04/11/2009

Barua ya wazi kwa Mheshimiwa Mkapa

Rais Mstaafu Benjamin Mkapa (kushoto) akiwa na Rais wa Finland, Tarja Halonen


Mwanasosholojia amefurahi kuisoma barua ya wazi ambayo Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Issa Shivji ameandika kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania, Mheshimiwa BenjaminWilliam Mkapa. Ni hii hapa...

Mheshimiwa Mkapa,

Assalam Alaykum.

Nakuamkia kwa heshima na taadhima. Natumai u mzima wa afya, wewe na familia yako. Nakuombea kila la heri na mapumziko mema, pamoja na majukumu yako mengi na mazito ya kimataifa.

Mheshemiwa, nimeshawishika kuandika barua hii baada ya kusoma kwenye tovuti (http://businessmirror.com.ph/home/opinion/14843-the-sudden-demise-of-neoliberal-economics.html) maoni yako ambayo yamenukuliwa na mwandishi wa habari Roberto Savio akiandika juu ya kifo cha uliberali mamboleo katika gazeti la Business Mirror la 19 Agosti 2009. Umenukuliwa ukisema:

“We privatized everything the state had. Everything was bought by foreign capital because we had no national capital to compete. The foreign companies almost always closed local businesses, which were not competitive, transforming them into distributors of foreign products and driving up unemployment. The experts of the World Bank and the IMF predicted that this would happen, but they told us: Now the influx of foreign investment will lead to the creation of new, competitive and technologically current businesses that will provide the foundations for a lasting, modern development. None of this happened for us.”

“Tulibinafsisha kila kitu kilichokuwa mikononi mwa dola. Kila kitu kilinunuliwa na wawekezaji kutoka nje kwa sababu hatukuwa na mtaji wa ndani wenye uwezo wa kushindana. Makampuni ya nje yakafunga mashirika ya ndani kwa sababu hayakuwa na tija na yakayageuza mashirika haya kuwa wachuuzi wa bidhaa kutoka nje na kwa hivyo kuongeza watu wasio na ajira. Wataalam wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa walitabiri kwamba hivyo ndivyo ingekuwa, lakini wakatuambia: Uwekezaji kutoka nje utazaa taasisi za kibiashara za kisasa, zenye uwezo wa kushindana, na teknologia ya kisasa, na kwa hivyo kujenga misingi ya kudumu ya maendeleo ya kisasa. Hakuna lolote kati ya hiyo lililotokea nchini mwetu”.

Mzee, unasononeka; kwa kiasi fulani, katika lugha yako ya kidiplomasia, unalalamika. Lakini hata baada ya maanguko ya mfumo wa uliberali mamboleo na utandawazi, ambao uliushabikia sana wakati wa utawala wako, hukuwa na ujasiri wa kuomba msamaha wa watu wako. Sikulaumu. Huwezi kulaumiwa. Ni hulka ya binadamu kutokuona au kukiri kosa lake. ‘Nyani haioni ngokoye.’ Katika hili huko peke yako. Katika mkutano wa kundi la nchi 20 (G20) zenye nguvu za kiuchumi ulioitishwa mjini London kuzungumzia hali mbaya ya uchumi mnamo Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu wa Uingereza, Bwana Gordon Brown, alikiri kwamba ‘Muafaka wa Washington umekufa’, alisema hivyo bila kuwaomba radhi watu wa ulimwengu, hasa wa nchi maskini, ambao waliathirika sana na “muafaka” huo wa nchi za kibeberu ambao nchi zetu zililazimishwa kuufuata.

Mheshemiwa Rais mstaafu: Ukweli ni kwamba haya yaliyotokea sasa si matokeo yaliyokuja kwa bahati mbaya au kwa miujiza tu. Wako viongozi na hasa wasomi (angalau wachache) walisema, tena kwa uchambuzi wa kina na yakinifu, kwamba mfumo huo hautufai, hautatuletea maendeleo, bali utauongeza tu unyonywaji wa watu wetu na uporwaji wa mali zetu. Mwalimu Nyerere alijitahidi sana kupinga masharti ya nchi za kibeberu, lakini hakufanikiwa. Mzee Mwinyi alifungua milango na wewe ukakumbatia, bila kuhoji mfumo huo, hasa masharti yale ya kubinafsisha mashiriki ya umma. Ni kweli mashirika mengine hayakuwa na tija, ni kweli pia mengine yalikuwa na menejimenti mbovu. Lakini je, tulijaribu kutafuta njia mbadala, licha ya hiyo ya kubinafsisha ‘kila kitu’? Wasomi wako wachache waliokosoa sera zako za kiuchumi uliwaita majina na kuwafananisha na ‘wavivu wa akili’. Ulipigia sana debe utandawazi kiasi kwamba jina lako litaingia katika historia kama mvumbuzi wa neno ‘utandawazi’ katika msamiati wa Kiswahili. Uliwafumbia macho viongozi wako wakati wakitumia vyeo vyao kujilimbikizia mali na utajiri wa kupindukia – au hili pia ilikuwa ni sera ya kujenga mabepari wa ndani?

