11/09/2011

Ajali ya Meli Zanzibar:Mtazamo na Tafakari

Meli ya LCT Spice Islanders kabla ya kuzama. Picha hii ilipigwa mwaka 2010, Stone  Town, Zanzibar.
 
Wengi tunafahamu kutokea kwa tukio baya na la kusikitisha lililogharimu maisha ya watu zaidi ya 160 na majeruhi zaidi ya 600 (takwimu za makadirio za mpaka jana usiku), baada ya meli ya abiria LCT Spice Islanders, iliyokuwa ikisafiri kutoka Unguja kwenda Pemba, kupinduka na kuzama baharini. Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa meli hiyo iliyokuwa imebeba abiria zaidi ya 600, ilizama usiku wa kuamkia jana kwenye Bahari ya Hindi kati ya Nungwi na Pemba, kilomita 20 kutoka Bandari ya Zanzibar. Kwa mujibu wa habari hizo, meli hiyo iliyotokea Unguja kwenye Bandari ya Malindi, ilipata hitilafu ikiwa njiani, kisha ikapinduka na kuanza kuzama taratibu. Ilikuwa na makoti ya uokoaji 200 tu.

Ni habari zinazoumiza sana na zinazosababisha si tu masononeko bali maswali kibao, tafakari na mitazamo tofauti tofauti. Watu wengi wanaliongelea tukio hili kama moja ya matukio mabaya sana kutokea Tanzania na kugharimu maisha ya watu wengi, sambamba na lile la kuzama kwa meli ya Mv Bukoba, tarehe 21 Mei, 1996.

Ado M. Kibogoya Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma (UDASA) wa Chuo hicho analitafakari tukio hili kwa ufupi;

"...Tunawapa pole wale wote waliohusika katika ajali hii na kumwomba Mwenyezi Mungu awapumzishe mahali pema peponi wote waliopoteza maisha.

Wakati tukihuzunika na msiba huu ni vema tukatafakari yaliyotokea na kuangalia mbele. Sina budi kusema kwamba inasikitisha kwamba tunasherehekea miaka kumi ya ajali ya Mv Bukoba kwa kuingia tena kwenye msiba mwingine kama ule! Cha kutisha ni kwamba ajali imetokea ya NAMNA ILEILE, KWA SABABU ZILEZILE NA KWA MTINDO ULEULE !! Sitakosea kusema kwamba ajali hii ni AJALI PACHA NA ILE YA Mv BUKOBA. Ajali zote mbili zimesababishwa na wingi wa abiria pamoja na mizigo kupita uwezo wa vyombo husika! Pili, chombo hiki kinasemekana kilikuwa kibovu na kimekuwa hakifanyi kazi kwa zaidi ya miaka miwili!!

Hapa kuna maswali mengi ya kujibu, na kwa ustaarabu mdogo inabidi watu wawajibike. Tumejifunza nini baada ya Mv Bukoba? Zinatakiwa Mv Bukoba ngapi ili tujifunze kitu? Serikali na vyombo vyake (SUMATRA, Polisi, n.k.) wanafanya nini, kwa nini makosa yaleyale yanaendelea kupoteza maisha ya watu wetu? Kama ni kweli chombo hiki kilikuwa kibovu ni nani amekifanyia matengenezo na kukiruhusu kirudi majini? Na ni nani amekikagua akathibitisha ubora wake?

Haitoshi kwetu sisi kuwa tayari kulia na kusononeka kila litokeapo tatizo; tunapaswa  KWENDA MBALI ZAIDI KWA KUTAFUTA SABABU NA KUZUIA TATIZO LISIJIRUDIE. Ushujaa wa kuendesha misiba ya kitaifa sio kitu cha kujivunia, na hasa kama misiba hiyo inasababishwa na uzembe. Tuangalie tusifike mahali ambapo tutakosa haki ya kuyaita matukio kama haya 'ajali', kwani ajali haitegemewi. Haya, kwa kutumia akili ndogo tu, ni wazi tunayatengeneza na kwa hiyo yanategemewa! Nimemsikia mtu mmoja anasema tusiingize siasa wala jazba kwenye hili; lakini ninajiuliza hapa siasa iko wapi na kwa faida gani! Uzembe ni uzembe bila kujali umefanywa na nani; isipokuwa inauma zaidi uzembe unapofanywa na vyombo vinavyopaswa kulinda na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao..."
Anamalizia Daktari Kibogoya.
Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mh. Zitto Zuberi Kabwe analitizama tukio hili kwa kuyaandika haya;
"...(Nimeandika makala haya nikiwa katika Benchi la Hospitali ya Mnazi Mmoja hapa Zanzibar. Mniwie radhi kama kuna spelling mistakes kwani nilitaka hisia zangu ziwe as raw as possible -Zitto Zitto and not Zitto a politician).

