12/10/2007

Profesa Chachage: Kumbukumbu inayonikumbusha Mwalimu Nyerere


Hapana shaka hata kidogo kuwa kuna mambo mengi ambayo aliyekuwa mkuu wa idara ya Sosiolojia na Anthroplojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hayati Profesa Chachage Seithy Loth Chachage alishabihiana sana na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ninazo sababu lukuki za kusema hivyo, lakini kubwa ni kwamba, ninapokumbuka uwezo mkubwa aliokuwa nao Mwl. Nyerere najikuta nikikumbuka pia umahiri aliokuwa nao Profesa Chachage, si tu katika kuchanganua mambo kwa kina, bali katika kuonesha uzalendo kwa nchi yetu ya Tanzania.

Kwa kuanzia, sote tunafahamu kuwa Mwl. Nyerere alikuwa na sifa nyingi. Nia yangu si kurudia sifa za Mwl Nyerere, lakini najaribu kuonesha namna ambavyo uwezo wa Baba wa Taifa utabakia katika historia ya vizazi na vizazi hapa duniani. Kwanza kabisa Mwl. Nyerere alikuwa mwalimu hasa, mwalimu ambaye wanafunzi wake wanajisikia faraja kufundishwa naye. Mwalimu ambaye ni makini awapo ndani na nje ya darasa. Mwalimu ambaye yupo tayari kumsaidia mwanafunzi kuelewa kinachotakiwa, ili na yeye asaidie wanafunzi wenzake anapokosekana. Zaidi Mwl. Nyerere alikuwa mwalimu ambaye anaona uchungu pale anapogundua kuwa mwanafunzi wake mmoja au wawili watatu hawamwelewi kutokana na sababu mbalimbali zinazotokana na udhaifu wao. Tumesoma na kusikia habari nyingi za watu ambao walitokea kufundishwa na Mwl. Nyerere, wakielezea jinsi ambavyo alikuwa mwalimu makini na anayejituma katika kipindi chake cha utumishi wa serikali kama mwalimu.

Yeye binafsi alichukia tabia ya walimu kutokuwa makini. Mfano mzuri ni pale alipotoa hotuba katika Chuo cha Ualimu Morogoro, Agosti 27, 1966 ambapo alionesha kukerwa na walimu wasiokuwa makini. Mwalimu Nyerere alisema kuwa, inapotokea mwalimu anaingia darasani amechoka au mwenye kuonekana kuchoka, aliyevunjika moyo na asiye na hamu ya kazi na ambaye anahitaji kila kazi ifanywe na wanafunzi huku yeye akiangalia, au ambaye anawaona wanafunzi kama wanamchosha, inapotokea hivyo wanafunzi watajenga mawazo kuwa ualimu ni kazi ya kuikwepa na kwamba kusoma ni kama jambo ambalo mtu anapaswa kupitia tu na pia njia ya kutumia mamlaka ni kuwafanya watu wengine wakufanyie kazi. Hapa Mwalimu Nyerere alikuwa akionesha kuwa waalimu wana nguvu zaidi ya watu wengi wanavyoelewa, na kwamba wana ushawishi mkubwa katika jamii kama tokeo la ushawishi huo kwa wanafunzi wao.

