27/05/2011

Wapogoro wapo Dar kucheza Sangula?

Sehemu ya eneo la Isongo, Mahenge

Upasuaji mbao katika moja ya hazina ya misitu iliyopo wilaya ya Ulanga

Madini maarufu ya ruby na red spinel yanayopatikana wilaya ya Ulanga

UMOJA wa Uhamasishaji wa Maendeleo ya Wilaya ya Ulanga (Uumau), wenye makao yake Dar es Salaam, umetangaza mkakati wa kusaidia maendeleo ya wilaya yao ili kwenda sambamba na malengo ya dunia kupambana na umaskini.

Hatua hiyo ni sawa na kuupa kisogo wimbo wa ngoma ya sangula uliokuwa ukiimbwa na wakazi wa kutoka wilaya hiyo kwa miaka mingi wakisema ‘ Sisi wapogoro wa Mahenge, tupo Dar es Salaam, kucheza sangula’.

Akitangaza uamuzi huo katika hafla ya kuwapongeza wabunge wanaotokea wilayani Ulanga juzi jioni, Mwenyekiti wa Uumau, Kassian Chibogoyo alisema umoja huo umeanzishwa kwa lengo la kuhamasisha wadau mbalimbali wanaokaa nje ya wilaya hiyo watoe misaada mbalimbali ya maendeleo.

"Tumegundua wilaya yetu inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za ubovu wa barabara, kero ya madaraja, uhaba wa nishati ya umeme, kero ya maji safi na hata huduma mbaya za afya" alisema.

Alisema wilaya hiyo pia inakabiliwa na matatizo ya kukosa benki na uharibifu wa mazingira kutokana na makundi ya wafugaji kuingia na kufyeka misitu kwenye milima mingi.

Alisema kufuatia ukweli huo , Uumau imepania kuchangia maendeleo ya Ulanga kwa hali na mali na kwamba wana umoja wengi ni watalaamu wa fani nyingi hivyo watajitahidi kwenda kufanya kazi zenye upungufu wa watalaamu wake zikiwamo za kufundisha, kutibu watu na kusimamia kilimo.

Kufuatia taarifa hiyo, wabunge wanaotoka Ulanga waliwapongeza wana umoja huo na kuwataka kuimarisha umoja ili maendeleo ya wilaya yao yasonge mbele.

Mbunge wa Ulanga Mashariki kupitia CCM, Celina Kombani alisema matatizo mengi ya wilaya hiyo yalichangiwa na kuzorota kwa elimu na kwamba katika kipindi chake aliweka kero yakukosa elimu kuwa namba moja, jambo alilolifanya kwa kuwasaidia vijana wengi wapate nafasi za ualimu na utumishi wa afya.

Alisema mpaka sasa amewasaidia zaidi ya walimu wapya 100 na maofisa maendeleo vijiji wengi kupata nafasi za elimu. Kombani alisema serikali nayo imepania kujenga daraja la Mto Kilombero ili kuondoa kero ya miaka mingi na kwamba tayari kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu imekamilika.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema, Regia Mtema alisema chama chake kitashirikiana na wananchi wote bila kujali itikadi za vyama katika masuala ya maendeleo.

Mbunge wa Ulanga Magharibi kupitia CCM, Dk Hadji Mponda alisema mipango yake ni kutekeleza falsafa ya Baba wa Taifa marehemu Julius Nyerere iliyosema ili kupata maendeleo lazima wawepo watu, ardhi,siasa safi na uongozi bora.

Alisema mambo hayo yote yapo Ulanga na kwamba kinachotakiwa ni uhamasishaji.Mbunge huyo aliwataka wana umoja huo kuhakikisha wanarudi nyumbani na kupata eneo la ardhi walau ekari tano kila mmoja ili kuepuka kujuta baadaye.

Habari na Mwandishi Wetu. Hisani ya Mohamed Mtenga wa Mahenge Community (mahenge@groups.facebook.com)

No comments:

Post a Comment