04/07/2009

Bado Twamlilia Profesa Haroub Othman

Profesa Haroub Othman

Pamoja na kwamba mwanazuoni maarufu nchini Tanzania, Profesa Haroub Othman, amezikwa Jumatatu nyumbani kwao kisiwani Zanzibar baada ya kuaga dunia siku ya Jumapili akiwa na umri wa miaka 66, bado Jumuiya ya Wanazuoni ya Chuo Kikuu Dar es Salaam (CKD) tunamlilia, na pengine kuendelea kujiuliza kwa nini lakini umauti umemchukua mpendwa wetu wakati bado tunamuhitaji.

Binafsi nilimuona Profesa Haroub kama mwanazuoni mwenye uwezo usiomithilika, pamoja na kwamba tunaelezwa alisomea sheria ingawa alifanya kazi katika taasisi ya masomo ya maendeleo (Institute of Development Studies) ya CKD, mimi naona pia alikuwa Mwanasosholojia kufuatia uwezo wake wa kuchambua mambo yanayoizunguka jamii kwa kina. Kila nilipokuwa namsikiliza Profesa Haroub nilikuwa napata taswira ya nguli Profesa Chachage ambaye naye alitutoka miaka kadhaa iliyopita. Hakuwa mwoga kuelezea kile alichokiamini, tabia ambayo hata Profesa Chachage alikuwa nayo!

Tunazidi kupoteza wanazuoni mahiri, narudi kukisaili kifo, kwa nini lakini kifo? Nilipopata taarifa za kifo chake, niliamua kuandika kwa haraka tenzi zifuatazo;

Kweli kifo ni fumbo
Chaweza kukupiga kikumbo
Bora kingekuwa wimbo
Kuuimba au kuuacha!

Kifo kweli msamiati
Hakiji kwa wakati
Hata upange mkakati
Chaweza tokeza kati!

Profesa Haroub wa Othumani
Ni kweli wafukiwa mchangani?
Ni kweli umefichwa mautini?
Jamani wewe kifo kwa nini?

Kwa nini kifo lakini?
Hukumwacha yeye duniani?
Tutafanya nini jamani?
Hatunaye mwanazuoni!

Mikono yanitetema
Kwa taabu ninahema
Nikikumbuka yako mema
Ewe Profesa wetu mwema!

Changamoto umetuachia
Kizazi kilichobakia
Kabla mauti kuwadia
Tuyafanye uloazimia

Nashindwa kuendelea
Uchungu wanilemea
Pole nawatolea
Familia na ndugu pia!

Masaa machache baadaye, nilikutana na tungo nyingine iliyoandikwa na rafiki yangu mwanazuoni Stephen L Kirama kutoka Idara ya Uchumi ya CKD. Niliifurahia na inakwenda namna hii;

Tulisikia kwa dhati, Redioni Ukichati,
Wakikuweka mtu kati, ukawajibu kwa dhati.
Hukukiboronga kiti, Hoja ulizidhibiti,
Profesa Haroub Kwaheri, Mola akupe akhera.

Wahadhiri tunokua, kwako tulijifunzia,
Hoja kuzipangilia, bila hadhira kuboa.
Hoja zako ukitoa, hadhira ilitulia,
Profesa Haroub Kwaheri, Ukajaliwe akhera.

Uwezo wa kusikiza, wengi ulituvutia,
Hukujiweka wa kwanza, isipositahilia.
Hukupenda kujikweza, hata lipostahilia
Profesa Haroub Kwaheri, Mbingu saba uzifike.

Familia lobakia, Pole zetu twazitoa,
Mola nguvu kuwatia, hiyo sala twatolea.
Mkabaki mkijua, mwili umetangulia
Jina lake linaishi, na Daima litadumu.

Ugumu tunaujua, machungu pia kadhia,
mhimili kupotea, mtu ulomzoea.
Mama nawe tunalia, Pole zetu tunatoa
Profesa Saida Pole, Mola kampenda zaidi.


1 comment: