15/06/2009

Wadau Mwanasosholojia Yupo Yupo!

Jamani wadau Mwanasosholojia yupo yupo! Hapa ninamaanisha kuwa msione kimya mkadhani Mwanasosholojia hayupo, nipo wadau wangu nimebanwa tu na majukumu ya kuuguza, mama yangu mzazi na mtoto wetu aliyezaliwa tarehe 9 mwezi huu Dominic a.k.a Mwanashosholojia Jr.

Mama amehamishiwa Mission Mikocheni Hospital kutoka Kituo cha Afya cha Chuo Kikuu Mlimani, hali yake bado si nzuri. Tuna matumaini makubwa kuwa hali yake itakuwa nzuri tu na atapona. Mwanasosholojia mtoto naye alizaliwa na flu kali kiasi cha kushindwa kunyonya. Pia alizaliwa akiwa na matatizo kidogo katika mfumo wa upumuaji, kiasi cha kuwekewa vifaa vya kumsaidia kupumua na kupewa dawa katika chumba maalumu (incubator). Mpaka leo asubuhi ana mabadiliko makubwa na ameanza kunyonya maziwa ya mama yake. Huenda naye pia akaruhusiwa kutoka hospitali na mama yake muda si mrefu.

Pamoja na misukosuko hii na mahangaiko yote haya, leo nimejisikia hamu ya kutunga kidogo, naomba wadau wangu niwarushie tungo hizi chache za kujifariji katika kipindi hiki kigumu;

Ewe mama yangu mpendwa
Tambua kwamba unapendwa
Wala katu hujatendwa
Wewe sio wa kutendwa!

Jipe moyo mama yangu
Mfariji wa moyo wangu
Unayejua kuzaliwa kwangu
Uliyenizaa kwa uchungu!

Nipo karibu nawe mama
Nafurahi kuwa unahema
Ingawa huwezi kusema
Wala huwezi kusimama!

Jipe moyo utapona
Mungu anakupenda mbona
Wanakuhitaji wote wana
Tunapenda kukuona!

Wajukuu zako mama
Kuanzia walosimama
Hata wanaolalama
Wanakupenda sana mama!

Pona sasa mama yangu
Uje nyumbani kwangu
Uwaone na wanangu
Pinu,Mage na Domi wangu!




4 comments:

  1. Dah!!nimesoma hizi tungo na zimenigusa sana,tumtangulize Mungu katika kila jambo nina imani kabisa mama yetu,pamoja na mtoto Domi watapona na wataruhusiwa mapema.

    ReplyDelete
  2. Pole na majukumu,Mwanasosholojia.Muumba ampe uponyaji wa haraka mzaa chema (bimkubwa).Na kijana wetu asichelewe kukopi mema yote za Mwanasosholojia.Tuko pamoja.

    ReplyDelete
  3. Kaka Mwanasosholojia! kwanza pole sana tena sana nipo pamoja nawe.
    Nina imani maombi yako Mungu ameyasikia
    Na mama atapata nafuu na utakuwa naye
    Pia atacheza na wajukuu wake
    Najua hakuna kitu cha kufananisha kama mama.
    Nakuomba mpe pole toka kwangu.Mungu yupo nanyi nami nitakazana kutoa maombi yangu.

    ReplyDelete
  4. Tungo nzuri...Kweli, mama mtu mhimu. Shukran kwa kutujulisha kinachoendelea... mambo ya dunia sio rahisi..

    serina.

    ReplyDelete