01/07/2011

Unajua 'Linalomdatisha' Mpenzi Wako?

Hakuna jambo linaloleta furaha na amani katika maisha ya kimapenzi kama kumsoma mpenzi wako na kujua mambo gani 'humdatisha' kisha ukamtimizia.

Hicho ndicho ambacho kimewafanya baadhi ya watu kufikia hatua ya kusema kwamba, mpenzi aliyenaye hatamani kumkosa hata kwa siku moja katika maisha yake. Wako watu wamekaa katika ndoa kwa miaka 25 ukiwauliza siku ambazo wamewahi kutokuwa pamoja hesabu yake kwa pamoja haitimii miezi 6.

Huo ndiyo ukweli wenyewe. Watu wananenepa, wanatakata na kutawaliwa na nyuso zenye furaha wakati wote kwasababu tu wanapatiwa kile kitu ambacho mioyo yao inapenda. Wengi ya wapenzi wa siku za hivi karibuni ukikutana nao wamezeeka, wamesinyaa, wamepata makunyanzi. Yote hata si kwamba yanatokana na umri kwenda, lahasa, wana kidonda moyoni, kidonda kinachowafanya kukunja uso wakati wote na kupelekea kuzeeka kabla ya wakati.

Wewe ungependa kuingia katika maisha hayo hasi? Sidhani, kama sivyo basi leo hii nataka kukufahamisha mambo ambayo yanaweza kuyaingiza maisha yako katika hatua nyingine, hatua ya furaha iliyotimia, furaha itakayopeleka kutabasamu tena, kuponya donda lako la moyo, na kuendelea kuonekana kijana japo umri unakwenda.

Wewe ni binadamu uliyekamilika ambaye hisia zako zimekutuma kumpenda mtu fulani ambaye naye ameonesha kukupenda? Hiyo ni bahati sana kwako lakini bado unakuwa na jukumu lingine la kuweza kumfanya huyo uliyempenda akupe nafasi kubwa katika moyo wake kiasi cha kumfanya asisikie la kuambiwa juu yako.

 
Unajua anachokipenda?
Yawezekana mmeishi kwa muda mrefu katika uhusiano wenu, je, umeshamsoma mpenzi wako na kujua mambo ambayo ukimtendea huwa anachanganyikiwa mnapokuwa faragha au sehemu nyingine? Kama tayari, nikupe ‘bravo’ lakini kama bado jaribu kuchunguza, la sivyo utaanza kuzeeka.

Yawezekana kuna siku ulimfanyia mpenzi wako kitu fulani akakuambia maneno haya, “Napenda sana unaponifanyia hivi mpenzi wangu, hakika unanifanya nizidi kukupenda”. Hakuna maneno matamu kama haya hasa unapoyasikia kutoka kwa mtu uliyemkabidhi moyo wako, wengine huenda mbali zaidi na badala ya kusema tu huenda mbele zaidi na kuonesha shukrani zake kwa vitendo.

Cha kufanya sasa, mfanyie hayo hayo kila mara na ikibidi wakati mwingine usisite kumuuliza, “Baby hivi unapenda nikufanyie nini zaidi ili ujue nakupenda? Zungumzeni, chunguzaneni kwa yale yanayowafurahisha, sio afya kuchunguza kama unaibiwa peke yake.

Kama ni muwazi atakurahisishia kwa kukuambia yale yanayomdatisha lakini wengine ni wagumu kusema hivyo itakuwa ni kazi yako kumdadisi, naamini ukiwa makini utagundua.
Unaziteka hisia zake?
Muwapo faragha, mfanye mpenzi wako azielekeze hisia zake kwako. Si wakati wa kuanza kumzungumzia mtu ambaye unahisi anatoka naye kwani kwa kufanya hivyo utamfanya aanze kumfikiria tena huyo unayemhisi badala ya kukufikiria wewe. Zungumza naye kwa upendo, mbusu kwenye shavu, mnong'oneze sikioni, mguse nywele zake, mtazame kama vile ndio unamwona leo kwa mara ya kwanza, fanyeni yote haya bila hata kuvuana nguo. Chezeni na kucheka kama watoto, ndio maana mkawa na chumba chenu wawili tu, hiyo ni faragha yenu, oneshaneni 'uchizi' wenu.

Uwapo naye jua kwamba ni wewe pekee mwenye nafasi katika maisha yake. Ondoa hisia hasi kuhusu yeye badala yake muda wote uutumie kumfanya aamini kwamba unampenda na umuweke katika mazingira ya kutofikiria kukusaliti kwa namna yoyote ile.

  Wewe ni mtundu na mbunifu?
Utundu wako na ubunifu katika uhusiano wako unaweza kumfanya mpenzi wako ahisi yupo na mtu wa kipekee. Hutakiwi kuwa yule yule kila siku bali unatakiwa kubadilika na kuwa tayari kujifunza. Mapenzi yanahitaji shule na shule hii si lazima uingie darasani. Muulize rafiki yako wa karibu, mbona nikimfanyia hivi mpenzi wangu anakuwa hivi? Naamini atakusaidia. Rafiki huyu awe ni yule mnayependana na kuaminiana kwa dhati, rafiki wa kufa na kuzikana, naamini marafiki wa aina hii bado wapo.

Wasiliana na wataalam wa mambo ya uhusiano au tembelea mitandao ya mapenzi, huko kuna mambo mengi yanayohusu namna ya kuboresha uhusiano wako, utajifunza na kuwa bora! Kwa taarifa yako ni kwamba, hata kama una umbo zuri na sura ya kuvutia, kama si mtundu na mbunifu kwa laazizi wako huwezi kudumu naye. Atalazimika kukuacha na kuangalia mtu mwingine anayejua maisha na mapenzi.

Jamani mapenzi yana raha yake, kama huamini waulize akina fulani. Ukifanikiwa kutengeneza furaha katika uhusiano wako, hata maisha yako yatakuwa ya furaha na utashangaa unanenepa tu hata kama huli chakula.

Chanzo: Bofya HAPA

3 comments:

  1. hii imetulia kaka safi sana

    ReplyDelete
  2. KWA KWELI NI UKWELI MTUPU, ILA KWA SASA MAPENZI YA KWELI NI AGHALABU SANA , EE MUNGU UTUSAIDIE.

    ANGELA JULIUS

    ReplyDelete