Jana asubuhi tarehe 10 Septemba 2011 Taifa liligubikwa na habari za kushtusha za maafa. Mwanzoni taarifa zilisambaa kwamba zaidi ya watu 2000 walikuwa kwenye Boti MV Spice Islander lililopinduka na kuzama mbele kidogo ya Nungwi likielekea kisiwani Pemba.

Habari hazikuwa za uhakika sana kwani vyombo vyetu vya habari na hasa Televeshini ya Taifa havikuwa vikitoa habari juu ya ajali hii. Habari zilisambaa kupitia mitandao ya intaneti na kufuatia uchu wa habari nilianzisha #ZanzibarBoatAccident katika mtandao wa twitter ili tuweze kufuatilia kwa karibu habari zote za ajali hii.

Habari zilisambaa kuwa Televisheni ya Taifa ilikuwa inaonyesha muziki wa Taarab na Baadaye vipindi vingine vya kawaida bila kutoa habari kwa Umma kuhusu msiba huu.

Watanzania waliokoa wakiwasiliana kupitia twitter na facebook walikuwa na hasira sana na kituo cha TBC1 kutoonyesha au kupasha habari juu ya ajali hii. Mpaka saa moja jioni kituo hiki cha Televisheni ya Taifa kilikuwa kinaonyesha watu wakicheza muziki wa Kongo, wanawake wakikatika viuno na hata ngoma za asili. 'Hallo, washa TBC1 uone Televisheni yenu inachoonyesha' yalikuwa ni maneno ya Mwakilishi Ismael Jussa Ladhu aliponipigia kuonyesha kusikitishwa kwake na kituo hiki. 

Mpaka jioni tulikuwa tumepata taarifa kuwa Watanzania wenzetu 198 walikuwa wamepoteza maisha. 570 hivi walikuwa wameokolewa. Binafsi nilipotembelea Hospitali ya Mnazi Mmoja niliweza kumwona Binti aliyeitwa Leyla, akisoma darasa la Nne huko kisiwani Pemba. Leyla alipona, aliokolewa. Nilimwambia leyla atapona na kurudi Shuleni. Mpaka ninapoandika tumeambiwa kuwa Watanzania 240 wamegundulika kupoteza maisha na zaidi ya 600 wameokolewa. Napenda kuwapongeza sana waokoaji wetu, wavuvi wa kijiji cha Nungwi na vijiji jirani, wamiliki wa mahoteli waliojitolea vifaa vyao kwenda kuokoa watu na wanajeshi wetu wa majeshi ya ulinzi na usalama kwa kazi hii kubwa ya kuokoa. Kwa kweli tumeokoa watu wengi kuliko ilivyotarajiwa. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejitahidi sana, ilitulia na kuonyesha uongozi dhabiti katika juhudi za uokoaji.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akafuta ziara yake huko Canada, ziara iliyokuwa imeandaliwa muda mrefu na kwa gharama. Lakini Rais aliona ni vema kupata hasara kuliko kuwa nje ya Nchi kipindi hiki. Hakutaka hata kumtuma Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Alifuta. Akatangaza siku 3 za kuomboleza. Hata hivyo waandaaji wa Miss Tanzania waliona hasara kubwa kuahirisha shindano la Urembo usiku huo. Wangepata hasara! Hata wafadhili wao Kampuni ya simu za mkononi ya vodacom ambao miongoni mwa waliofariki wamo wateja wa vodacom, waliendelea na shindano hili. Jumatatu, tarehe 12 Septemba 2011 ni siku ya khitma ya kuwaombea marehemu wetu. Nimeamua kutotumia simu ya ngu ya Voda kwa siku nzima, sina njia ya kuiadhibu Kampuni hii isipokuwa kugoma kutumia simu yao japo kwa siku moja kuonyesha kutoridhishwa kwangu na uamuzi wao wa kutojali msiba huu kwa Taifa. 

