05/05/2009

Ufisadi: Mengi tena aendeleza Libeneke

Bwana Reginald Abraham Mengi

MALUMBANO kati ya wafanyabiashara maarufu nchini Reginald Mengi na Rostam Aziz, yaliendelea jana kufuatia wanasheria wa Mengi, Michael Ngalo na Agapitus Nguma kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Rostam juzi huku wakiacha kujibu hoja nyingine na kuongeza maswali kadhaa waliyodai yanahitaji majibu.

Katika mkutano na waandishi wa habari mwanasheria wa Mengi, Michael Ngalo wa Ngalo & Company Advocates alijibu baadhi ya tuhuma hizo kwa niaba ya Mengi na kudai kuwa wako mbioni kumfungulia kesi Rostam Aziz kutokana na tuhuma hizo wanazodai kuwa ni za uongo.

Tuhuma zilizojibiwa na wanasheria hao ni kuhusu fedha za Import Support, kampuni ya Anche Mwedu Limited, utajiri wa Mengi, ukwepaji ulipaji kodi, fedha za misaada na kuwekeza katika biashara, uwekezaji wa kampuni ya NICO kwenye kiwanda cha Interchem Pharma Limited na kuwaita wengine ni wauaji.

Tuhuma ambazo hazikujibiwa na Mengi ambazo zilitolewa na Rostam ni kuhusu kuwa na akaunti ya fedha za kigeni nje ya nchi, malipo kwa wafanyakazi wake, kuhusu kuwa na ugomvi na baadhi ya viongozi na kutaka matatizo hayo yawe ya kitaifa na tuhuma nyinginezo.

Kuhusu fedha za Import Support, Ngalo alisema deni la fedha za import support zimeshalipwa tangu mwaka 2008 hivyo Mengi hana deni kama hilo huku wakionyesha kivuli cha hundi walizolipia deni hilo.

Kuhusu kampuni ya Anche Mwedu Limited alisema suala hilo liliamuliwa mahakamani katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupitia hukumu iliyosomwa Septemba 30 mwaka 2008 na dai la NBC kupitia Consolidated Holding Cooperation kwenye kesi hiyo lilikataliwa na mahakama kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kuthibitisha deni hilo.

Kesi hiyo ya madai nambari 197 ya mwaka 1993 ilifunguliwa na Anche Mwedu Limited dhidi ya Benki Kuu, kampuni za Societe General De Surveilanche S.A, SGS India Private Ltd, Consolidated Holding Corporation, Benki ya NBC na kampuni nyingine ya J.G. Vacuum Flasks Ltd.

Kuhusu ukwepaji kodi wanasheria hao walidai kuwa si Mengi wala kampuni yake yoyote ina tuhuma za kukwepa kulipa kodi.

Kuhusu uwekezaji wa NICO, Ngalo alidai kuwa si Mengi wala kamati ya uwekezaji ya NICO ilihusika kwa namna yoyote ili katika mchakato wa maamuzi ya kuwekeza kwenye kampuni ya Interchem kwa kuwa alipogundua hilo alijiuzulu nafasi ya Uenyekiti wa kamati ya uwekezaji na ujumbe na alifanya hivyo kupitia barua aliyoiandikia NICO Agosti 3 mwaka 2007. Aliwataka wanahabari kwenda NICO kuthibitisha suala hilo.

Hata hivyo Mengi kupitia mwanasheria wake aitwaye Nguma alimtaka Rostam kujibu maswali manne, la kwanza, likiwa la kutaka kujua anafanya biashara gani nchini na ataje biashara hizo anazoziendesha na pia kama kampuni zake zimesajiliwa BRELA kwa kutumia jina lake.

Pia alimtaka aeleze kama zinalipa kodi, na kuhusu kuwa hana uhusiano na Kagoda aeleze alikuwa akienda benki kujadiliana juu ya akaunti ya Kagoda alikuwa akifanya hivyo kama nani.

