28/03/2009

Mgomba Kuzaa Ndizi (Jibu)

Wadau nimeamua kumjibu Kamarade Mroki swali lake kuhusu Mgomba kuzaa Ndizi. Nifuate hapa chini tafadhali!

Mgomba ulomtatiza Kamarade Mroki na hawa jamaa inaonekana kama unawatatiza pia!!!

Mgomba Kuzaa Ndizi (Jibu)

Nilishtushwa kidogo, siku ishirini na sita
Kabla sijala muhogo, siku ipate kupita
Nilipofungua bulogo, ya Mroki majita
Malenga usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Kwanza nikajiuliza, malenga wangu kawaje
Akili yamtatiza, swali anaulizaje
Nini hasa anawaza, anataka tumjibuje
Malenga usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Nikawaza na kuwazua, jibu kumpatia
Kichwa nikasugua, vitabu nikapitia
Ndipo nikagundua, baada ya kufikiria
Malenga usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Mgomba unaelezewa, pulantae Kingidomia
Familia ulowekewa, Musaseae wanatuambia
Uwezo ulopewa, ni aseksho repulodakshonia
Malenga usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Kama umenisoma, sayansi naitumia
Najua haikupi homa, na maini kuumia
Inatusaidia kusema, ushahidi kutumia
Malenga usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Ipo mimea mingi, sifa sanjari na mgomba,
Unavipanda vigingi, inatoa kamba kamba
Unaipanda kwa wingi, inavizaa vyembamba
Malenga usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Sijataka geukia, uumbaji wa Rabuka
Mengi umeyasikia, sina haja kulipuka
Sayansi nimeitumia, ili hoja kuzisuka
Malenga usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Naona nimetosheleza, majibu nilokueleza
Kama bado wawaza, waweza endeleza
Kufafanua naweza, na SUA utawauliza
Malenga usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Tusiwanyime nafasi, malenga wafuasi
Nao wajiunge nasi, si tu kwa sayansi
Watoe ukakasi, utunzi ushike kasi
Malenga usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Kalamu naweka chini, kituo nasimamia
Nafuatilia kwa makini, maswali nasubiria
Kutoka magazetini, buloguni na wabia
Mroki usishangazwe, mgomba kuzaa ndizi

Mtunzi: Mathew Agripinus Senga
Tarehe: 21/03/2009, Saa: 7 Usiku

2 comments:

  1. Imekaa vizuri mkuu!

    ReplyDelete
  2. kwani muda wa kidhungu ni upi? UK? US? au?

    ReplyDelete