge wa Same Mashariki, Mama Anne Killango Malecela anazidi kuuonesha. Nimefurahishwa na kitendo chake cha kuamua kumwaga mlolongo wa tuhuma za ufisadi kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii na kueleza kusudio lake la kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka kuundwa kwa kamati teule kuchunguza wizi wa nyara za serikali.

Mbunge huyo anataka tume hiyo ichunguze jinsi watendaji wa wizara hiyo walivyoshiriki kwenye usafirishaji wa makontena mawili yaliyosheheni nyara za serikali kwenda nchini Vietnam. Killango alitoa kusudio hilo bungeni wiki iliyopita akipinga bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyosomwa jana na Waziri Shamsha Mwangunga.

Akiwa mchangiaji wa kwanza wa hotuba ya bajeti ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo, Killango alisema wizi wa nyara unafanyika nchini kama vile hakuna ulinzi.

"Tanzania hatukustahili kuwa maskini kwa rasilimali hizi. Sielewi wizara imeshindwa nini kudhibiti wizi mkubwa kiasi hicho," alisema Kilango baada ya kuelezea wizi wa makontena mawili ya pembe za ndovu yaliyokamatwa wiki iliyopita nchini Vietnam.

"Mheshimiwa Spika naomba nizungumze kuhusu jambo ambalo kwa kweli limenisikitisha sana ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii; wizi wa nyara; wizi wa pembe za ndovu. Wizi huu Mheshimiwa Spika, unafanyika kama vile nchi yetu hakuna ulinzi," alisema Kilango.

"Nimefanya utafiti nina faili zima; Mheshimiwa Spika nilikwenda kufanya utafiti, baada ya kusoma kwenye magazeti kuhusu makontena mawili yaliyokamatwa Vietnam, nikaona nisiishie hapo niende ndani mpaka nipate faili zima.

"Nasikitika sana. Nilikwenda kuhoji; nikaelezwa; nikapewa na faili; nikasoma kontena zile mbili zilipitia bandari yetu kama kawaida."

Aliongeza kwamba katika hati za kusafirishia makontena hayo kinachoonekana kusafirishwa ni plastiki chakavu zinazopelekwa kubadilishwa na kutengenezwa bidhaa nyingine wakati ukweli halisi makontena hayo yalibeba pembe za ndovu.

Akizungumza kwa umakini mkubwa na kujiamini, Kilango alisema: "Mheshimiwa Spika naomba kwa kutumia kanuni ya 117 ya Bunge, kifungu cha 10(b), Mheshimiwa Spika niombe ruhusa kwako nitoe kusudio langu la kuleta hoja binafsi. Napendekeza kuomba tuunde kamati teule ya kulichunguza hili. Mheshimiwa Spika nielekeze taratibu zote nilete mapendekezo yangu iundwe kamati kwa jambo hili leo hii."

Alisema iwapo jambo hilo litaachwa bila hatua hiyo, mianya ya ufisadi katika Wizara ya Maliasili na Utalii aliyodai kuwa ni mikubwa, haitazibwa na kwamba huwezi kuvumilia kuona nchi ikiibiwa wakati serikali ipo imara.

"Lakini Mheshimiwa Spika nashindwa kuelewa hii Wizara ya Maliasili na Utalii imeshindwa vipi 'kuprotect' mali za Watanzania. Hili jambo ni kweli, tunaomba tuelezwe yamekwenda kwendaje kule. Hatuwezi kukubali nchi kuendeshwa hivi, hapana. Mheshimiwa Spika hapana; naomba nikuambie ukweli hili jambo ni zito. "

Alisema analo jina la mtu aliyetumiwa makontena hayo, lakini si kazi yake kuyataja na kwamba serikali ndiyo itatoa majibu ya kashfa hiyo.

"Mheshimiwa Spika, kama kuna ufisadi unaoua nchi yetu ni huu. Kwa kweli Mheshimiwa Spika ningepata dakika tano ningelia kwanza ndipo niendelee kusema. Kama kuna vitu vinavyomaliza nchi yetu ni hivi. Kontena mbili zimejaa nyara, pembe za ndovu.

"Vietnam wanatupigia simu; custom Vietnam ndio wanatupigia simu; wanapigia mamlaka zetu kwamba jamani huku kuna kontena zenu. Mheshimiwa Spika, sizungumzi kama chekechea, nimefanya research (utafiti) nina faili zima.

"... kwamba sasa watu wachache ambao ni wezi wanaamua kuharibu jina la serikali ya Chama Cha Mapinduzi, hatutaki.

"Mimi ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini watendaji wa aina hii hatutaki waharibu jina la chama chetu, hatuwataki."

Kilango alikuwa akizungumzia mzigo wa pembe za ndovu zenye thamani ya takriban Sh15 bilioni zilizokamatwa na maofisa forodha wa Bandari ya Hai Phong ya Vietnam Ijumaa iliyopita. Mzigo huo uliokuwa na pea zinazokadiriwa kufikia 200 za ndovu, uliondoka Bandari ya Dar es Salaam mwezi Januari.

Habari zinadai kuwa mzigo huo ulikuwa ukisubiriwa na mmiliki wake, ambaye alisemekana kutimka baada ya kupata habari kuwa polisi walikuwa wakimsaka. Akitoa maelezo kuhusu hoja hiyo, Spika Samuel Sitta alisema, kanuni ya Bunge inayoweza kutumika kuunda kamati teule ni ya 117 na kuwa kinachosubiriwa ni majibu ya serikali leo kabla ya kujua nini cha kufanya.

Ujasiri wa Mbunge Killango, ni wa kipekee hususani miongoni mwa wabunge wenzake wa CCM. Ninavyoamini mimi, kuna maovu mengi na uzembe unaosababishwa na kutowajibika ipasavyo, vitu ambavyo kwa pamoja vinajulikana na wabunge, lakini wamekuwa wakiendelea kukaa kimya na kutafuna posho kwa kuhofia "kufulia" pindi watakapoyatamka mabaya ya watendaji wa serikali. Hii ni nidhamu ya uoga lakini kikubwa, naichukulia kama "ufisadi ndani ya ufisadi". Kwa nini nasema hivi? Nasema hivi kwa sababu kubwa moja; Bunge ni chombo cha kutunga sheria sambamba na kuyaeleza na matatizo ya wananchi kupitia wawakilishi wao ili yaweze kufanyiwa kazi. Mbunge yeyote awe wa CCM au wa upinzani, kama hatekelezi hayo anashabihiana na fisadi.

Kila mtu anapenda maendeleo. Tanzania tunahitaji maendeleo ili utu wa mwananchi maskini uthaminike. Wabung e kama wawakilishi wa wananchi (tena ambao wamewafuata wananchi wenyewe na kuomba kura zao), wanapaswa kuwajibika. Kuwajibika si kuhudhuria vikao vya bunge kila inapobidi pekee, ni pamoja na kufanya utafiti na kuyafichua maovu yanayoangamiza nchi yetu, bila kujali itikadi za chama kama ambavyo Mbunge Killango anafanya. Hongera mbunge Killango, tumefurahi kusikia ulichotamka, Waziri wa Maliasili na Utalii pia amekiri "kisiasa". Kwa nini Wabunge wengine msifuate mfano wa Mama Killango?

Sehemu ya habari hii ni kupitia http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=13180

04/07/2009

Bado Twamlilia Profesa Haroub Othman

Profesa Haroub Othman

Pamoja na kwamba mwanazuoni maarufu nchini Tanzania, Profesa Haroub Othman, amezikwa Jumatatu nyumbani kwao kisiwani Zanzibar baada ya kuaga dunia siku ya Jumapili akiwa na umri wa miaka 66, bado Jumuiya ya Wanazuoni ya Chuo Kikuu Dar es Salaam (CKD) tunamlilia, na pengine kuendelea kujiuliza kwa nini lakini umauti umemchukua mpendwa wetu wakati bado tunamuhitaji.

Binafsi nilimuona Profesa Haroub kama mwanazuoni mwenye uwezo usiomithilika, pamoja na kwamba tunaelezwa alisomea sheria ingawa alifanya kazi katika taasisi ya masomo ya maendeleo (Institute of Development Studies) ya CKD, mimi naona pia alikuwa Mwanasosholojia kufuatia uwezo wake wa kuchambua mambo yanayoizunguka jamii kwa kina. Kila nilipokuwa namsikiliza Profesa Haroub nilikuwa napata taswira ya nguli Profesa Chachage ambaye naye alitutoka miaka kadhaa iliyopita. Hakuwa mwoga kuelezea kile alichokiamini, tabia ambayo hata Profesa Chachage alikuwa nayo!

Tunazidi kupoteza wanazuoni mahiri, narudi kukisaili kifo, kwa nini lakini kifo? Nilipopata taarifa za kifo chake, niliamua kuandika kwa haraka tenzi zifuatazo;

Kweli kifo ni fumbo
Chaweza kukupiga kikumbo
Bora kingekuwa wimbo
Kuuimba au kuuacha!

Kifo kweli msamiati
Hakiji kwa wakati
Hata upange mkakati
Chaweza tokeza kati!

Profesa Haroub wa Othumani
Ni kweli wafukiwa mchangani?
Ni kweli umefichwa mautini?
Jamani wewe kifo kwa nini?

Kwa nini kifo lakini?
Hukumwacha yeye duniani?
Tutafanya nini jamani?
Hatunaye mwanazuoni!

Mikono yanitetema
Kwa taabu ninahema
Nikikumbuka yako mema
Ewe Profesa wetu mwema!

Changamoto umetuachia
Kizazi kilichobakia
Kabla mauti kuwadia
Tuyafanye uloazimia

Nashindwa kuendelea
Uchungu wanilemea
Pole nawatolea
Familia na ndugu pia!

Masaa machache baadaye, nilikutana na tungo nyingine iliyoandikwa na rafiki yangu mwanazuoni Stephen L Kirama kutoka Idara ya Uchumi ya CKD. Niliifurahia na inakwenda namna hii;

Tulisikia kwa dhati, Redioni Ukichati,
Wakikuweka mtu kati, ukawajibu kwa dhati.
Hukukiboronga kiti, Hoja ulizidhibiti,
Profesa Haroub Kwaheri, Mola akupe akhera.

Wahadhiri tunokua, kwako tulijifunzia,
Hoja kuzipangilia, bila hadhira kuboa.
Hoja zako ukitoa, hadhira ilitulia,
Profesa Haroub Kwaheri, Ukajaliwe akhera.

Uwezo wa kusikiza, wengi ulituvutia,
Hukujiweka wa kwanza, isipositahilia.
Hukupenda kujikweza, hata lipostahilia
Profesa Haroub Kwaheri, Mbingu saba uzifike.

Familia lobakia, Pole zetu twazitoa,
Mola nguvu kuwatia, hiyo sala twatolea.
Mkabaki mkijua, mwili umetangulia
Jina lake linaishi, na Daima litadumu.

Ugumu tunaujua, machungu pia kadhia,
mhimili kupotea, mtu ulomzoea.
Mama nawe tunalia, Pole zetu tunatoa
Profesa Saida Pole, Mola kampenda zaidi.


22/06/2009

Pigo la Mwaka: Mama Yangu Ameaga Dunia

Jeneza lililohifadhi mwili wa mama

Familia ikiomboleza, mjukuu wa marehemu mama, binti yangu Magreth akiwa amefumbata mikono katika lindi la mawazo

Nilishindwa kujizuia kutoa machozi kwa uchungu baada ya kuiona sura ya mama kwa mara ya mwisho

Baba yangu akiaga mwili wa mkewe

Jeneza lililobeba mwili wa marehemu mama likishushwa kaburini

Niliweka shada la maua katika kaburi la mama

Kimya hiki kingine kimesababishwa na msiba mkubwa niliopata. Tarehe 16 mwezi huu, siku ya Jumanne, mama yangu mzazi aliaga dunia katika hospitali ya Mission Mikocheni, Dar es Salaam. Pamoja na jitihada zote za kuokoa maisha yake, mama alifariki saa mbili asubuhi.

Tulimzika mpendwa wetu tarehe 18, katika makaburi ya City, Yombo Dovya na kuendelea na kipindi cha maombolezo. Lazima niwe mkweli, nimempoteza mtu muhimu sana maishani mwangu, nafahamu fika kuwa ni lazima sote twende mbele ya haki, kwa vipindi na nyakati tofauti, lakini sikutegemea kama hili lingetokea kwa sasa. Faraja pekee niliyonayo baada ya msiba huu ni kwamba, nimeweza kuonana na mama baada ya kurudi toka Dublin (wengine wanasema ni kama alikuwa ananisubiri!).

Nitajitahidi kuyaenzi mazuri aliyoniachia na kunifanyia mama, kama ishara ya kuthamini mchango wake kwangu. Mama alipenda sana nipate elimu, na alinisaidia kivitendo. Naliona jukumu kubwa mbele yangu la kuwasaidia wengine kama ambavyo mama alifanya kwangu.

15/06/2009

Wadau Mwanasosholojia Yupo Yupo!

Jamani wadau Mwanasosholojia yupo yupo! Hapa ninamaanisha kuwa msione kimya mkadhani Mwanasosholojia hayupo, nipo wadau wangu nimebanwa tu na majukumu ya kuuguza, mama yangu mzazi na mtoto wetu aliyezaliwa tarehe 9 mwezi huu Dominic a.k.a Mwanashosholojia Jr.

Mama amehamishiwa Mission Mikocheni Hospital kutoka Kituo cha Afya cha Chuo Kikuu Mlimani, hali yake bado si nzuri. Tuna matumaini makubwa kuwa hali yake itakuwa nzuri tu na atapona. Mwanasosholojia mtoto naye alizaliwa na flu kali kiasi cha kushindwa kunyonya. Pia alizaliwa akiwa na matatizo kidogo katika mfumo wa upumuaji, kiasi cha kuwekewa vifaa vya kumsaidia kupumua na kupewa dawa katika chumba maalumu (incubator). Mpaka leo asubuhi ana mabadiliko makubwa na ameanza kunyonya maziwa ya mama yake. Huenda naye pia akaruhusiwa kutoka hospitali na mama yake muda si mrefu.

Pamoja na misukosuko hii na mahangaiko yote haya, leo nimejisikia hamu ya kutunga kidogo, naomba wadau wangu niwarushie tungo hizi chache za kujifariji katika kipindi hiki kigumu;

Ewe mama yangu mpendwa
Tambua kwamba unapendwa
Wala katu hujatendwa
Wewe sio wa kutendwa!

Jipe moyo mama yangu
Mfariji wa moyo wangu
Unayejua kuzaliwa kwangu
Uliyenizaa kwa uchungu!

Nipo karibu nawe mama
Nafurahi kuwa unahema
Ingawa huwezi kusema
Wala huwezi kusimama!

Jipe moyo utapona
Mungu anakupenda mbona
Wanakuhitaji wote wana
Tunapenda kukuona!

Wajukuu zako mama
Kuanzia walosimama
Hata wanaolalama
Wanakupenda sana mama!

Pona sasa mama yangu
Uje nyumbani kwangu
Uwaone na wanangu
Pinu,Mage na Domi wangu!




10/06/2009

Mwanasosholojia Jr Azaliwa!

Jamani wadau wangu, sina budi kushea nanyi furaha niliyo nayo leo! Mimi na mama Mwanasosholojia tumepata mtoto wa kiume usiku wa kuamkia leo. Kwa muda tunamwita Mwanasosholojia Jr. wakati tunafikiria jina la kumpatia. Natamani mtoto huyu aje kuwa Mwanasosholojia! Huenda akaja kuwa Mwanasosholojia. Ni mtoto wetu wa tatu baada ya Agripinus mwenye umri wa miaka minane (alizaliwa tarehe ya leo, 10/06), anasoma darasa la pili na binti yetu Magreth ambaye kwa sasa ana umri wa miaka mitano, na anasoma darasa la kwanza hapa Dar es Salaam. Tunawashukuru wapendwa ndugu, rafiki na jamaa zetu ambao wamekuwa nasi bega kwa bega katika kipindi chote tulichopitia.

Nachukua nafasi hii pia kuwajulisha wadau kuwa, pamoja na kuongeza memba katika familia yangu, jana mama yangu alilazwa hospitalini baada ya hali yake kubadilika ghafla na kupata kitu kama dege dege. Tulimuwahisha kituo cha afya cha Chuo Kikuu Kampasi ya Mlimani, ambapo anaendelea kupata matibabu. Mpaka asubuhi hii hali yake ilikuwa inaendelea vizuri, pamoja na dawa nafikiri pia hasa baada ya kupewa taarifa za ujio wa Mwanasosholojia Jr. (mumewe!!!)