11/04/2009

DECI Yakubali Kuvunja Sheria

Hatimaye kampuni ya Development Entrepreneurship Community Initiative (DECI) inayoendesha shughuli za upatu ambazo haziruhusiwi kisheria, imesalimu amri na kukubali kuwa imekuwa ikivunja sheria za nchi, imefahamika. Kwa mujibu wa tangazo la kampuni hiyo lililotolewa jana katika vyombo mbalimbali vya habari, Deci ilieleza sasa ndiyo inafanya jitihada za kusajili shughuli zake ziendane na sheria zilizopo. 

“Menejimenti ya Deci inapenda kutoa taarifa kwa wateja wake kuwa kampuni inachukua jitihada zote muhimu kuziweka shughuli zake kwa mujibu wa taratibu, ziendane na sheria na taratibu zilizoko,” lilieleza tangazo hilo. Tangazo hilo lilitolewa wakati Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, akisisitiza msimamo wa Serikali kuwa kampuni hiyo haina sifa za kuendesha shughuli za kibenki ambazo kisheria ilipaswa kupata kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kabla ya kuanza kufanya shughuli hizo. 

Kampuni hiyo inayodaiwa kuendesha mchezo wa ‘Vuna Kutokana na Mbegu Uliyopanda’ unaofanyika katika mfumo wa Piramidi, ambao unadaiwa uliwahi kutumika kuchukua amana za watu nchini Kenya na kupotea nazo, imekuwa ikifanya kazi zake kwa kutumia mgongo wa dini bila kufafanua kwa undani shughuli zake. 

Katika tangazo lake hilo la jana, iliwataka wateja wake kutambua kuwa mitaji yao ni salama bila kufafanua ilipo na huku ikitambua kuwa usalama wa mitaji nchini ni dhamana ya Serikali kupitia BoT na Mamlaka ya Masoko ya Hisa na Mitaji (CMSA), ambazo zimeikana kampuni hiyo. Pia Deci katika tangazo lake, ilijihalalisha kuwa ilisajiliwa chini ya Sheria ya Kampuni ya 2002 tangu Julai 2007. 

Hata hivyo, Mkulo alionya kuwa Wakala wa Usajili wa Kampuni Nchini (BRELA) ambaye ndiye anayepaswa kusajili kampuni, hawezi kutumika kupotosha umma kwa kuwa kampuni yoyote inayokusanya fedha za watu lazima isajiliwe BoT. Pia tangazo la BoT na CMSA ambalo ndilo lililoamsha hofu ya usalama wa fedha za wateja walioweka fedha zao Deci na kuamsha sakata la kuwapo kwa kampuni hiyo, liliweka bayana kuwa fedha hizo ziko hatarini kwa kuwa hakuna mamlaka yoyote ya Serikali ambayo inajua zilipo. 

Msimamo wa Serikali uliotolewa jana katika vyombo vya habari, iliwataka Watanzania na wanachama wa Deci kutokaidi tahadhari iliyotolewa na BoT, kuwa kuweka fedha kwenye kampuni hiyo ni hatari kwa usalama wa fedha zao. “Deci haina kibali cha kufanya kazi za kibenki, hivyo inachukuliwa kuwa ni batili na wanachama wanaojihusisha nayo wanatakiwa kuchukua tahadhari,” alinukuliwa Mkulo. 

Kuhusu sheria ya kampuni, Mkulo alinukuliwa akisema: “Hata ukiwa na kampuni ya ususi, unaweza kusajiliwa Brela hivyo Deci wasitumie kigezo hicho kutaka kupotosha umma, ili ifanye kazi za kukusanya fedha za watu, ni lazima uwe na kibali kutoka BoT.” Wakati haya yakitokea pamoja na tahadhari kadhaa kutolewa, kuna taarifa za kuongezeka kwa wanachama wanaojitokeza ‘kupanda’ katika makao makuu ya kampuni hiyo yaliyoko Mabibo, Dar es Salaam.


Wadau imekaaje hii?Kufuata sheria kutasaidia DECI kuleta maisha bora kwa "wapandaji mbegu" wake?

No comments:

Post a Comment