Sifa hii ya Mwl. Nyerere ndiyo inayonifanya pia nijaribu kufananisha na ile aliyokuwa nayo Profesa Chachage, ya “ualimu makini”. Kama alivyokuwa Mwl. Nyerere, Profesa Chachage alikuwa Mwalimu makini, anayejituma, na mwenye uchungu na kazi yake. Bahati nzuri nilitokea kuwa mmoja wa wanafunzi wa Profesa Chachage kuanzia masomo yangu ya shahada ya kwanza na ile ya uzamili katika sosiolojia. Hapa ndipo nilipoweza kuona umakini wa Mwl. Nyerere kupitia yeye. Profesa alipenda kila mwanafunzi wake aelewe, na alipojua kuwa hujaelewa ni lazima utagundua ni jinsi gani alikuwa akijisikia uchungu, uchungu wa kuona kwa nini humwelewi. Tumeelezwa kuwa darasa la Mwl. Nyerere lilikuwa linawajibika kujiandaa kabla hajaingia ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo alikuwa akizitoa kwa wanafunzi wake. Hali hiyo ndiyo iliyokuwa ikitukuta sisi tuliokuwa wanafunzi wa Profesa Chachage. Ilikuwa ni vigumu kwa mwanafunzi kujisikia amani moyoni kama anajijua kuwa hajajiandaa. Ukiulizwa swali na Profesa ni lazima uhakikishe ya kuwa utakachojibu ni lazima umekisoma na hata kukifanyia utafiti wa kina. Ilikuwa si rahisi kumdanganya Profesa, kama ambavyo haikuwa rahisi kumdanganya Mwl. Nyerere. Hii inaonesha kuwa walimu hawa wawili walikuwa wanatumia muda wao si kwa ajili ya kufundisha tu, bali pia kuongeza ujuzi wa mambo mbalimbali yanayohusiana na kile wanachokifundisha. Nimewahi kudokezwa na Dakta Abu Kambhaga Mvungi, mkuu wa idara ya Sosiolojia na aliyekuwa swahiba mkubwa wa hayati Profesa Chachage kuwa, Profesa alikuwa na tabia ya kuingia vitabu “msalani” (chooni)!!

Hivi leo ni walimu wangapi ambao wana sifa kama hizo? Asilimia kubwa ya walimu waliopo sasa wanachojua kuwa ni jukumu lao ni kufundisha, tena kufundisha kwa mtindo wa kuwasomea wanafunzi notisi zilizoandaliwa miaka na miaka. Mwalimu kazi yake kubwa inakuwa ni kusubiri muda wa kipindi na kutafuta alichowafundisha wanafunzi wake wa mwaka uliopita, na kwenda kukitoa kama kilivyo darasani. Mwalimu haanzishi mada zinazochangamsha darasa kujadiliana masuala mbalimbali. Kibaya zaidi ni kwamba, anachelewa darasani kwa dakika kumi na anawahi kutoka dakika kumi na tano kabla muda wa kuhitimisha. Lakini ni mwalimu huyu huyu ambaye haishi kulalamika kuwa wanafunzi wa siku hizi ni wagumu kuelewa, wavivu na hawana tabia ya kujisomea na kuchunguza mambo kwa kina. Hali hii ni tofauti kabisa na ile aliyokuwa nayo Mwl. Nyerere na Mwl. Profesa Chachage. Nafikiri wakati umefika wa walimu kuiga mwenendo wa walimu hawa wawili mahiri ili kujenga kizazi bora cha watanzania makini, wenye tabia ya kujisomea na kutafiti mambo kwa kina na kisha kuyatolea ufafanuzi. Hii itasaidia pia kujenga uzalendo kwa nchi yetu katika zama hizi ambazo Mwl. Nyerere na Profesa waliziita kwa majina tofauti lakini yenye maana zinazofanana, ‘ukoloni mambo leo’ na ‘utandawizi’.

Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi thabiti. Sifa za uongozi za mwalimu ni vigumu kuzielezea kwa uhakika. Mwl. Nyerere alikuwa miongoni mwa viongozi wachache wa kutolewa mfano, si tu katika bara la Afrika bali duniani pote. Baba wa Taifa alikuwa na sifa zote za kiongozi thabiti, alikuwa kiongozi anayejituma na aliyejitoa kwa ajili ya nchi yake. Haya yanadhihirishwa na nyadhifa mbalimbali za uongozi ambazo hakuwahi kuziomba au kuzipigania. Mwalimu alikuwa kiongozi wa watu na wao ndiyo waliopenda siku zote awe kiongozi wao. Historia inatueleza kuwa Mwalimu alianza kuwa kiongozi tokea akiwa na umri mdogo katika shule na maeneo mbalimbali aliyopitia. Hii inaonesha kuwa kipaji cha uongozi cha Mwl. kilianza kuonekana mapema miongoni mwa watu aliokutana nao, na ndiyo maana hawakusita kumpendekeza au kumchagua kuwa kiongozi wao. Kuonesha kuwa alikuwa na uchungu na nchi yake, Mwl. alikubali hata kuacha kazi ya ualimu “wa darasani” ili ashiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa nchi yetu ya Tanzania. Mwl. alidhihirisha uthabiti hata alipokuwa Rais wa nchi hii. Tunaelezwa ya kuwa Mwl. alikuwa mwiba mkali kwa watendaji wazembe katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

