15/07/2009

Slaa naye aendeleza Libeneke

Dk. Willibroad Slaa

MBUNGE wa Karatu, Dk Willibrod Slaa (Chadema), ambaye ni maarufu kwa kuanika uovu, jana aliulipua mradi mkubwa wa kusambaza maji kwa wananchi wanaoishi kwenye miji ya Shinyanga na Kahama uliogharimu takriban Sh252 bilioni za walipakodi, akidai kuwa una harufu ya ufisadi.

Dk Slaa alitoa kauli hiyo jana akiwa mchangiaji wa tatu katika hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2009/10.

Alidai kigogo mmoja wa Mamlaka ya Maji safi na Majitaka wa Shinyanga kuwa alifanya ufisadi mkubwa, akishinikiza wenzake wakubali kupitisha fedha ambazo haziko katika utaratibu mzuri huku akionekana kuwekewa ulinzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Dk Slaa alisema katika mradi, ambao unatoka ndani ya mradi mkubwa wa Ziwa Victoria, ameingia mdudu anayeonekana wazi, lakini wahusika hawaonyeshi kasi katika namna ya kumshughulikia.

“Ni lazima iundwe Takukuru nyingine kwa ajili ya kuichunguza Takukuru iliyopo hivi sasa, kwani inaonekana kuwa imeshindwa kabisa kutekeleza majukumu yake na inaingilia kazi ambazo zinaonekana wazi kuwa ni sehemu ya rushwa,” alisema.

Aliitaka serikali iunde taasisi nyingine ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa ajili ya kuichunguza Takukuru iliyoko hivi sasa.

Alisema sababu za kutaka kuundwa kwa taasisi hiyo mpya ni kutokana na kile alichokieleza kuwa, Takukuru imeshindwa kabisa kutekeleza majukumu yake.

Akiongea kwa hisia kali, siku moja baada ya Spika Samuel Sitta kuruhusu watu kuonyesha hisia zao, mbunge huyo ambaye ni katibu mkuu wa Chadema, alizungumza huku akionyesha baadhi ya vielelezo vyake.

Alisema: "Tarehe 13 Machi mwaka huu, kigogo huyo alikwenda katika Hoteli ya Karena na kuongea na mkurugenzi wa Trans Ocean Supply Ltd na kukubaliana mambo ambayo ni wazi yanaonyesha kuwa kuna mianya ya kifisadi.

“Kama haitoshi siku iliyofuata alikwenda tena mkurugenzi huyo na kumchukua mgeni wake bila ya kujua walikuwa wanazungumza kitu gani, lakini kwa kutumia gari la serikali aina ya (Toyota)Prado namba STJ 6463 alimbeba na kumpeleka kwenye Uwanja wa Ndege wa Shinyanga.”

Dk Slaa alifafanua kuwa siku chache baada ya kuondoka kwa mkurugenzi wa Trans Ocean Supply Ltd, Gulam aliwaita wenzake na kuwaeleza kuwa alikuwa na maagizo kutoka kwa wakubwa ili aweze kununua vifaa vya kufunga mitambo ya maji katika miji ya Shinyanga na Kahama.

Kwa mujibu wa Dk Slaa, mkurugenzi huyo alikataliwa na mkurugenzi wa fedha wa Shinyanga kwamba asingeweza kutoa fedha zozote kwa ajili ya manunuzi ambayo yalikuwa nje ya utaratibu, lakini alilazimishwa na kutishwa ili akubali kuidhinisha kiasi cha Sh 2.1 bilioni ambazo tayari zilikuwa zikidaiwa.

Mbunge huyo alifafanua zaidi kuwa, baadhi ya viongozi waliendelea kumtishia mkurugenzi wa fedha na hata kiasi cha kumwandikia barua ya kumsimamisha kazi huku Takukuru ikiingilia kati kwa kuwasaidia baadhi ya watu ili wambane mkurugenzi huyo wa fedha ambaye aliendelea kuweka msimamo na kugoma.

Aliongeza kuwa, mkurugenzi wa maji aliamua kutembeza karatasi kwa ajili ya kuwasainisha wajumbe wa bodi kwenye nyumba zao ili waidhinishe fedha hizo bila ya kufuata maoni ya mkurugenzi wa fedha.

Alisema wakati huo tayari mita 4,000 za maji zilishafika katika eneo hilo bila ya kujua tenda hiyo ilikuwa imepitishwa na nani na kwa muda gani.

Maelezo ya Dk Slaa yalisema kuwa, kutokana na msimamo wa mkurugenzi huyo, alipelekewa fedha katika bahasha na alipokana, aliitiwa watu wa Takukuru ambao walimchunguza na bila kupata kitu chochote, lakini waliendelea kumfuatilia bila ya kujua sababu zipi ziliwafanya wamfuatilie.

Pamoja na kuihusisha Takukuru katika masuala ya rushwa, Dk Slaa aliijia juu Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambayo alisema imeonyesha udhaifu katika mradi huo baada ya kutumia fedha nyingi huku ikitambua kuwa bado kuna matatizo makubwa katika eneo hilo.

Alisema kuwa, taasisi hiyo haikutenda haki katika jambo hili kutokana na kuhusika moja kwa moja katika masuala mazima ya kushughulikia jambo hilo kwa kuwa iliwaacha wahusika kamili na kumfuata mtu mwingine tena kwa vitisho.

Alisema tayari ameshamfikishia Waziri wa Maji na Umwagiliaji taarifa zote na orodha ndefu ya majina ili aweze kushughulikia, vinginevyo hakuna haki inayotendeka kwa watumishi wenye misimamo ya kweli ndani ya wizara hiyo.

Kwa upande wa Maji, Dk Slaa aliibebesha lawama kwa kusema ilitumia kiasi cha Sh 700 milioni katika mradi huo huku itambua kuwa kuna tatizo kubwa katika mgogoro wa uendeshaji shughuli zake na kwamba, fedha hizo hazikutumika ipasavyo.

Dk Slaa alisema Sh700 milioni zingeweza kutosha kugharamia mradi mzima wa kusambaza maji katika miji ya Shinyanga na Kahama na kwamba kuidhinisha Sh2 bilioni ni sehemu ya ufisadi mkubwa usio na huruma kwa wananchi wa Tanzania.

Katika hotuba ya makadirio ya matumizi, wizara hiyo iliomba Bunge lipitishe jumla ya Sh 264,933,617,000 ili ziweze kutumiwa katika miradi mbalimbali.

Chanzo cha habari hii; http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=13275

Mwanasosholojia anakupa heko Dk Slaa, endeleza libeneke mpaka kieleweke!

2 comments:

  1. Kaka upo wapi tunakumiss maana umepotea kweli.

    ReplyDelete
  2. Ni kweli dadangu, baada ya mkasa ulonikumba, nikabanwa kweli. Kupost vitu imekuwa issue, ila ntarudi kuendeleza libeneke soon! Nawapenda na kuwamiss jamani!

    ReplyDelete