21/05/2011

Mroki na Gamba la CCM

Malenga Mroki Mroki almaarufu Father Kidevu ana neno juu ya "gamba" linalodaiwa kuvuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), na haya hapa ndiyo maneno yake...
 
Eti wajivua gamba, kama nyoka na kinyonga,
Wengine wao ni Mamba, hayatoki hadi panga,
Mkijifanya miamba, yatawakuta ya kinyonga,
Gamba mlilojivua, lisiishie mabegani,

Lisishie mabegani, Gamba mlilojivua,
Myaweke mchangani, yajesombwa na mvua,
Msiyafiche kiganyani, walahi yatawaumbua,
Chama kishike hatamu, gamba kuliweka chini.

Sote tulishangilia, kauli lipotokea,
Gamba kujivulia, CCM tuliwapokea,
Kamwe tu msijelia, Gamba litapokomea,
Gamba mlilojivua, Msiliweke ghalani.

Msiliweke ghalani, hayo mliojivua,
Hayafai asilani, labda kujikinga mvua,
Hayana tena thamani, ni chuya ulochagua,
Chama kishike hatamu, gamba kuliweka chini.
Mtembelee Father Kidevu hapa kijijini kwake http://mrokim.blogspot.com

No comments:

Post a Comment