04/04/2009

Kumbukizi ya Martin Luther King Jr.

Martin Luther King Jr.

Jina la Martin Luther King Jr. si geni masikioni mwa watu (wakiwemo wanaharakati vijana wa sasa, ukiacha kundi kubwa la wazee). Martin Luther King Jr. mwanaharakati na mpigania haki za binadamu, hususani wamarekani weusi, leo ametimiza miaka 41 tangu auawe huko Memphis, Tennessee, Marekani.Mwanaharakati huyu ambaye ameacha jina ambalo halitafutika katika historia ya kupigania haki hapa duniani, alizaliwa Januari 15, 1929, Atlanta, Georgia, Marekani na alikuwa kiongozi maarufu wa changamoto za kuhakikisha ya kwamba weusi katika Marekani wanapata haki sawa na weupe. King aliupinga waziwazi ubaguzi wa rangi, na alisisitiza umuhimu wa weusi kupatiwa elimu ya mpaka ngazi ya chuo kikuu bure.Mwaka 1955 King aliongoza mgomo huko Montgomery ambao ulikuwa unapinga unyanyasaji na ubaguzi katika mabasi, na mwaka 1963 aliongoza maandamano maarufu kama "Maandamano ya Washington" ambapo alitoa hotuba yake maarufu ya "Nina Ndoto" (I have a Dream), hotuba ambayo baadhi ya maneno yake yametumiwa hivi karibuni hata na Rais wa Marekani, Barack Obama wakati wa kampeni za kumuingiza jumba jeupe (State House).Mbali na kupata tuzo ya Nobel miaka minne kabla ya kifo chake (1964), kufuatia mchango wake wa kupinga ubaguzi wa rangi na unyanyasaji kwa kutumia njia ya amani, King alianzisha na kuwa Rais wa kwanza wa Southern Christian Leadership Conference mwaka 1957. Mpaka kipindi cha kifo chake, King alijikita kupigia upatu jitihada za kumaliza umasikini na kupinga waziwazi vita vya Vietnam (akitumia mtazamo wa kidini pia).King anaendelea kuenziwa pamoja na kwamba kimwili hayupo duniani, na miongoni mwa tuzo alizojipatia baada ya kifo chake ni Presidential Medal of Freedom (1977) pamoja na Congressional Gold Medal (2004). Marekani iliitangaza Jumatatu ya tatu ya mwezi Januari kila mwaka kuwa sikukuu ya kitaifa ya King kama ishara ya kumuenzi.Binafsi namuona mwanaharakati huyu kama chachu kubwa ya changamoto za kutetea usawa na haki za binadamu, pamoja na kupinga ubaguzi wa rangi. Tuna mengi ya kujifunza kupitia kwa King hasa katika kipindi hiki ambacho tofauti kati ya matajiri na masikini inaendelea kuwa kubwa, pia unyonyaji na unyanyasaji unaofanywa na wamiliki wa njia kuu za uzalishaji mali dhidi ya makundi yasiyomiliki njia hizo.


Angalia video inayomwelezea na kumwonesha Martin Luther King Jr kwa kobofya hapa;
http://www.brasschecktv.com/page/590.html

No comments:

Post a Comment