02/04/2009

Elimu ina Mchango gani juu ya Mgogoro katika Ubepari?

Hivi karibuni nilipata nafasi ya kuhuduria mhadhara ulionifurahisha hapa University College Dublin. Mhadhara huo wenye kichwa cha habari Crisis in Capitalism: The Role of Education mtoa mada alikuwa ni Profesa Stanley Aronowitz na kuandaliwa na UCD School of Social Justice. Profesa Aronowitz anafundisha City University of New York na miongoni mwa vitabu alivyotunga ni pamoja na kile maarufu kinachoitwa Left Turn Forging a New Political Future.
Ambacho kilinifurahisha katika mhadhara huo uliohudhuriwa na wanazuoni mbalimbali kutoka ndani na nje ya UCD, ni ule uwezo wa Profesa Aronowitz kuchanganua mambo kwa ule mtazamo wa mbali zaidi ya kuona (observation), ambao unaitwa Realism (kama unataka kutumia kidhungu). Profesa huyu alikuwa anaongelea namna ambavyo elimu inaweza kutumika kuwafanya watu kuuelewa kwa undani huu mgogoro mkubwa unaoendelea katika ubepari, ingawa wenyewe wanauita mgogoro wa kiuchumi (Financial Crisis), Profesa Aronowitz anaona zaidi kama ni mgogoro katika ubepari (Crisis in Capitalism).
Profesa alisema kuwa kuna haja ya kubadilisha mfumo wa elimu iliyopo sasa na kuifanya kuwa ya maana zaidi kwa kuwawezesha watu kutambua ubepari ni kitu kibaya na ambacho hakitakiwi katika maisha ya watu. Alisema, elimu hii itawafanya watu waweze kubadilisha mfumo wa kibepari ambao ni kandamizi na wa kinyonyaji. Alisisitiza kuwa jambo hili linawezekana kabisa, na kutoa changamoto kwa wanazuoni kuwa chachu ya mabadiliko hayo.
Maneno ya Profesa Aronowitz yalirindima kichwani kwangu na kuisogeza karibu taswira katika ubongo wangu. Nilikumbuka kipindi kile tukiwa darasani, na hata midahalo mbali mbali na mihadhara iliyokuwa/ inayoendelea kufanyika nyumbani Bongo. Kwa kiasi kikubwa ninakubaliana na maneno ya huyu Profesa mnazi wa itikadi za nguli Karl Marx. Kwa mapana na marefu hata mimi pia naona kuna haja ya kuangalia tena elimu hii tunayotoa na tunayoipata katika mashule na vyuo vyetu. Ina lengo gani, inatupeleka wapi na kwa manufaa ya nani?
Lakini zaidi, mada ya Profesa ilinifanya nione haja ya kuliweka wazi jambo moja. Hivi ni kweli kwamba watanzania masikini wanamfahamu adui wao wa kweli?Ukisoma na hata ukisikiliza msisitizo wa wahusika, watanzania masikini wanaelezwa kuwa adui wao namba moja ni umasikini! Na hapa ndipo tunapoona wahusika wanapopigana vikumbo kunadi mikakati ya kile kinachoitwa kupunguza umasikini! Sasa ukija katika mtazamo mpana na wa mbali, umasikini siyo kitu (thing) ambacho mtu anaweza kupigana nacho kwa nia ya kukishinda!Umasikini ni hali (condition) ambayo inaletelezwa na mifumo, mahusiano na michakato (kwa kidhungu structural and social relations, pamoja na social processes). Kinachotakiwa basi ni kukabiliana na hii mifumo, kama njia ya kukabiliana na hali inayoileta (umasikini). Kivitendo ni kumaliza mahusiano ya kinyonyaji na yasiyo ya usawa (exploitative relations na unequal social relations). Wanazuoni hapa wana kazi kubwa kama inavyobainishwa na Profesa huyu. Kuwafundisha watu adui zao wa kweli kabla ya kuanza kukabiliana nao. Ni kazi kubwa ambayo inahitaji kujitoa muhanga, lakini inawezekana, kwa umoja thabiti!
Profesa Stanley Aronowitz
Waweza kusoma zaidi kazi za Profesa Aronowitz kwa kubofya hapa http://www.globalresearch.ca/index.php?context=va&aid=11494
Wadau mnasemaje kuhusu mada ya Profesa huyu na mawazo yangu??

No comments:

Post a Comment