Misiba huweka jamii pamoja. Msiba huu uliotokea Zanzibar ni jaribio kubwa kwa Umoja wa Taifa letu. Shirika la Utangazaji la Taifa limeshindwa jaribio hili la kudhihirisha Umoja wetu katika kipindi hiki. Nataraji wakubwa wa Shirika hili linaloendeshwa kwa kodi watawajibika au kuwajibishwa!

Jumla ya Majeruhi na marehemu sasa inafikia zaidi ya Abiria 800! Asubuhi ya jana 10 Septemba 2011 tuliambiwa na Serikali kwamba uwezo wa Boti la MV Spice Islander ilikuwa ni abiria 500 na wafanyakazi 12. Pia tumejulishwa kuwa boti hili lilikuwa la Mizigo na sio la Abiria. Natumai mara baada ya kumaliza maombolezo haya ya siku tatu Wakuu wa Mamlaka zinazohusika na usafiri wa Majini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar watawajibika au kuwajibishwa. Mkuu wa Bandari ya Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe na Waziri wa Miundombinu Hamad Masoud wanapaswa kufukuzwa kazi mara moja kama hawatawajibika wenyewe kwa kujiuzulu.

Kufukuzwa kwao kazi hakutarudisha ndugu zetu duniani bali itakuwa ni somo kuwa hatutarudia tena kufanya makosa yaliyoleteleza ajali kama hii.  

Mwenyezimungu atupe subira wakati huu wa msiba mkubwa katika Taifa letu. Alaze roho za marehemu wetu mahala pema peponi na awape unafuu wa haraka majeruhi wetu..."

 Huo ni mtazamo na maoni ya awali ya Mheshimiwa Zitto kufuatia tukio hili baya. 

Tuna uwezo wa kulichambua tukio hili kwa mapana na marefu na hata kupendekeza njia za kujikinga kwa majanga kama haya katika siku zijazo. Lakini kabla ya kufanya hivyo, tunapaswa kujiuliza kwa majanga ambayo yametokea mpaka sasa, hakuna watu waliothubutu kutoa mapendekezo ya nini kifanyike baada ya ajali na majanga kama haya? Je tumetekeleza ushauri au mapendekezo yako kwa kiasi gani mpaka sasa?
Hapa lazima nikiri kuwa sisi watanzania ni wepesi sana wa kusahau mambo, lakini zaidi sio watu wa vitendo au kwa ufupi, tumekuwa watu wa maneno kwa muda mrefu sasa, huku mzaha mzaha ukisababisha kutumbua usaha! 
Kwa nini tusiwe kama wenzetu, ambao makosa kama haya huwa yakitokea hayaambatani na maneno (ikiwemo bahati mbaya...kazi ya Mungu haina makosa..na  kadhalika) bali huambatana na vitendo thabiti vinavyotekelezwa ipasavyo kuzuia kurudiwa tena kwa majanga yale yale, yanayogharimu maisha ya wenzetu namna hii. Jamani, wakati umefika sasa wa sisi kuacha haya masikhara kwa uchu wa fedha au kutotimiza wajibu wetu ipasavyo!

2 comments:

 1. Nianza kwa kutoa pole kwa Msiba huu wa kitaifa, nahuita wa kitaifa kwa sababu tumepoteza ndugu zetu wengi kutoka pande zote yaani Tanzania bara na Visiwani.
  Pili idadi ya watu iliyopotea ni nguvu kazi kubwa kwa taifa. Tumepoteza kizazi cha sasa namaanisha watu wazima na vijana umri wa kati na kizazi kijacho namaanisha watoto waliokufa ajalini.
  Baada ya pole hii, napenda kueleza kuwa ajali hii ni ajali ya kushangaza kwa sababu iliwahi kutokea kama hii kule kwetu Bukoba, ni ya kushangaza kwa sababu serikali haikujifunza hata kidogo japo ya watu zaidi 1000 wali kufa maji kitika ziwa victoria.

  NI ya kushangaza kwa sababu inasemakana sababu zile zile ndizo zilizopelekea ajali hii kutokea.
  Msiba ni msiba ila uchunguzi ni lazima, japo dukuduku langu na wasi wasi wangu ni juu ya tume/kamati zinazo undwa kisha kutokomea na ripoti za matukio na sintashandaa kuona kimya kingi baada ya maziko.

  Tatizo kubwa nchini mwetu ni upungufu au kutokuwepo kabisa kwa uwajibikaji sahihi, watu wanawajibika pale matukio yanapotokea hasa ya vifo, hakuna hatua madhubuti zinazoweka kudhibiti au kuzui kabisa matukio hatarishi kama haya.

  Matatizo tunayoyaona katika idara au vitengo mbali mbali serikalini adhari zake ni kama
  hizi.

  Naungana na watu waliotoa maoni yao na hasa Mh zito aliyesema anategema watu husika kuwajibishwa baada ya tukio hili.

  Jamani, namalizia kwa kusema tujali maisha yetu na ya wenzetu, wewe kama ni dereva wa gari endesha kwa umakini wajali watembea kwa miguu, kama ni mwendesha traini goma kuendesha kama imejaa watu zaidi ya uwezo, kama ni nahodha wa meri goma kuendesha chombo kama mzigo ni mkubwa kuliko uwezo wa meli. Hakika tutaweza okoa maisha ya watu wengi.

  Mungu zilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
  Mungu ibariki Afrika
  Mungu Ibariki Tanzania

  Dezidery.

  ReplyDelete
 2. Nianza kwa kutoa pole kwa Msiba huu wa kitaifa, nahuita wa kitaifa kwa sababu tumepoteza ndugu zetu wengi kutoka pande zote yaani Tanzania bara na Visiwani.
  Pili idadi ya watu iliyopotea ni nguvu kazi kubwa kwa taifa. Tumepoteza kizazi cha sasa namaanisha watu wazima na vijana umri wa kati na kizazi kijacho namaanisha watoto waliokufa ajalini.
  Baada ya pole hii, napenda kueleza kuwa ajali hii ni ajali ya kushangaza kwa sababu iliwahi kutokea kama hii kule kwetu Bukoba, ni ya kushangaza kwa sababu serikali haikujifunza hata kidogo japo ya watu zaidi 1000 wali kufa maji kitika ziwa victoria.

  NI ya kushangaza kwa sababu inasemakana sababu zile zile ndizo zilizopelekea ajali hii kutokea.
  Msiba ni msiba ila uchunguzi ni lazima, japo dukuduku langu na wasi wasi wangu ni juu ya tume/kamati zinazo undwa kisha kutokomea na ripoti za matukio na sintashandaa kuona kimya kingi baada ya maziko.

  Tatizo kubwa nchini mwetu ni upungufu au kutokuwepo kabisa kwa uwajibikaji sahihi, watu wanawajibika pale matukio yanapotokea hasa ya vifo, hakuna hatua madhubuti zinazoweka kudhibiti au kuzui kabisa matukio hatarishi kama haya.

  Matatizo tunayoyaona katika idara au vitengo mbali mbali serikalini adhari zake ni kama
  hizi.

  Naungana na watu waliotoa maoni yao na hasa Mh zito aliyesema anategema watu husika kuwajibishwa baada ya tukio hili.

  Jamani, namalizia kwa kusema tujali maisha yetu na ya wenzetu, wewe kama ni dereva wa gari endesha kwa umakini wajali watembea kwa miguu, kama ni mwendesha traini goma kuendesha kama imejaa watu zaidi ya uwezo, kama ni nahodha wa meri goma kuendesha chombo kama mzigo ni mkubwa kuliko uwezo wa meli. Hakika tutaweza okoa maisha ya watu wengi.

  Mungu zilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
  Mungu ibariki Afrika
  Mungu Ibariki Tanzania

  Dezidery

  ReplyDelete