02/04/2011

Bakora hii Nzuri kwa Watendaji?

Gazeti la Mwananchi leo linaripoti kuwa viongozi wa juu wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, watakatwa sehemu ya mishahara yao ikiwa ni adhabu kwa kosa la kushindwa kuwasilisha michanganuo ya taarifa fedha katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2008/09, kwa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac).

Msimamo huo ulitolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Iddi Azan, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kikao cha kamati hiyo.

Alisema viongozi hao waliipelekea kamati hiyo, taarifa ya matumizi ya fedha ya mwaka wa fedha wa 2008/09 bila kuonyesha  michanganuo kuhusu namna fedha hizo zilivyotumika.Azan aliwataja viongozi watakaokatwa asilimia 15 ya mishahara yao kuwa ni Mkurugenzi Mkuu wa halmashauri hiyo, Mweka hazina, Ofisa mipango na Mkaguzi wa hesabu wa ndani.

"Kamati imeona kwamba viongozi hawa wanastahili adhabu kwa kosa la kuleta taarifa ambayo haikuwa na mchanganuo unaoonyesha matumizi ya zaidi ya Sh5 bilioni," alisema Azan ambaye pia  ni Mbunge wa Kinondoni.

Alisema kufuatia hali hiyo, kamati imeirudisha taarifa hiyo kwa viongozi wa halmashauri hiyo ili waweke michanganuo na kuirudishia tena kwa kamati kwa ajili ya ukaguzi, katika vikao vijavyo.

"Kamati imeshangazwa na viongozi hawa ambao wanashindwa kufahamu taratibu za namna ya kuweka mahesabu ya fedha za serikali," alisisitiza.Azan alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, ukaguzi umegundua kuwa viongozi walikuwa wakilipana posho kubwa kinyume cha taratibu.Alisema kamati hiyo itatoa taarifa baadaye kuhusu hatua zitakazochukuliwa dhidi ya viongozi wa halmashauri hiyo.
Mh. Iddi Azan, Makamu Mwenyekiti wa Kamati

Mh. Augustine Lyatonga Mrema, Mwenyekiti wa Kamati

Unafikiri bakora kama hii itasaidia watendaji kuwajibika ipasavyo?

1 comment:

  1. Hiyo ni fimbo ya uchelewa, haiumizi...jaribu kufikiria madhara watakayopata wananchi kwa kukosekana kwa taarifa hizo, vifi nk vitatokea, ukinyumbulisha, kwani pengine yangehitaika madawa, nk...nk..sasa huyu mtu unamchapa kwa fimbo ya chelewa atasikia kweli!

    ReplyDelete