08/06/2009

Kizazi Hiki Kimelaaniwa?

Bhangi a.k.a jani, likivutwa huku moshi ukifuka

Wadau, jana nilipata nafasi ya kwenda kumtembelea tena Mama yangu kule Yombo, ili kumjulia hali. Bado afya yake haijatengamaa sawasawa, na zaidi hana hamu ya kula baada ya kufanyiwa ule upasuaji kutatua tatizo la utumbo kujikunja.

Nikiwa njiani, nilipita kumsabahi rafiki yangu mmoja maeneo ya karibu na wanapoishi wazazi wangu, huko huko Yombo. Ilipita takribani miezi minne tangu tuonane mara ya mwisho na rafiki yangu huyo ambaye ni kama vile tumekuwa pamoja kirika toka enzi zile nikiwa mwanafunzi wa Sekondari.

Jirani na nyumba ya rafiki yangu huyo, eneo linaloitwa Yombo Dovya- Mcharingeni, nilikuta kundi kubwa la vijana wakiwa wamekaa mbele ya nyumba moja ambayo haijamalizika kujengwa na inayooneshwa kutelekezwa (pagara). Vijana hawa ambao wengi wao walionesha kuwa wanafunzi wa shule ya msingi, walikuwa wanasokota na kuvuta bhangi (jani), mchana kweupeeee! Kwanza nilishikwa na bumbuwazi, maana pagara lile liko barabarani kabisa na wakazi walikuwa wanaendelea kupita na wengine kuendelea na shughuli zao za biashara ndogo ndogo, kama kuuza samaki na mihogo ya kukaanga karibu kabisa na eneo lile ambalo vijana hawa "mateja" walikuwa wanapiga "jani".

Niliziona hatari nyingi, kwanza kwa kuanzia mimi mwenyewe, kwa kuwa wakati nikiwa Dublin, nilidunduliza na kununua simu ya kiganjani, raba na mavazi kadhaa. Nilipowaona, nikaweka simu yangu mfukoni na kuongeza mwendo. Bahati nzuri hawakunisalimia, nami nikajifanya kama sikuwaona vile, huku roho ikinidunda, nikawapita kwa macho ya kuibia ibia nikaona jinsi ambavyo sura zao zilionesha kukomaa na misokoto na macho yao mekundu na yaliyolegea! Nikashusha pumzi baada ya kuvuka salama eneo lile.

Katika maongezi na rafiki yangu nikamuuliza, inakuwaje mnaishi na wavuta banghi eneo lenu? Akanijibu bwana wee rafiki yangu acha tu...hapa hakuna serikali, kila mtu ana serikali yake! Vijana wana serikali yao, na sisi raia kila mtu ana ka-serikali kake kanakomsaidia- kaserikali ka moyoni ka kuchukua tahadhari ya kutotembea majira mabaya na kutobeba vitu vya thamani! Nikasema kwanini wakazi msichukue hatua ya kuwashirikisha Polisi wa Kamanda Kova? Akasema hilo lishafanyika mara kadhaa, lakini polisi huwa wanakuja wa nadra na kuwatimua (huwa hawa mateja wanakimbilia bondeni na kutokomea). Wakiona kumetulia (mandata hawapo) wanarudi tena na kuendeleza libeneke!

Nilimuuliza huwa mnajadili zaidi nini kifanyike, akanijibu kuwa hakuna mkazi anayejali...wamewazoea mateja na huwa hawawakabi "roba" wakazi wa Mcharingeni, wao wanadili na wageni kama sisi (nikashukuru sikuwa kitoweo chao!). Tukaendelea kujadiliana na rafiki yangu yule, na nikajaribu kumweleza mtazamo wangu juu ya suala lile na nini kifanyike.

Wadau, mimi naliona suala hili kuanzia ngazi ya familia. Jinsi tunavyolea watoto wetu, na jinsi ambavyo sisi wenyewe tunalelewa. Nakubaliana kabisa na ukweli kuwa zama za utandawazi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuharibu watoto wetu, au sisi wenyewe kuharibika. Lakini tunafanya jitihada gani kukabiliana na changamoto hii? Tumekubali kushindwa? Tunaishia kusema kizazi hiki kimelaaniwa? Nadhani si sawa, bado familia ina mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa watoto wanakua katika malezi sahihi. Kumfuatilia kwa karibu mtoto ndani ya familia si kumyima uhuru! Ni kumsaidia kukua katika maadili mema.

