13/07/2009

Kwa nini Wabunge Wasifuate Mfano wa Mama Killango?

Mbunge wa Same Mashariki, Mama Anne Killango Malecela

Nimevutiwa sana na ujasiri ambao mbunge wa Same Mashariki, Mama Anne Killango Malecela anazidi kuuonesha. Nimefurahishwa na kitendo chake cha kuamua kumwaga mlolongo wa tuhuma za ufisadi kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii na kueleza kusudio lake la kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka kuundwa kwa kamati teule kuchunguza wizi wa nyara za serikali.

Mbunge huyo anataka tume hiyo ichunguze jinsi watendaji wa wizara hiyo walivyoshiriki kwenye usafirishaji wa makontena mawili yaliyosheheni nyara za serikali kwenda nchini Vietnam. Killango alitoa kusudio hilo bungeni wiki iliyopita akipinga bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyosomwa jana na Waziri Shamsha Mwangunga.

Akiwa mchangiaji wa kwanza wa hotuba ya bajeti ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo, Killango alisema wizi wa nyara unafanyika nchini kama vile hakuna ulinzi.

"Tanzania hatukustahili kuwa maskini kwa rasilimali hizi. Sielewi wizara imeshindwa nini kudhibiti wizi mkubwa kiasi hicho," alisema Kilango baada ya kuelezea wizi wa makontena mawili ya pembe za ndovu yaliyokamatwa wiki iliyopita nchini Vietnam.

"Mheshimiwa Spika naomba nizungumze kuhusu jambo ambalo kwa kweli limenisikitisha sana ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii; wizi wa nyara; wizi wa pembe za ndovu. Wizi huu Mheshimiwa Spika, unafanyika kama vile nchi yetu hakuna ulinzi," alisema Kilango.

"Nimefanya utafiti nina faili zima; Mheshimiwa Spika nilikwenda kufanya utafiti, baada ya kusoma kwenye magazeti kuhusu makontena mawili yaliyokamatwa Vietnam, nikaona nisiishie hapo niende ndani mpaka nipate faili zima.

"Nasikitika sana. Nilikwenda kuhoji; nikaelezwa; nikapewa na faili; nikasoma kontena zile mbili zilipitia bandari yetu kama kawaida."

Aliongeza kwamba katika hati za kusafirishia makontena hayo kinachoonekana kusafirishwa ni plastiki chakavu zinazopelekwa kubadilishwa na kutengenezwa bidhaa nyingine wakati ukweli halisi makontena hayo yalibeba pembe za ndovu.

Akizungumza kwa umakini mkubwa na kujiamini, Kilango alisema: "Mheshimiwa Spika naomba kwa kutumia kanuni ya 117 ya Bunge, kifungu cha 10(b), Mheshimiwa Spika niombe ruhusa kwako nitoe kusudio langu la kuleta hoja binafsi. Napendekeza kuomba tuunde kamati teule ya kulichunguza hili. Mheshimiwa Spika nielekeze taratibu zote nilete mapendekezo yangu iundwe kamati kwa jambo hili leo hii."

Alisema iwapo jambo hilo litaachwa bila hatua hiyo, mianya ya ufisadi katika Wizara ya Maliasili na Utalii aliyodai kuwa ni mikubwa, haitazibwa na kwamba huwezi kuvumilia kuona nchi ikiibiwa wakati serikali ipo imara.

"Lakini Mheshimiwa Spika nashindwa kuelewa hii Wizara ya Maliasili na Utalii imeshindwa vipi 'kuprotect' mali za Watanzania. Hili jambo ni kweli, tunaomba tuelezwe yamekwenda kwendaje kule. Hatuwezi kukubali nchi kuendeshwa hivi, hapana. Mheshimiwa Spika hapana; naomba nikuambie ukweli hili jambo ni zito. "

Alisema analo jina la mtu aliyetumiwa makontena hayo, lakini si kazi yake kuyataja na kwamba serikali ndiyo itatoa majibu ya kashfa hiyo.

"Mheshimiwa Spika, kama kuna ufisadi unaoua nchi yetu ni huu. Kwa kweli Mheshimiwa Spika ningepata dakika tano ningelia kwanza ndipo niendelee kusema. Kama kuna vitu vinavyomaliza nchi yetu ni hivi. Kontena mbili zimejaa nyara, pembe za ndovu.

"Vietnam wanatupigia simu; custom Vietnam ndio wanatupigia simu; wanapigia mamlaka zetu kwamba jamani huku kuna kontena zenu. Mheshimiwa Spika, sizungumzi kama chekechea, nimefanya research (utafiti) nina faili zima.

"... kwamba sasa watu wachache ambao ni wezi wanaamua kuharibu jina la serikali ya Chama Cha Mapinduzi, hatutaki.

"Mimi ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini watendaji wa aina hii hatutaki waharibu jina la chama chetu, hatuwataki."

Kilango alikuwa akizungumzia mzigo wa pembe za ndovu zenye thamani ya takriban Sh15 bilioni zilizokamatwa na maofisa forodha wa Bandari ya Hai Phong ya Vietnam Ijumaa iliyopita. Mzigo huo uliokuwa na pea zinazokadiriwa kufikia 200 za ndovu, uliondoka Bandari ya Dar es Salaam mwezi Januari.

Habari zinadai kuwa mzigo huo ulikuwa ukisubiriwa na mmiliki wake, ambaye alisemekana kutimka baada ya kupata habari kuwa polisi walikuwa wakimsaka. Akitoa maelezo kuhusu hoja hiyo, Spika Samuel Sitta alisema, kanuni ya Bunge inayoweza kutumika kuunda kamati teule ni ya 117 na kuwa kinachosubiriwa ni majibu ya serikali leo kabla ya kujua nini cha kufanya.

Ujasiri wa Mbunge Killango, ni wa kipekee hususani miongoni mwa wabunge wenzake wa CCM. Ninavyoamini mimi, kuna maovu mengi na uzembe unaosababishwa na kutowajibika ipasavyo, vitu ambavyo kwa pamoja vinajulikana na wabunge, lakini wamekuwa wakiendelea kukaa kimya na kutafuna posho kwa kuhofia "kufulia" pindi watakapoyatamka mabaya ya watendaji wa serikali. Hii ni nidhamu ya uoga lakini kikubwa, naichukulia kama "ufisadi ndani ya ufisadi". Kwa nini nasema hivi? Nasema hivi kwa sababu kubwa moja; Bunge ni chombo cha kutunga sheria sambamba na kuyaeleza na matatizo ya wananchi kupitia wawakilishi wao ili yaweze kufanyiwa kazi. Mbunge yeyote awe wa CCM au wa upinzani, kama hatekelezi hayo anashabihiana na fisadi.

Kila mtu anapenda maendeleo. Tanzania tunahitaji maendeleo ili utu wa mwananchi maskini uthaminike. Wabung e kama wawakilishi wa wananchi (tena ambao wamewafuata wananchi wenyewe na kuomba kura zao), wanapaswa kuwajibika. Kuwajibika si kuhudhuria vikao vya bunge kila inapobidi pekee, ni pamoja na kufanya utafiti na kuyafichua maovu yanayoangamiza nchi yetu, bila kujali itikadi za chama kama ambavyo Mbunge Killango anafanya. Hongera mbunge Killango, tumefurahi kusikia ulichotamka, Waziri wa Maliasili na Utalii pia amekiri "kisiasa". Kwa nini Wabunge wengine msifuate mfano wa Mama Killango?

Sehemu ya habari hii ni kupitia http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=13180

No comments:

Post a Comment