09/02/2010

Shule za Sekondari za Kata Dar na Matokeo ya Kidato cha Nne!

Wanafunzi wa sekondari wakiwa darasani

Wakati matokeo ya mitihani ya kumaliza kidato cha nne yakiwa yametangazwa, imefahamika kuwa shule za sekondari za kata, mkoani Dar es Salaam, zimefanya vibaya kutokana na wanafunzi wengi waliohitimu masomo katika shule hizo mwaka jana kufeli mitihani hiyo.

Matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) mwishoni mwa wiki, yanaonesha kuwa kati ya shule hizo, 26 zilizoko katika Wilaya za Kinondoni na Temeke, zimefanya vibaya baada ya jumla ya wanafunzi wake 2,321 kufeli, huku 2,963 wakifaulu kwa kiwango cha daraja la nne.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, kati ya shule zilizofanya vibaya, baadhi zimefikisha wanafunzi 119, nyingine 129 na nyingine 176 waliofeli, huku waliofaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza wakiwa ni 45.

Jumla ya waliofaulu kwa kiwango cha daraja la pili katika shule hizo, ni 120 wakati waliofaulu kwa kiwango cha daraja la tatu wakiwa 533.

Hii ni changamoto ya aina yake kufuatia ukweli kwamba matokeo haya ni ya kwanza tangu kuanzishwa kwa shule hizo na serikali mwaka 2006 ili vijana wengi wanaohitimu elimu ya msingi waweze kupata elimu ya sekondari. Wasiwasi mkubwa ulioneshwa na watu wengi tangu kuanza kwa mpango huu kufuatia changamoto kama vile uhaba wa vifaa kama vile maabara na maktaba pamoja na walimu wenye uzoefu na sifa. Ikumbukwe kwamba walimu wengi waliopelekwa katika shule hizi ni wale waliohitimu kidato cha sita na kisha kuhudhuria kozi ya miezi mitatu ya nadharia ya ualimu maarufu kwa jina la "voda fasta". Hapa mwanasosholojia hana nia ya kubeza sifa za walimu hawa, la hasha! Lengo ni kuainisha umuhimu wa utoaji elimu katika viwango vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi sambamba na uwepo wa nyenzo muhimu.

Zinahitajika juhudi za makusudi ili kuboresha shule hizi kuwawezesha wanafunzi wake waweze kufanya vyema.

No comments:

Post a Comment