02/10/2009

Mroki na Kitendawili cha Dereva na Konda!


Kamarade Mroki amerusha swali kupitia tungo. Anauliza juu ya mwenye mamlaka kati ya dereva na kondakta. Maswali yake yanatiririka namna hii;

Wabilahi tawafiki, nyote nawasalimuni,
Nyote msio na chuki, habarari za nyumbani,
Sibagui marafiki, na mlio ofisini,
Kondakita na dereva, nani mwenye mamlaka.


Nani mwenye mamlaka, dereva na kondakita,
Mtu akitaka shuka, tamtafuta kondakta,
Dereva utamruka,mlango utaufata,
Kondakta na dereva, nani mwenye mamlaka.


Breki ipo kwa dereva, unaanza muita konda
We konda shusha Kizava, njiapana kihonda,
Kazi hiyo ya dereva, vipi wamuita konda,
Kondakita na dereva, nani mwenye mamlaka.


Yamkini upo mbele, siti karibu na suka,
Inakutoka kelele,eti unatakashuka,
Ukae kiti cha mbele,kituo muite suka,
Kondakita na dereva, nani mwenye mamlaka.


Konda atakuitika, kisha tamjuza suka,
Shusha mmoja kafika,siunge mwambia suka,
Breki huzifinga suka, kituoni ukifika,
Kondakita na dereva, nani mwenye mamlaka.


Konda hukusanya fedha, ndo yake kazi muhimu,
Hujiongezea adha, na wingi wa majukumu,
Kuwaita abiria, askari kwa walimu,
Kondakta hastahili, kulisimamisha gari.


Dereva anastahili, kulisimamisha gari,
Hata matuta mawili,suka talizima gari,
Yupo makini kwahili,muonapo msafiri,
Kondakta hastahili, kulisimamisha gari.


Mwisho ninamalizia, kituoni nimefika,
Kitini sikusinzia,siokwamba sijachoka,
Jibu nasikilizia,sote weze faidika,
Kondakta hastahili, kulisimamisha gari.Mtunzi: Mroki Mroki (Father Kidevu)
"Bepari wa Kikamba"
Box 9033, Dar es Salaam
Email. mrokim@gmail.com
+255 7171 002303
Tanzania.


Haya wadau, mwenye majibu anakaribishwa, nafikiria fikiria kumjibu huyu mtunzi

No comments:

Post a Comment