18/10/2009

Wahi Nakala yako ya Chemchemi

Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Issa Shivji

Kigoda cha Kitaaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu Dar es Salaam kimetoa toleo la pili la Chemchemi lililozinduliwa rasmi na Makamu Mkuu wa Chuo mwezi huu. Toleo hili ni la Kiswahili.

Bodi ya uhariri ya Jarida hilo inabainisha kuwa ndani ya toleo hili mna makala mbalimbali kama vile; Haja na Namna ya Kutoa Elimu ya Uraia Tanzania (Bashiru Ally) Tafsiri na Muhtasari wa Kijitabu cha Hamidu Ismail Majamba Kiitwacho 'Uwezekano na Mantiki ya Kuanzisha Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara (Aldin Mutembei), Edward Moringe Sokoine na Mapinduzi Vijijini (Issa Shivji) na kadhalika. Pia kuna makala ya Dkt. Mwami juu ya Ulimbikizaji wa Mtaji kwa Unyang'anyi Chini ya Ubeberu Nchini Tanzania (kwa taarifa ya ziada: Dkt. Mwami anakaribia kumaliza tafsiri ya Das Kapita kwa Kiswahili!)

Vile vile toleo hili lina mazungumzo marefu kati ya Shivji na Kingunge Ngombale Mwiru yaliyoandaliwa na Jacquiline Mgumia. Katika mazungumzo haya Ndugu Ngombale Mwiru anazungumzia maisha yake ya kisiasa tokea alivyojiunga na TANU miaka ya 1950, jinsi alivyokwenda kusoma Liberia na kwanini alikimbia Liberia na kwenda kusoma Dakar, Senegal na kadhalika. Shivji anamdodosa Ngombale jinsi CCM ilivyotoa Mwongozo wa mwaka 1981 wenye uchambuzi wa kitabaka chini ya Mwalimu Nyerere ilhali Mwalimu alikuwa hakubaliani na mtizamo wa kitabaka. Na je, Ndugu Ngombale anateteaje "Azimio la Zanzibar" wakati yeye bado ni muumini wa Ujamaa?

Mazungumzo mengine ni juu ya Muungano wa Tanzania kati ya Shivji na Ismail Jussa (CUF), Bakari Mohamed (Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala CKD), Ng'wanza Kamata (Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala CKD, Chris Peter (Shule ya Sheria), Bernadetha Killian (Shule ya Uandishi wa Habari) na Adolf Mkenda. Mambo makuu mawili yanajadiliwa, chimbuko la muungano na muundo wa muungano.

Pia kuna mapitio ya kitabu cha Mohamed Said (kilichotafsiriwa na A.S. Mkangwa). Kitabu hiki kinaitwa "Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924-1968): Historia Iliyofichwa Kuhusu Harakati za Wailsam Dhidi ya Ukoloni wa Waingereza Katika Tanganyika" Mpitiaji wa kitabu Adolf Mkenda.

Toleo hili lina pia CD ya wimbo wa kusisimua wa Karola Kinasha- wimbo alioutunga mahsusi kwa ajili ya Wiki ya Tamasha la Kitaaluma la Mwalimu Nyerere na kuuimba kwa mara ya kwanza kabisa pale Nkrumah. Waliokuwepo pale Nkrumah watakumbuka jinsi wimbo huu ulivyoshangiliwa na kusisimua. Karola amekubali CD hii iambatane na kila toleo la Chemchemi bila kudai malipo yeyote.

Mwisho, toleo hili lina pia kumbukizi ya Haroub Othman iliyoandikwa na Chris Peter na shairi lililotungwa na Shivji. Beti kadhaa za shairi la Mwalimu Nyerere pia zimechapishwa. Baadhi ya beti hizo ni hizi hapa;


1.Tanzania yetu ina

Watu aina aina:

Inao hao Wapemba

Watochomewa majumba,

Sera hii ikipita

Bila ya kupigwa vita.


2.Lakini ina Wahaya,

Na Wasumbwa na Wakwaya,

Ina Waha na Wamwera,

Na Wakwavi, na Wakara.


3.Ina Anna ina Juma,

Ina Asha ina Toma,

Kadhaka ina Pateli,

Na wengine mbali mbali.


4.Uhasama ukipamba

Mkafukuza Wapemba,

Anajua ni Manani

Mbele kuna mwisho gani.


Jipatie nakala yako kutoka kwa Walter Luanda (0754 281 837)

Taarifa hii ni kwa hisani ya Dkt. Adolf Mkenda wa idara ya uchumi, Chuo Kikuu Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment