07/02/2010

Nembo ya Taifa na Hofu ya Kughushiwa

Imezuka hofu na utata wa masuala ya kughushi kwenye nembo ya Taifa ambapo uchunguzi wa vyombo vya habari umebaini kuwa sasa zipo aina mbili za nembo ya Taifa zinazotumika kwenye nyaraka mbalimbali za serikali.

Nembo ya Taifa ni mamlaka na kielelezo na ushahidi halali wa serikali ya Jamhuri ya Tanzania na kwamba kuitumia isivyo ni kosa la jinai.

Kwa mujibu wa tamko la namba 488 la mwaka 1996 ni marufuku kwa taasisi au kampuni na hata idara za serikali kuwa na mhuri wenye nembo ya serikali na kwamba wenye nembo isiyo halali walitakiwa kuziwasilisha ofisi ya Waziri Mkuu mara moja.

Uchunguzi umegundua kuwepo kwa nembo tofauti katika nyaraka zikiwemo kalenda za taasisi za serikali au hata wizara kadhaa kutokana na kutofautiana kwa mambo muhimu ambayo kimsingi hayatakiwi kutofuatiana.

Moja ya nyaraka zenye nembo inayotofautiana ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2005 na nembo iliyopo kwenye baadhi ya nyaraka za Tume ya uchaguzi.

Baadhi ya nyaraka za Tume ya Uchaguzi zina nembo yenye maneno ya UHURU NA UMOJA yaliyoandikwa kwa wino mweusi wakati ya maneno yaliyoko kwenye katiba yana rangi nyekundu, lakini pia baadhi ya nyaraka za Tume zimeandika neno 'na' kwa herufi ndogo kama 'UHURU na UMOJA'.

Hali kadhalika wakati nembo iliyoko kwenye katiba ikiwa na alama za njano katikati ukiwemo mwenge, nembo ya kwenye nyaraka za tume ina alama nyeupe na mwenge ni mwekundu wakati pia nembo hiyo inaonesha miguu yote ya picha ya mtu wa kulia ambaye ni hawa wakati nembo ya kwenye katiba haioneshi miguu yote.

Nembo ya kwenye katiba pia inaonesha maandishi ya UHURU NA UMOJA yakiwa yameandikwa kwenye karatasi maalumu ambalo mwisho wake limepambwa na mimea yenye matunda, lakini nembo ya nyaraka za Tume yameandikwa kwenye karatasi lililoishia kwenye majani yaliyolala.

Uchunguzi katika nembo hizo pia uligundua kwamba mawimbi yaliyopo katikati chini ya nembo yanatofautiana kutokana na ukweli kwamba mawimbi katika nembo ya katiba ni ya rangi ya bluu, wakati yaliyopo kwenye nembo ya tume ni ya rangi ya kijani.

Unaweza kuangalia baadhi ya tofauti hizo hapo chini, na kuipata habari hii kwa upana zaidi, bofya hapa

No comments:

Post a Comment