26/03/2009

Kamarade Mroki na Mabucha ya UtumboKamarade Mroki katika kuendeleza utunzi kama njia ya kuchanganua matatizo, ameibuka na shairi la Mabucha ya Utumbo. Hebu jionee anavyotiririsha vina kuelezea anachokiona kero;

Sija ufahamu pata, hadhi ya haya mabucha,
Utumbo wakula kata, pachafu kila kukicha,
Mabati ndio ukuta, mabanzi uchafu kucha,
Mabucha haya utumbo, kwanini sio masafi?Kwanini sio masafi?, Mabucha haya utumbo,
Hii wala sio haki, tutaumwa na matumbo,
Tunahitaji usafi, Vibandani sio fumbo,
Mabucha haya utumbo, kwanini sio masafi?Nipepita kila kona, Tandale mpaka posta,
Sijaona wakupona, muuzaji wakusota,
Nimtamu kinoma, Utumbo wakusokota,
Mabucha haya utumbo, kwanini sio masafi?Niambieni watunzi, wabara na visiwani,
Tutakaa fukuza nzi, hadi lini mabuchani,
Senga we ni mkufunzi, nakuhitaji safuni,
Mabucha haya utumbo, kwanini sio masafi?Mabwanaafya mijini, mehalalisha kwanini?
Ama mwakaa vitini, hamkemei kwanini,
Ondokeni ofisini, mkatepushe tafrani,
Mabucha haya utumbo, kwanini sio masafi?
Mtunzi: Mroki Mroki "Father Kidevu".
Ili kuendeleza libeneke la kutumia utunzi kama njia ya kuchambua matatizo, nilishika kalamu na kuendeleza hoja ya Kamarade Mroki. Jisomee;
Umenigusa Mroki,nilifikiri wajoki
Mada kuikoki,mabucha kuyashitaki
Umenena huropoki,uchafu huutaki
Ingawa utumbo mtamu,mabuchaye ni machafu
Ingawa utumbo mtamu,mabuchaye ni machafu
Unaweza ishiwa hamu,na moyoni kujaa hofu
Unapotoka zako homu, unusapo buchani harufu
Ingawa utumbo mtamu,mabuchaye ni machafu
Utumbo maarufu sana,wachaga hawatakana
Mtori wanajichana,kwa utumbo ule mpana
Na zile ndizi za kichana,na utumbo zawiana
Ingawa utumbo mtamu,mabuchaye ni machafu
Hapa kuna tatizo,linalo leta mzozo
Watendaji ni kikwazo,miji kuwa uozo
Hawa hawana uwezo, Mroki katoa wazo
Ingawa utumbo mtamu,mabuchaye ni machafu
Hatuwezi shika bakora,kuwatimua maofisini
Kalamu ni kitu bora,kuwafanya wawe makini
Waache kudorora,uvivu waweke chini
Ingawa utumbo mtamu,mabuchaye ni machafu
Mazingira watengeneze, semina waelekeze
Mate siye tuyameze, na wengine wawekeze
Mabucha yatengenezwe,usafi yafidikizwe
Ingawa utumbo mtamu,mabuchaye ni machafu
Senga siishiwi hamu,natamani kuendeleza
Mroki shika kalamu,malenga kuwahimiza
Bloguni na hata humu,watendaji tuwahimiza
Ingawa utumbo mtamu,mabuchaye ni machafu
Jamani wadau lakini mwaonaje suala hili la mabucha ya utumbo?Endelezeni libeneke hili malenga!!!!!

1 comment:

  1. Kaka shairi hili tangu jana tunaliona katika gazeti la habarileo, jana lilitoka la Mroki na leo huo Mwendelezo wako. Mnajitahidi sana.

    ReplyDelete