29/05/2011

Ndoto ya Jumapili!


Ni asubuhi nimeamka
Mwili unachemka
Kijasho kinaniteremka
Kwa ndoto niliyoota

Nilipopanda kitandani
Nilipotoka salani
Kichwa changu mchagoni
Nikapitiwa usingizi

Wala sikuhisi baridi
Na kujifunika zaidi
Hata sikusikia radi
Ndoto nikaanza 'ota

Naanza ingia chomboni
Na kuruka mawinguni
Chombo ni ndege jamani
Tupo juu sana angani

Tumeruka juu sana
Tena kwa kasi hapana
Tunakata wingu pana
Kwa raha na utulivu

Mara ghafla yatokea
Chombo chaanza potea
Chayumba na kulegea
Hatari wanatutangazia

Chini kwa kasi twashuka
Moyo unanishtuka
Huku macho yamenitoka
Nahisi roho kunitoka

Purukushani za angani
Zamalizikia baharini
Ndege yajikita majini
Pumzi kubwa naishusha

Punde tunaanza tolewa
Nje kuliko na hewa
Mizigo yetu tunapewa
Vingine ninapotelewa

Mara nauona mwanga
Wapiga kama upanga
Ninakaa na kujipanga
Ni ndoto ya Jumapili!

1 comment: