11/04/2009

Kigoma Wamcharukia Mkuu wa Mkoa

Wananchi Kigoma wakiingia kwenye MV Mwongozo

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Joseph Simbakalia juzi alijikuta katika wakati mgumu baada ya kubanwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa, wakielezea kutoridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho katika kutatua kero za wananchi. Simbakalia alijikuta kwenye hali hiyo alipowasilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 kwa wajumbe wa NEC ya Mkoa wa Kigoma katika kikao kilichofanyika kwenye Hoteli ya Hilltop. 

Wajumbe hao walidai hawaridhishwi na kasi ya serikali katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme, maji na barabara na kueleza kuwa kero hizo zinawaweka katika wakati mgumu kwa chama hicho kupata kura za kutosha kwenye Uchaguzi Mkuu ujao. Mjumbe wa kwanza kuchangia katika taarifa hiyo ya Mkuu wa Mkoa alikuwa ni Katibu wa CCM Wilaya ya Kigoma Mjini, Mtoni Komanya aliyedai serikali ni kama haijali hali inayowakabili wananchi wa Mkoa wa Kigoma hasa Manispaa ya Kigoma Ujiji. 

1 comment:

  1. Namna hiyo ndiyo tunataka!!!

    ReplyDelete