03/03/2010

Nipo kwa ajili yako!

Ninakupenda mpenzi, ulonijaa moyoni

Daima nitakuenzi, siku zote maishani

Nakutungia utenzi, uelewe ya rohoni

Nipo kwa ajili yako, ewe wangu maabuba


Hainipiti dakika, bila kukufikiria

Sikufanyii dhihaka, ukweli nakuambia

Umeniteka hakika, mpenzi nakuapia

Nipo kwa ajili yako, ewe wangu maabuba


Nikosapo kukuona, moyoni ninaumia

Mpweke ninajiona, uchungu nagugumia

Mara tu nikikuona, furaha inanijia

Nipo kwa ajili yako, ewe wangu maabuba


Tunapokuwa pamoja, wanipa raha hakika

Tumeujenga umoja, ewe wangu malaika

Tusivifanye vioja, penzi letu kuvunjika

Nipo kwa ajili yako, ewe wangu maabuba


Daima nakutunzia, hili penzilo mwanana

Moyoni nakuwekea, usipate shaka sana

Popote napoelekea, usiku hata mchana

Nipo kwa ajili yako, ewe wangu maabuba

2 comments:

 1. Shairi limetulia kweli kaka nadhani uliyemtungia atafurahi au amefurahi kweli.

  ReplyDelete
 2. Wewe ni langu chaguo, mwinginewe sijamwona,
  Wewe si sawa na nguo, na mwingine kufanana,
  Upendo wangu ni huo, kwingine kote hakuna,
  Hakika nitakuenzi, kwa maisha yangu yote!

  ReplyDelete