10/05/2009

Tunamjongea zaidi Mungu kwenye vipindi vigumu tu?


Wadau leo Jumapili nimehudhuria ibada hapa University College Dublin (ee.. na mimi huwa napata wasaa wa kumwomba Mungu jamani!). Kwanza nilipigwa na butwaa kiaina baada ya kuingia katika nyumba ya ibada na kukuta imefurika waumini tofauti na ambavyo huwa jumapili nyingine. Nikajiuliza chap chap, kulikoni?! Nikakumbuka anhaaa... wanafunzi hapa chuoni sasa wanafanya mitihani. Nikaendelea kujiuliza, mbona jumapili nyingine nyumba hii ya ibada huwa inapwaya? Kipindi cha mitihani ndicho kimepelekea wanafunzi kukusanyika kwa wingi katika nyumba ya ibada na kukaza maombi yao kwa Muumba wao? Nikaona nisihitimishe kwanza nilichokuwa nikikiwaza.

Ibada ilipoanza, hususani kipindi kile cha mahubiri, ndipo nikahitimisha kuwa kumbe idadi hii kubwa ya waumini waliojaza kanisa imesababishwa na nilichokuwa nafikiria. Mchunga kondoo wa Bwana (wanamwita pia Padri) alianza kwa kutuvunja mbavu pale aliposema kuwa kuna ombi maalumu limepelekwa kwake kabla ya kuanza ibada na muumini mmoja ambaye alimuomba mchunga kondoo huyu ajaribu kufupisha mahubiri yake ili muumini yule na wengine wakawahi kusoma kwa ajili ya kujiandaa na mitihani!

Wakati mchunga kondoo akiendelea kutoa mahubiri ya kuwaasa waumini kutenda yanayompendeza Mungu, mawazo yangu mara kadhaa yaligubikwa na maswali, ina maana tunamuhitaji na kumjongea Mungu katika vipindi vigumu na labda tunapokuwa na shida zaidi ya vipindi vingine vyote?

Wadau mnaionaje hii?

No comments:

Post a Comment