Sifa za uongozi za Mwalimu Nyerere zilizidi kujidhihirisha hata kwa jirani zetu na nchi nyingine mbalimbali duniani pale ambapo alikubali kuwa kiongozi katika harakati za kupigania uhuru kwa nchi ambazo zilikuwa hazijapata uhuru, na hata kufikia kukaribisha harakati hizo kuanzia katika nchi yetu. Nchi yetu ilikaribisha vyama kama ANC na SWAPO kuifanya Tanzania kuwa makao yao katika kupanga mikakati ya kujikomboa katika makucha ya ukoloni. Hii ni sifa kubwa ambayo kiongozi mwenye kujua maana ya uhuru anapaswa kuwa nayo. Mwalimu aliona mbali, na kila mara alikuwa akiielezea dhana yake kuwa si kitu kwa Tanzania kuwa huru wakati nchi nyingine za kiafrika bado zinatawaliwa. Baba wa Taifa pia hakuyumbishwa na siasa wala vitisho vya nchi zinazojiita zilizoendelea. Alijali dhana ya utaifa na uzalendo katika maamuzi yeyote yaliyogusa maslahi ya wananchi. Ni viongozi wachache mno ambao wana upeo na mtazamo kama wa mwalimu. Tunayo shuhudia leo kwa viongozi wengi wa nchi za kiafrika na nyingine zinazoitwa zinazoendelea ni kuwakumbatia mabeberu wa dunia kwa kigezo cha kuogopa kunyimwa misaada. Sera za mataifa makubwa ndizo bado zinaendelea kupigiwa upatu huku hakuna juhudi zozote miongoni mwa nchi za ‘dunia ya tatu’ kuonesha msimamo katika maamuzi yanayojali maslahi ya mataifa hayo.

Hili linanifanya pia nimkumbuke Profesa Chachage, uthabiti katika uongozi. Katika kipindi nilichofanya kazi chini yake nikiwa Tutorial Assistant na yeye akiwa mkuu wa idara ya Sosholojia na Anthropologia niligundua mambo mengi kupitia Profesa Chachage. Kama inavyoelezwa na watu waliowahi kufanya kazi chini ya Mwalimu Nyerere, Profesa Chachage pia alikuwa kiongozi thabiti, asiyeyumbishwa na asiyetetea uzembe katika kazi. Pamoja na kuwa alikuwa na majukumu makubwa ya kiuelemishaji, lakini Profesa kama ilivyokwa kwa Mwalimu alijituma mno katika kazi, na haikuwa jambo la kushangaza sana kwetu tulipokuwa tukimuona akiondoka ofisini usiku kutokana na majukumu mbalimbali ya kikazi yaliyokuwa yakimkabili. Mbali na ukuu wa idara, Profesa alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) na siku zote alijali maslahi ya wafanyakazi wenzake, na si wafanyakazi tu bali hata ya wanafunzi pale ambapo palitokea mvutano kati yao na utawala au serikali. Hali hii ya uongozi makini ambayo alikuwa nayo Profesa Chachage inashabihiana kabisa na ile aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere. Wote alijitoa kwa ajili ya kupigania maslahi ya umma, bila ya kujali rangi, kabila wala dini.

Lakini leo hii tukiangalia, ni viongozi wangapi walio na mioyo kama hiyo? Ni viongozi wangapi ambao wapo tayari kubaki maofisini wakifanya kazi za ujenzi wa taifa mpaka usiku uliopitiliza? Tunachoshuhudia leo ni majibu kutoka kwa makatibu mahsusi wao kuwa hawapo katika ofisi zao, na unapochunguza kwa makini unagundua kuwa, kutokuwepo kwao ofisini hakusababishwi na kuwa na majukumu ya kikazi nje ya ofisi zao, bali kunatokana na kuwa na majukumu binafsi nje ya ofisi zao katika muda wa kazi. Wengi wamekuwa wakifanya ziara katika vivutio mbalimbali vya watalii, wakijaribu kuiga mfumo wa wenzetu wa mataifa ya magharibi ambao kwao sehemu za kuliwaza mawazo yao baada ya kazi ni katika mbuga zetu za wanyama, na sehemu za kuongeza ufahamu katika kile wanachoamini ‘kutokuendelea’ kwetu ni kuja kutembea na ‘kushangaa’ juu ya mfumo wetu wa maisha. Kiongozi ambaye tunategemea yupo ofisini kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali za wananchi, au ambaye tunategemea kuwa ndiye anayepaswa kutembelea wananchi kule waliko ili kutatua shida zao, ndiye huyo huyo kiongozi ambaye anaomba muda ukimbie haraka ifikie ule rasmi wa kumaliza shughuli za kiofisi ili aweze kukimbilia kupata ‘moja moto moja baridi’! Hapa sina maana ya kusema kuwa viongozi makini hawapaswi kujipumzisha na kuburudika, hata Profesa Chachage alikuwa akipata moja moto moja baribi pale Klabu ya UDASA, lakini ninachokiongelea ni ile hali ya kutumia muda ambao ulipaswa kuwa wa kuwatumikia wananchi kwa ajili ya manufaa binafsi. Kwangu hili nalifananisha na unyonyaji na udhalimu mkubwa, kwa kuwa kiongozi amewekwa na wananchi ili aweze kuwatumikia kikamilifu, kutofanya hivyo, si tu ni kuwadhulumu haki zao, bali ni kuwanyonya!

Mwalimu Nyerere alikuwa ni mpenda haki, usawa na amani. Mwalimu hakupenda dhuluma na siku zote alitetea usawa wa binadamu na kupigania amani. Hili tunaliona katika mambo mengi ambayo mwalimu aliyafanya, ikiwemo pia hotuba zake. Nyingi ya hotuba za Mwalimu zimejaa maudhui ya haki usawa na amani. Mwalimu alikuwa mkorofi kwa wale ambao kwa makusudi waliwanyima haki wenzao. Yeye alitaka kila mmoja aweze kupata haki katika nyanja mbalimbali kwani aliamini kuwa haki haikuwa suala la wachache kutokana na kwamba siku zote haki haiuzwi kama vile ambavyo bidhaa zinavyouzwa dukani. Aliamini ya kuwa umoja wa kitaifa unajengwa na misingi ya haki na endapo misingi hiyo itavunjwa au kupindishwa ndiyo mwanzo wa machafuko ambayo ni kikwazo cha maendeleo ya kweli. Mwalimu pia alipenda usawa bila kujali nafasi ya mtu katika jamii. Kwa Mwalimu kila mwananchi alikuwa sawa na mwenzake pasipo kujali cheo au dhamana, uwezo wala rangi yake. Katika makala yake iliyochapishwa katika gazeti la The Nationalist, Februari 14, 1967 iliyobebwa kichwa cha habari chenye tafsiri “Ujamaa si ubaguzi wa rangi”, Mwalimu alisema kuwa kama sehemu kubwa ya watu katika jamii fulani ni weusi basi watakaofaidika na ujamaa ni weusi, lakini hili haalina maana katika rangi yao, bali ni katika ‘utu’ wao. Lakini pia alisisitiza kuwa bila ya kukubalika kwa usawa wa binadamu hakutakuwa na ujamaa. Ingawa katika Tanzania kwa sasa hatuongelei juu ya ujamaa lakini tunapaswa kutambua ya kuwa usawa kwa wanadamu ni jambo la msingi. Na mara nyingi tunashindwa kutambua ya kuwa, watu wanazungumzia kukosekana kwa usawa na haki katika jamii yetu kwa kuwa tupo katika mfumo ambao suala la usawa halipo.

