25/10/2009

Kuna Asiyependa Kwao?

Leo nikiwa njiani narudi nyumbani, hapa uwanja wa ndege wa Cork nimepata hamu ya ghafla ya kutunga tungo mbili tatu za kuelezea nyumbani. Pamoja na safari yangu ughaibuni kunichukua kama wiki mbili tu, nilikumiss nyumbani!


Nyumbani ni nyumbani jamani, hata kuwe kwa namna gani
Wahenga hawakuwa punguwani, kuliweka wazi barazani
Hata usafiri kote duniani, utarudi nyumbani mwishoni
Kuna anayesema asilani, Hapendi kwao jamani?


Nimekaa na kuwaza vilivyo, pasingekuwepo nyumbani
Kila kitu kingekuwa hovyo, tungekosa raha duniani
Tungetangatanga visivyo, bila kuwa na maskani
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?


Wasanii nao wanaimba, nyumbani kwako ni nyumbani
Kwa zao tungo wanatamba, luningani na redioni
Ni nyumbani wanakuimba, kumwaga sifaze jamani
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?


Pamoja na umuhimuwe, kuna wengine wakubeza!
Wamejawa na kiwewe, na maisha ya kuigiza
Hawataki kwao kamwe, wanaranda wakibangaiza
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?


Hawa wamejisahau, kutukuza ugenini
Wanasahau nahau, kujiweka utumwani
Kwenda kwao walau, hawawazi akilini
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?


Mwenzenu napenda kwetu, hata nipewe nini,
Siwezi utupa utu, kwa kupenda ugenini
Kwetu kunabaki kwetu, nakupenda kama nini
Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?

2 comments:

  1. Nanukuu "Mwenzenu napenda kwetu,
    hata nipewe nini,
    Siwezi utupa utu, kwa kupenda ugenini
    Kwetu kunabaki kwetu, nakupenda kama nini
    Kuna anayesema asilani, hapendi kwao jamani?" Dr: Remmy Ongala aliimba wimbo wake mmoja hivi:- Narudi nyumbani, narudi Peramiho nakwenda kula likolo la nanyungu,nyumbani kwako ni nyumbani hata kama kukiwa porini.....na kuendeleaaa. Napenda kuamini hakuna asiye na nyumbani.

    ReplyDelete
  2. Tatizo kubwa ni kwamba kunawafikiriao kuwa walikokuwa na nyumba au walikotoka wazazi wao ndio nyumbani.

    Swala ni rahisi kulielewa kama unastukia kuwa kuna MGOGO nyumbani kwake ni Dar-es Salaam ingawa akijieleza hivyo kuna watakaofikiria hajivuniii DODOMA asiyoijua.:-(

    ReplyDelete