28/03/2009

Mgomba wamtatiza Kamarade Mroki

Safari hii Kamarade Malenga wangu Mroki Mroki "Father Kidevu" ameibuka na Swali kiutunzi....anatatizwa na mgomba kuzaa ndizi! Mmh inashangaza kidogo jamani wadau...si ndiyo? Hebu sasa soma hapa chini anavyojenga hoja. Mgomba nao....! Unamtatiza mpaka unamtatiza Mroki!

Mgomba kuzaa ndizi (Swali)

Asalamu salimuni, wa bara na visiwani,
Mhali gani jamani, wote ughaibuni,
Naja kwenu masikani, swali kuwatupieni,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.

Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini,
Mbona sio ka mbaazi, au mdalaasini,
Mkulima panda nazi, hutaivuna katani,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.

Utalima lako shamba, upande yako mazao,
Wapanda wako mgomba, na lingine lake zao,
Akivuna ajilamba, kwa matunda ya uzao,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.

Inatiza akilini, nataka jibuni watunzi,
Lipi jibu makini, mbegu halisi ya ndizi,
Wataalamu jibuni, toka SUA na uswazi,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.

Mgomba si kama hindi, au kunde na mtama,
Embe walimazo Lindi, zina mbegu za kulima,
Hata machungwa Kilindi, yanamsimu kuchuma,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.

Kila tunda linambegu, kasoro ya hii ndizi,
Mtaniona mimi Pwagu, namsakama Pwaguzi,
Nawauliza wa Magu, Nanyi hapo Mlandizi,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.

Ndizi tamu kwa kuliwa, ikiivia mgombani,
Ndizi tamu kwa kuliwa, ikipikwa majumbani,
Ndizi mbali na kuliwa, pika mbege uchagani,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.

Kilimo huwa Kagera, Moro nao Uchagani,
Mkungu huwa desera, ndizi zikiwa chanani,
Miche hutafutwa bora, kuzilima mashambani,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.

Utaupata mtwike, Kimalindi na ngazija
Ukiukata jitwike, mkungu hutaufuja,
Nyumbani ukaupike, nautumbo wa mrija,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.

Karata naimaliza, jokeri nawatupia
Senga ntakufatiza, jibu ukinitupia,
Malenga sitafukuza, simu napokea pia,
Mgomba kuzaa ndizi, haikai akilini.
By Mroki Mroki –“Father Kidevu”Box 9033 Dar es Salaam.Date 19/3/2009. Time 23:28hrs
Waweza pia kubofya hapa kulipata shairi hili;

No comments:

Post a Comment