Hatuwezi kuwa na usawa katika mfumo ambao unaruhusu matabaka, unyonyaji na unyanyasaji miongoni mwa watu. Jambo hili lilimkera sana Mwalimu na hakusita kuliongelea mara kwa mara na kuliunganisha na suala la amani. Hali hii ilisababisha Mwalimu kupewa nafasi ya kuwa kiongozi katika usuluhishi wa migogoro mbalimbali hata mara baada ya kung’atuka na hili lilidhihirishwa na kutetea kwake haki, usawa na amani. Kwa upande wa Profesa Chachage hali ilikuwa hivyo pia. Pamoja na kwamba hakuwa kiongozi wa nchi kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere, Profesa pia alikuwa mtetezi mkubwa wa haki, usawa na amani. Kazi nyingi na machapisho ya Profesa yalisisitiza dhana hizi. Profesa Chachage aliamini ya kuwa hatuwezi kuongelea amani ya kweli kama tunaendelea kuwa na tabaka la watu wanaojilimbikizia mali ambazo wanazipata kutokana na unyonyaji, kunyonya tabaka lisilomiliki njia za uzalishaji. Na mara nyingi alisema kuwa amani tunayozungumzia ni amani ya juu juu (superficial) kwani hata wale ambao wamejilimbikizia mali wanaishi kwa wasiwasi na ndio maana wanaweka vizuizi katika milango yao pamoja na walinzi kwa hofu ya kuvamiwa na majambazi kwa mfano. Tunaona pia ya kuwa Profesa alipenda amani, usawa na haki na hili linathibitishwa na kufikwa na umauti wakati akiwa katika kazi aliyopewa ya kuratibu maoni ya Muungano.

Mitazamo ya Mwalimu Nyerere pamoja na Profesa juu ya masuala ya haki, usawa na amani inashabihiana. Lakini yatupasa tujiulize jambo moja, amani, usawa na haki vinavyohubiriwa leo hii na wengi miongoni mwa viongozi wetu vinatoka katika mioyo yao kwa dhati? Ni viongozi wangapi ambao wanahubiri usawa, haki na amani katika majukwaa na mikutano mbalimbali lakini wao wakiwa wamejilimbikizia mali, wakiendelea kuwanyonya walala hoi na hata kuwanyanyasa? Ni wangapi ambao kwa makusudi wamekuwa wakitumia nyadhifa zao na madaraka katika kuwakandamiza wanyonge wanaodai haki zao. Sote tunategemea ya kuwa vyombo vya dola na vya kisheria ndio mahali pa kukimbilia pale ambapo haki inakosekana, lakini tumesikia mara ngapi malalamiko ya watu kutotendewa haki katika vyombo hivyo? Mlinda sheria ndiyo anakuwa mvunja sheria, wapi basi raia wanyonge wasio na fedha wala madaraka waende kwa ajili ya kupata haki zao?

Mwalimu Nyerere alichukia sera kandamizi na mifumo ya kibepari na kibeberu. Mwalimu aliamini kuwa ni vigumu kwa wananchi kujikwamua katika hali ngumu kiuchumi kama mifumo ya kinyonyaji itaendelea kujikita katika nyanja mbalimbali za maisha yao. Hakusita wala kuwaonea haya mabeberu ambao kupitia sera kandamizi walizoziandaa wanafikiria njia za kukusanya utajiri kinyonyaji kwa vigezo vya misaada na soko huria. Mwalimu hakupenda kabisa ubinafsishaji wa mashirika na taasisi za umma na alikuwa akitamka wazi kabisa kuwa kufanya namna hiyo ni kukaribisha matabaka na kuruhusu kupenya kwa mirija ya unyonyaji, vitu ambavyo havishabihiani na haki, usawa na amani. Hata alipokuwa katika ziara mbalimbali katika mataifa ya nchi zinazojiita zimeendelea, Mwalimu hakusita kuwapa ‘vidonge’ vyao. Aliwaeleza wazi jinsi ambavyo tawala na sera zao dhalimu hazikuwa na maana kwa maendeleo ya bara letu na nchi zetu kwa ujumla. Mwalimu hakuwa msemaji wa nchi ya Tanzania peke yake, bali alikuwa kinara wa nchi zote zilizogubikwa na unyonyaji unaofanywa kwa kigezo cha maendeleo na mataifa hayo ‘teule’. Hakusita pia kuelezea athari za utandawazi na kuwataka wananchi kuwa makini nao.