Kuhusu Dowans aeleze mipango ya benki kuipatia Dowans fedha za mkopo aliokuwa na aliushughulikia kama nani, na uhusiano na Richmond anawafahamu vipi wahusika wake.

Hatua hiyo ya Mengi kujibu baadhi ya tuhuma, na kutoa maswali hayo imekuja siku mbili baada ya mfanyabiashara Rostam Aziz kumlipua Mengi na kumbatiza jina la "nyangumi wa ufisadi" baada ya Mengi kumwita yeye na wenzake wanne kuwa ni mafisadi papa.

Rostam Aziz, ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara watano waliotuhumiwa na Mengi kuwa mapapa wa ufisadi, alitoa mlolongo wa tuhuma za ufisadi dhidi ya mwenyekiti huyo mtendaji wa makampuni ya IPP, na kueleza kuwa atawasilisha vielelezo kwa vyombo husika ndani ya saa 48 ili Mengi aanze kuchunguzwa.

Mapigo ya Rostam, ambayo yanazidi kupandisha joto la vita hiyo ya maneno, yametokana na tuhuma nzito ambazo Mengi alizitoa Aprili 23 wakati alipotaja wafanyabiashara watano akitaka wadhibitiwe mapema, akiwemo mbunge huyo wa Igunga.

Tofauti na Mengi ambaye hakutoa vielelezo hapo mwanzo wakati anawataja mafisadi papa hao na kusema yuko tayari kupandishwa kizimbani ili ukweli udhihirike, Rostam aliorodhesha tuhuma nyingi na kuahidi kuzikabidhi kwenye vyombo vya serikali ili hatua zichukuliwe.

Chanzo cha habari hii bofya hapa

Habari zinazoshabihiana na hii, kong'oli hapa na hapa

Haya wadau, sasa sijui ni zamu ya nani kuendeleza libeneke!tusubiri...mvumilivu hula mbivu ingawa wanasema samtaimz anaweza kula mbovu vile vile!

3 comments:

  1. Bado sijaelewa kwa migogoro kila kukicha

    ReplyDelete
  2. Dada Yasinta na kamarade Kamala,naamini katika falsafa ya migogoro kama chanzo cha maendeleo!Watu wanaweza kunishangaa kidogo hapa, lakini namaanisha kuwa kama jamii ya wanyonge inaendela kuwa submissive kwa wachache wenye uwezo na wamilikaji mali, hapo hakutakuwa na maendeleo ya wote katika jamii. Itaonekana tu wachache wameneemeka, wakati wengi wanateseka, kama tu ilivyo Tanzania kwa sasa. Hapa sasa dhana ya mgogoro kama chanzo cha maendeleo ndipo inaingia. Lazima wanyonge waanzishe vuguvugu la mabadiliko (ambalo walioneemeka wataliita mgogoro), kwa ajili ya kumaliza mianya inayopelekea wao kunyonywa na kuendelea kywa wanyonge, hatimaye kuleta usawa na maendeleo. Nafahamu kabisa kuwa si rahisi kwa jamii yote kuwa sawa, lazima kutakuwa na madaraja (maana dhana ya classless society ni ngumu kidogo),lakini kusiwe na tofauti kubwa kati ya walio nacho na wasio nacho. Tukirudi katika huku kutupiana maneno (ingawa wengine wanaita mgogoro) kati ya hawa wafanyabiashara, mimi naona hakuna mgogoro hapo! Maana wote wamejaaliwa neema (pamoja na kwamba wanao-take side watasema mzee Mengi anawasemea walala hoi), bado naona hakuna kigezo cha kuuita huu mchezo wa siasa- biashara kuwa eti ni mgogoro. Waache waendelee kuanika "siri" zao, zinatusaidia sana kuamsha utambuzi wa kweli na hatimaye true consciousness. Hapo ndipo tutaungana na kubomoa daraja lililopo kati ya walio nacho na wasio nacho! Ipo siku tu, tuwaache jamani waendelee "kumwaga kuku kwenye mchele wengi!"

    ReplyDelete