Mbaya zaidi, mheshimiwa, chini ya uongozi wako tukakubali kutoa uhuru kwa taasisi za kifedha, na kukubali soko huria katika biashara ya fedha, (na kutokudhibiti akaunti ya mtaji (capital account)) bila udhibiti na usimamazi wowote wa dola. Hili ndilo hasa lilikuwa chanzo cha chumi zetu kuathirika kupita kiasi pale anguko la mfumo wa fedha wa kimataifa lilipotokea.

Nchi ambazo zilikataa soko huria katika mambo ya fedha, kama China na Malaysia, hazikuathirika kama nchi zingine. Naomba nisiendelee. Wananchi wetu, pamoja na kutokuwa na usomi au ustaarabu wako au wangu, wanahisi moyoni mwao udhaifu wa mfumo wa utandawazi na binamu yake uliberali mamboleo. Ndio maana wakati wa kuadhimisha miaka kumi tangu kifo cha Mwalimu, wakalilia sana Azimio la Arusha.

Mwalimu hakuwa malaika, alikuwa kiongozi wa kisiasa. Alikuwa na mapungufu yake lakini alijali watu wa chini, watu ambao walisahaulika kabisa katika awamu ya tatu na wanaendelea kupuuzwa katika awamu ya nne. Kila mlalahoi aliyetoa maoni yake alikuwa na maneno haya tu: Mwalimu alitujali; Azimio la Arusha lilitujali sisi wanyonge. Azimio lilitoa matumaini. Uliberali mamboleo na utandawazi ulitoa matumaini yapi kwa matabaka ya chini, zaidi ya kuwa njia ya viongozi kujilimbikizia mali bila aibu!

Mheshemiwa Rais mstaafu, sio nia yangu kurudia yale yaliyotokea. Lakini, utakubaliana nami kwamba historia ni muhimu. Kujifunza kutokana na historia yetu na ya wengine ni hatua ya kwanza katika safari ndefu ya kujikomboa na kujiletea maendeleo halisi. Kama kweli umejifunza na umeyaona madhara ya sera ulizozikumbatia wakati ukiwa madarakani, je, huoni kwamba una wajibu wa kumsaidia mrithi wako, na hasa kutusaidia sisi wananchi, ili tujifunze kutokana na makosa ya serikali yako? Je, kweli, bado unanadi na kutunasihi kwamba utandawazi hauepukiki? Je, bado unatushauri kwamba msukumo wa maendeleo ni uwekezaji kutoka nje, uwekezaji ambao umejidhihirisha wazi ni uporaji wa maliasili yetu? Je, huoni kwamba unao wajibu, kwa upande wako, wa kufanya kila iwezekanayo – na wewe sio mtu mdogo katika nchi hii – kutusaidia kuzindua mjadala wa kitaifa juu ya hatma ya nchi yetu na bara letu?

Wasalaam,

Issa Shivji

Profesa wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Okotoba 24, 2009

7 comments:

  1. Da! Ama kweli watanzania wengi twaangamia kwa kushindwa kuyafahamu mambo kwa undani. Lol!
    Ahaaa! Kumbe!

    ReplyDelete
  2. mwanasosholojia upo wapi maana umepotea kweli SALAMA KAKA?

    ReplyDelete
  3. Dada yangu Yasinta, mahangaiko na pilikapilika za dunia zinafanya kipindi fulani kutokuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na wapendwa wako. Nimerejea salama usalimini!

    ReplyDelete
  4. Kaka Mathew
    Kwa niaba ya familia yangu na wapenda mema wote nakutakia kila lililo jema wakati huu wa sikukuu na usalama kuelekea mwaka mpya
    Baraka kwako

    ReplyDelete
  5. Natoka nje ya topiki. Heri ya Krismasi Mkuu!

    ReplyDelete
  6. Nashukuru sana Mkuu! Nakutakia sikukuu njema pia!

    ReplyDelete
  7. Ahsante sana Mzee wa Changamoto, Sikuuu njema yenye heri na fanaka!

    ReplyDelete