“Nguvu za masikini mtaji wa matajiri….masikini hana mtaji”
Na. Emmanuely Deodath Lyimo
“Mtaji wa
masikini ni nguvu zake” kati ya semi maarufu za lugha ya Kiswahili. Lakini
nimewahi kujiuliza upi mtaji wa tajiri?. Hii
inatokana na wasiwasi niliokuwa nao kama kweli masikini hufaidika kadiri ya
nguvu anazotumia katika kuzalisha. Kabla sijafika mbali ni muhimu kujiuliza hivi
mtaji ni nini? Kadiri nijuavyo mimi mtaji ni mzunguko wa fedha na rasilimali
ambazo zinawekezwa katika kuzalisha faida, kwa maana hii fedha zilizoko mfukoni
au benki bila ya kuwa katika mzunguko wa kuzalisha faida haziwezi kuwa mtaji.
Katika mfumo wa
kibepari, ili kuzalisha faida fedha hutumika kunulia bidhaa kubwa mbili: nguvu kazi na zana za uzalishaji. Nguvu kazi ni ule uwezo wa mfanyakazi kuzalisha
bidhaa au huduma, kwa upande mwingine zana za uzalishaji ni mashine, eneo la
kufanyia kazi pamoja na malighafi. Hivyo basi nguvu kazi huwa mtaji pale inapotumika katika kuzalisha
faida.
Tofauti na
wakati wa utumwa ambapo watumwa walikuwa wanamilikiwa kikamilifu, katika mfumo
wa kipepari mabepari wamekuwa wakinunua na kumiliki uwezo wa mfanyakazi/nguvu
kazi ili kutengeneza faida. Hivyo basi katika mfumo wa kibepari nguvu kazi ni
bidhaa ambayo inaweza kuuzwa na kununuliwa.
Kwa maana hii basi,
katika mfumo huu wa kibepari ambao ndio unaoongoza uzalishaji wa bidhaa, uuzaji
wa bidhaa sokoni, kilimo, siasa na kila Nyanja ya maisha yetu haiwezekani hata
kidogo kwa masikini kumiliki hata nguvu kazi yake mwenyewe. Hata ajitahidi
kufanya kazi kwa bidii kiasi gani, nguvu zake zitaendelea kuwa mtaji wa mtu
mwingine aliyenunua uwezo wake wa kuzalisha mali.
Ikumbukwe kuwa,
nguvu kazi ndiyo bidhaa pekee yenye uwezo wa kuzalisha thamani zaidi wakati wa
uzalishaji wa bidhaa kuliko gharama iliyowekezwa awali. Njia pekee ya kupata
faida hii ni kwa kumlipa mzalishaji pungufu ya kile anachozalisha, njia hii ya
kupata faida inaitwa unyonyaji.
Kwa maana hii
usemi huu ni sehemu ya propaganda za mabepari kuendelea kutoa matumaini ya
ndoto za alinacha kwa masikini ili waendelee kuwanyonya kiulaini. Katika fikra
pevu kamwe kisichokuwa chako hakiwezi kuzalisha faida ikawa yako. Badala ya
masikini kuzidi kufanya kazi kwa bidii katika mfumo huu wa kibepari ambao
hauruhusu wao kutengeneza faida ni lazima wajitahidi kupambana ili kurudishiwa uwezo
wa kumiliki nguvu yao kwanza.
Walalahoi
wanajukumu la kijikomboa wao na kila kilicho chao, ikiwemo nguvu kazi yao
halafu ndipo wanze kuitumia katika kujikomboa kiuchumi. Hapa ninamaanisha kuwa,
kabla ya kuamini kuwa mlalahoi anaweza kujiinua kiuchumi kwa kumfanyia bepari
kazi kwa bidii lazima akatae kunyonywa. Maana kabla ya fukara kupata kitu kwa
kufanya kazi kwa bidii katika mfumo huu wa kibepari, basi bepari atakuwa
amepata mara mbili zaidi yake.
Ninamaliza kwa
kutoa changamoto kuwa mtaji wa masikini katika mfumo huu wa kibepari ni mtaji
wa matajiri wanaowanyonya mafukara ambao ni wakulima na wafanyakazi. Katika
mfumo wa kibepari masikini hana mtaji ila ndoto za alinacha zisizo na tija
zinazowafaidisha mabepari kila uchwao. Tuamke tuwe na fikra sahihi, tukatae
vimisemo vinavyotupa matumaini yasiyofika milele!!!!
Mmmh!
ReplyDeleteDeo, nzuri sana.
ReplyDeletePamoja na kujaribu kutambua unyonyaji dhidi yetu, bado tunaendelea kufanya kazi. Hii si ndo Marx aliita "false consciousness"?
Tunatambua kuwa tonanyonya, lakini hatuna hatua ya kudai haki zetu.
Wafanyakazi wa umma, taasisi binafsi, Civili societies, japo si sana na wengine wote katika industry nchini, tusimame tutee utu wetu, tusipofanya hivyo hakuna atakaye tutea.