Mroki malenga wetu, salamuzo nimepata
Nakujibu mwanakwetu, nipo safi pasi tata
Ulichokiuliza kwetu, jibu lake utalipata
Mwenye mamlaka dereva, kondakta ni msaidizi
Kondakta ni msaidizi, mwenyewe umeonesha
Wala hafanyi ajizi, vituoni kutushusha
Hata kupiga uluzi, dereva kumgutusha
Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi
Dereva ndiye mwamuzi, gari kulisimamisha
Anaviruka vihunzi, abiria kuwafikisha
Kumsikiliza msaidizi, ukweli si kubadilisha
Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi
Anashika usukani, gari kuliongoza
Anapokuwa barabarani, kulipoza na kukoleza
Breki zi miguuni, aweza kuzichokoza
Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi
Hakuna ubishi malenga, anayo mamlaka
Anaweza kukutenga, asisimame Malampaka
Matusi ukimlenga, atakuvukisha mpaka
Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi
Nilipata walau dakika, Kamarade nimjibu
Naweza tena andika, kwa sababu ni wajibu
Ila ninayo hakika, ataridhishwa na jibu
Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi
Safi sana kaka,sikujua wewe ni mwandishi wa tungo.Kweli kabisa mwenye mamlaka dereva,kondakta msaidizi.
ReplyDeleteKuna wakati sina uhakika Dereva aendeshaye nchi-Tanzania ni nani hasa!
ReplyDeleteHivi kuna uwezekano watu kutostukia kuwa kumbe dereva ni kondakta ?
Kaka Kitururu, yawezekana kabisa, labda abiria tunaendeshwa na dereva "asiye dereva"
ReplyDelete