Mtazamo na fikra za Mwalimu katika kuchukia mifumo hiyo havikutofautiana na Profesa Chachage. Profesa alipinga kwa nguvu zake sera za utandawazi ambao aliubatiza kwa jina la ‘utandawizi’ na aliona kuwa sera hizo ndizo zinazoletelezea umaskini mkubwa katika ‘nchi za dunia ya tatu’. Mfano mzuri ni katika moja kati ya kazi zake iliyochapishwa katika kitabu cha Globalisation and Social Policy in Africa kilichoandaliwa na CODERSRIA (Council for the Development of Social Science Research in Africa), yenye kichwa cha habari chenye tafsiri ya “Hitimisho- Ajenda ijayo: Zaidi ya Utandawazi”, Profesa Chachage alieleza kuwa kwa njia moja au nyingine utandawazi ndio umekuwa chanzo cha watu kukosa huduma za kijamii na kukosa kazi. Alisema pia kuwa utandawazi umewatupa watu katika shida na matatizo makubwa yasiyoweza kuvumilika. Usadifu huu wa mawazo na fikra juu ya mifumo hii kandamizi umeshabihiana sana na ule wa Mwalimu Nyerere. Tukiangalia kwa umakini, matatizo mbalimbali ambayo jamii yetu inakabiliana nayo kwa sasa, chanzo chake ni mifumo hii ambayo ‘manabii’ hawa walikuwa wakiipigia makelele waziwazi na kukuchukizwa nayo. Kinachotokea kwa sasa ni kunyamaza kimya kwa kuogopa kunyimwa misaada na mataifa haya huku tukijua fika ya kuwa tunaumia. Sifahamu hali hii itaendelea mpaka lini, lakini nafikiri kuwa hatuna budi kuiga mfano wa Mwalimu, Profesa na baadhi ya viongozi kama Hugho Chavez wa Venezuela na Fidel Castro wa Cuba ili tusikubali kuuza ‘utu’ wetu.

Bado kuna maeneo mengi ambayo Mwalimu Nyerere na Profesa walifanana. Nia ya makala hii si kuyazungumzia yote lakini ni kutoa changamoto kwa wasomi na viongozi waliopo sasa. Kazi kubwa iliyo mbele yao ni kuhakikisa kuwa maslahi ya taifa yanawekwa mbele kwanza na kusahau kabisa maslahi binafsi. Kinachotakiwa hapa ni uzalendo, na si uzalendo wa maneno bali wa vitendo. Tunapokuwa na uchungu na maendeleo ya nchi yetu na kuonesha kwa vitendo ndipo tunaposhiriki kikamilifu katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Wasomi watumie nafasi zao katika kufanya tafiti mablimbali zinazogusa maisha ya watu na kuweka wazi kipi kifanyike kwa ajili ya maendeleo ya pamoja. Viongozi wahakikishe kuwa mipango ambayo ina mtazamo wa kitaifa inatekelezwa kwa wakati kwa faida ya wananchi ambao wao ni sehemu yao. Tusiogope kuyumbishwa na wanaojiona wenye nguvu, tuzingatie uzalendo kama ambavyo Mwalimu Nyerere pamoja na Profesa Chachage walivyokuwa wakizingatia. Nia yangu si kusema kuwa hawa wawili pekee ndio walikuwa wazalendo kwa nchi yetu, nafahamu kuwa tunao wengine kadhaa. Lakini kinachotakiwa hapa si maneno bali matendo ya kila mmoja wetu kwa ajili ya faida ya nchi yetu, bila kujali dini, rangi, kabila, jinsia wala umri. Zidumu fikra za muasisi wa Taifa letu Mwalimu Nyerere pamoja na mwanazuoni Profesa Chachage!

* Mwandishi wakati akiandika makala haya, alikuwa ni Tutorial Assistant katika idara ya Sosiolojia na Anthropolojia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa sasa ni Assistant Lecturer katika idara hiyo hiyo, na ni mwanafunzi wa shahada ya Uzamivu (PhD), University College Dublin, Ireland, anapatikana pia kwa barua- pepe: magripinus@hotmail.com

No comments:

Post a Comment