25/03/2009

Utunzi: Nyenzo ya Uchambuzi wa Matatizo

Nauona utunzi kama njia muafaka ya kuchambua matatizo mbali mbali yanayokabili jamii yetu. Tofauti na zamani, utunzi kwa sasa ni kama umepoa poa vile! Nakumbuka kipindi kile tukiwa wadogo, sio tu kwamba tulikuwa na mshawasha wa kusoma kazi za watunzi mbalimbali, lakini pia ilikuwa ni faraja kusikia mtu anakusifia... Dah! unaghani kama Shaban Robert, au unaandika hadithi kama Musiba (zile za Willy Gamba). Ipo haja ya kuurudisha utunzi na kuufanya nyenzo ya kuchambua na hatimaye kupendekeza njia za kutatua matatizo yetu ya kijamii. Tatizo likichambuliwa kiutunzi linampa hamu hata msomaji kutaka kujua kwa undani ni nini hasa na hatimaye kuchukua hatua. Mimi na Mdau Kamarade Mroki Mroki, tumeazimia kurudisha tena utunzi, tukianza na ushairi. Hebu onja kwanza kidogo baadhi ya majibizano yetu ya kupeana hamasa hapa chini;
Mroki T Mroki
Ni jioni umewadia hapa kwetu Tanzania
nyote nawasalimia mhali gani jamia
Afrika na Ulaya pia Vipi mlo ninunia
Au ni kazi za vigunia Poleni ndo dunia.


Mathew Agripinus Senga
Wasaalamu Mroki,Senga nakusalimia,

Mlango sikuuloki,vijimambo ibukia,

Ndani wala sitoki,maandiko kuzamia,

Tutengenezeni meza, tuzizatiti tungo

Mroki kamarade,na malenga wengineo,

Tulipigeni parade,kwenye yetu maeneo,

Sote tuwe rede, tusivijali vyeo,

Tutengenezeni meza, tuzizatiti tungo
Wahenga wamenena, mwanzo huwa ni mgumu,
Lakini inasemekana, umoja ni wa muhimu,
Mnaposhikamana, hakuna wa kulaumu,
Tutengenezeni meza, tuzizatiti tungo
Tunaweza kuchapisha,majarida na vitabu,
Ng'ambo tukavivusha, kwa wazungu na waarabu,
Heshima tukaipandisha, tuwashikishe adabu,
Tutengenezeni meza, tuzizatiti tungo
Ni lazima tukiri, nchi yetu ni tajiri
Wala hatustahili,wazungu kutuajiri,
Kwa nini jambo hili, linaonekana dili?
Tutengenezeni meza, tuzizatiti tungo
Hivi kamarade Mroki, na wengineo malenga,
Hatuwezi kujidhiki, tungo tukazijenga?
Kueleza wanafiki, Tanzania twaijenga
Tutengenezeni meza, tuzizatiti tungo
Mroki T Mroki
Namshukuru Rabuka, afya njema alonipa,
Asubuhi pambazuka, nimeamka ubapa,
Nimeshaliacha shuka, tumboni nina mifupa
Tunaweza kwa umoja, nahakika tutafikaTunaweza kwa umoja, nahakika tutafika,
Senga meitoa hoja, Tanzania tasifika,
Tuunde wetu umoja, nasema tunajitwika
Tuanzisheni umoja, kuyakuza mashairi.


Muda unanikamata, nakimbia ofisini,
Wananchi wananiita, kero kuzitoa chini,
Mi hoja sitaifuta, taiweka hadharani
Tuanzisheni umoja, kuyakuza mashairi


Mathew Agripinus Senga
Mroki nimekupata,nazidi farijika
Na wala sitasita,juhudi kujivika
Ili umoja kupata,tuivuke mipaka
Wadau tuwajulishe,tuanzisheni umoja
Wala si jambo gumu,mimi navyofikiri
Kuhamasisha muhimu, ili wadau wakiri
Na wengine wajihimu, kuziweka nadhiri
Wadau tuwajulishe, tuanzisheni umoja
Mroki wafahamu wengi, wengi pia nawafahamu
Pale kwa mzee Mengi,Fungamwango ana hamu
Mwananchi wako wengi,wanoweza shika kalamu
Wadau tuwajulishe,tuanzisheni umoja
Hapo kwako mediani,malenga hawakosekani
Hata pale Mlimani, wamejazana kifani
Anza weka buloguni,waone wa ughaibuni
Wadau tuwajulishe, tuanzisheni umoja
Haya malenga wangu,ngoja nikaperuzi
Nishike vitabu vyangu,niuongeze ujuzi
Nisubiri malenga wangu,urudi kwenye upekuzi
Wadau tuwajulishe, tuanzisheni umoja

Umecheki mambo haya mdau??Jamani sasa si mnakubali utunzi nyenzo muhimu???

2 comments:

  1. Kazi kwelikweli, nami nita................

    ReplyDelete
  2. ANGELA JULIUS05/10/2011, 10:41

    WEWE NI NOUMA KWENYE MASHAIRI UTUNZI

    ReplyDelete