Kupiga "jani" kuna sababu nyingi...kufuata mkumbo (mob psychology), kutaka tamaa, kumeguka kwa familia, na kadha wa kadha. Utandawazi kama nilivyosema una nafasi yake kubwa tu. Wengine pia wanasema ni umasikini, sawa inaweza kuwa sababu, lakini kwa hili tunapaswa kujiuliza, ni watoto wangapi wa masikini ambao wanavuta bhangi na kubwia unga, na ni wangapi ambao hawafanyi hivyo. Nasema hivi kwa sababu hata watoto wa matajiri wengine nao wanafanya hivyo. Ni suala pana ambalo mizizi yake inaanzia katika suala la uwajibikaji katika ngazi ya familia.

Naomba niishie hapa ili kukaribisha maoni ya wadau, jamani wadau ni kweli kizazi hiki kimelaaniwa?

4 comments:

 1. kizazi hiki kimalaaniwa? HAPANA ni kweli wazazi ni jukumu letu kwafuatilia watoto wetu. Ni kweli sio kuwanyima uhuru. Ni kweli watoto wengi wanafuata mkumbo, kwani wasipofanya hivyo wanakuwa nje ya marafiki yaani wankosa marafiki kwa hiyo ina kuwa kama ni lazima na inapokuwa lazima basi wanakwama kulekule. Yaani haiwi siku moja tu.
  Nshukuru mungu hukukuwa chakula chao:-)

  ReplyDelete
 2. Kizazi hiki wala hakijalaaniwa,kikubwa zaidi ni kuielimisha jamii,kuanzia shule za msingi na pia sisi wazazi tunatakiwa tujifunze jinsi ya kuongea na watoto wetu kuhusu hili tatizo.,jamani itafikia wakati mtu utashindwa kwenda matembezi peke yako.Una bahati sana kaka hukuwa kitoweo chao.Tunamuombea mama apate nafuu.

  ReplyDelete
 3. Nimeona hii article na imenigusa kidogo, haswa kwa sababu haya matatizo ya watoto (deliquency)yamekuwa ni jambo la kawaida mitaani mwetu. Japokuwa mimi simtalam wa soshologi, lakini naamini kwamba, momonyoko wa maadili katika jamii zetu ndio sababu kubwa ya haya matatizo. Suala la msingi ni kwamba, wazazi wa hao watoto wako wapi? serikali (POLISI) Iko wapi?Kwa kawaida, ilikuwa kwamba jamii nzima, yaani kuanzia jirani mpaka mtipa njia walikuwa na uwezo wa kumuadabisha mtoto yoyote anapoonyesha utovu wa nidhamu. Lakini leo hii kila mtu anaangalia pembeni kana kwamba alimuhusu.
  Kwa mtazamu wangu ni kwamba, mfumo wetu wa maisha umeanza kubadilika wa kasi kubwa. Ubinafsi ndio umetawala, kila mtu na maisha yake. Umaskini nao pia unachangia kwa kiasi kikubwa, leo hii wazazi wote wawili wanafanya kazi, hivyo watoto wanakuwa na UHURU kipita kiasi. Peer pressure nayo pia inachangia sana kuwarubuni vijana kuvuta bangi, wanadhani its COOL! au ndio UJANJA.
  Ukosefu wa KAZI (UNEMPLOYMENT) pia ni sababu kubwa inayowafanya vijana wetu kuangukia kwenye MADAWA YA KULEVYA. Kila unapopita unakutana na vijana wadogo wa umri wa miaka kuanzia 18-25 wamekaa vibarazani hawana chochote cha kufanya. Ni rahisi sana kutumbukuia kwenye hilo janga, AS WE ALL KNOW, AN IDLE MIND IS THE DEVIL'S PLAYGROUND. Vijana damu inachemka na hawana shughuli ya kufanya, hakika ni rahisi kupotea. Angalia vijana wetu wa mitaani wanavyo sniff petroli na gundi, history repeat itself.

  Kizazi hiki kimelaaniwa? La hasha, JAMII yatu imepoteza muelekeo, ubinafsi unaendelea kuota mizizi katika jamii zetu, na serikali hailipi kipaumbele kendeleza na kuboresha sekta ustawi wa jamii nchini mwetu. TUNACHELEA JUZIBA UFA MWISHO TUTAJENGA UKUTA.

  Sherbrooke- QC

  ReplyDelete