02/10/2009

Jibu la Kitendawili cha Mroki

Nimepata walau kadakika kamoja ka kumjibu Kamarade Mroki kwa tungo mbili tatu kufuatia swali lake juu ya mwenye mamlaka kati ya kondakta na dereva.

Mroki malenga wetu, salamuzo nimepata

Nakujibu mwanakwetu, nipo safi pasi tata

Ulichokiuliza kwetu, jibu lake utalipata

Mwenye mamlaka dereva, kondakta ni msaidizi


Kondakta ni msaidizi, mwenyewe umeonesha

Wala hafanyi ajizi, vituoni kutushusha

Hata kupiga uluzi, dereva kumgutusha

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi


Dereva ndiye mwamuzi, gari kulisimamisha

Anaviruka vihunzi, abiria kuwafikisha

Kumsikiliza msaidizi, ukweli si kubadilisha

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi


Anashika usukani, gari kuliongoza

Anapokuwa barabarani, kulipoza na kukoleza

Breki zi miguuni, aweza kuzichokoza

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi


Hakuna ubishi malenga, anayo mamlaka

Anaweza kukutenga, asisimame Malampaka

Matusi ukimlenga, atakuvukisha mpaka

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi


Nilipata walau dakika, Kamarade nimjibu

Naweza tena andika, kwa sababu ni wajibu

Ila ninayo hakika, ataridhishwa na jibu

Mwenye mamlaka dereva, kondakta msaidizi

3 comments:

 1. Safi sana kaka,sikujua wewe ni mwandishi wa tungo.Kweli kabisa mwenye mamlaka dereva,kondakta msaidizi.

  ReplyDelete
 2. Kuna wakati sina uhakika Dereva aendeshaye nchi-Tanzania ni nani hasa!

  Hivi kuna uwezekano watu kutostukia kuwa kumbe dereva ni kondakta ?

  ReplyDelete
 3. Kaka Kitururu, yawezekana kabisa, labda abiria tunaendeshwa na dereva "asiye dereva"

  ReplyDelete