|
Mbunge Mteule wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari |
|
|
|
BARUA YA
WAZI KWA Ndg. JOSHUA NASSARI, MBUNGE WA ARUMERU MASHARIKI
Ndugu Joshua,
Natumai umepata pongezi za kutosha juu ya kushinda
kwako katika kinyang’anyiro cha Ubunge. Ushindi wako haukua lelemama. Nchi
nzima iligeuzia macho na masikio yake Arumeru. Uliposhinda ndipo nilipogundua
kuwa hukuwa chaguo la Wanaarumeru wala wapenzi wa Chadema. Kila niliyekutana
naye alilitaja jina lako kwa furaha huku akishangilia kushindwa kwa CCM. Hapa
Chuoni (UDSM), ushindi wako ulikuwa gumzo. Mtaani umejaa vinywani mwa watu. Kwa
utafiti mdogo nilioufanya, wengi wamefurahia zaidi kuporomoka kwa ngome ya CCM.
Kwa ukubwa wa majukumu uliyopewa na matumaini
uliyotwishwa, nadhani hata wewe unatishikatishika. Binafsi nachelea
kukupongeza. Kila nikutazamapo naona nyuso za vikongwe, akina mama na wototo
wenye njaa, waliodhoofu na wagonjwa. Nawaona vijana wasio na ajira na waliokata
tama. Naona umbali mrefu watembeao akinamama kuteka maji. Nawaona yatima,
wajane, n.k. Nawaona wanafunzi waliofukuzwa shule na vyuo kwa kukosa ada…
Wamepoteza matumaini, wote wanakutazama wewe kama jibu la matatizo yao. Huo ni
upande mmoja. Upande wa pili, naona watu wakipanga kugawana fedha za kodi na
miradi ya maendeleo. Naona jinsi rasilimali za nchi hii zinavyoneemesha mataifa
ya nje na vijibwa vyao vya hapa nchini. Na wewe upo katikati ukipiga makelele,
kama kilivyo chama chako [kiitikadi?]. Je, ni silaha gani utakazotumia
kurejesha matumaini kwa wanyonge?
Tafakuri ilinipeleka mbali na kunifanya nikumbuke
Januari 2009, nikiwa mwasisi wa Bunge Kivuli la Vijana wa Dar es Salaam (DSM
Youth Shadow Parliament – DAYOSHPA). Hili lilikuwa jukwaa la aina yake ambalo
liliwakutanisha vijana wa makundi mbalimbali ili kujadili namna ya kuboresha
mfumo wa elimu hapa nchini. Hii ilikuwa ni baada ya mgomo mkubwa wa wanafunzi
wa vyuo vikuu wakipinga mfumo wa madaraja ya mikopo uliopelekea kufungwa kwa
vyuo vikuu vya umma takribani nane. Jukwaa hili halikuwa na mfadhili. Lilikuwa
ni jukwaa la vijana na liliondeshwa kwa nguvu ya vijana bila kulipwa chochote.
Kuna mmoja wa wabunge mahiri katika kambi ya
upinzani ‘aliyenikosesha raha’ katika kiti cha uspika nilichokuwa nimekikalia.
Kila mara alinitumia ki-‘memo’ kunikumbusha kuwa nikimwita jina lake, mwishoni
nitaje ‘Mbunge wa Arumeru Mashariki’, ilhali akijua kuwa wabunge wote wa bunge
lile kivuli hawakuwa na majimbo! Walikuwa ni wabunge wa kitaifa. Mbunge huyo
hakuwa mwingine bali ni wewe Joshua Nassari.
Hiyo ilikuwa ni mwaka 2009. Tayari ulikuwa na ndoto
za kuwania ubunge wa Arumeru Mashariki. Mara kadhaa ulinishawishi kuwa lazima
vijana tushike nafasi za uongozi ili tulete mabadiliko. Niliposema kushika
nafasi za kisiasa sio sawa na kumkomboa myonge, ulinikosoa: ‘Wewe ‘political
scientist’ (mwanasayansi wa siasa) gani usiyependa siasa?’ Nami nikakutahadharisha
kutofautisha kati ya siasa na madaraka huku nikimnukuu Prof. Shivji: ‘[M]imi si
mwanasiasa, ingawa ninapenda siasa. Wanasiasa huwa hawapendi siasa, wanapenda madaraka‘.
Kwa kuwa
tulikuwa tukiishi mtaa mmoja, aghalabu tulikutana kwa mama ntiliye na kuanza
kutaniana. ‘Mheshimiwa Spika, hata wewe unakula kwa mama ntiliye?’ Ila
tukajifariji: sisi ndio wawakilishi halisi wa wanyonge. Tunapanda nao daladala
na tunakula nao kwa mama ntiliye. Na hatukufanya hivyo kwa kuigiza bali ndivyo
maisha yalivyotulazimisha.
Lakini sasa
wewe si mbunge-kivuli tena. Ni mbunge wa ukweli. Hutalazimika kuazima koti na
tai au kushangilia hotuba yako iliponukuliwa gazetini au sura yako kuonekana
katika televisheni [kama tulivyokuwa tukifanya enzi zile]. Hivi sasa, ili magazeti
yauze sharti yaandike habari zako, iwe za kweli ama za uongo. Nafasi yako
inakurusha mbali kimaisha na watu waliokuchagua. Ukipanda daladala au kula kwa
mama ntiliye, utafanya hivyo kwa kuigiza si kwa kulazimishwa na hali ya kipato
chako. Mwisho wa mwezi huu, bila shaka, akaunti yako itakua na salio
lisilopungua milioni kumi! Tena utaongezewa zingine milioni tisini kwa ajili ya
gari. Hayo ndio maisha mapya ya uwakilishi wa wananchi. Sina hakika kama dhana
ya uwakilishi inaleta maana hapa.
Ningependa kukukumbusha
sehemu ya hotuba yako katika Bunge Kivuli mwaka 2009. Kila mmoja alikereketwa
kwa utamu wa hotuba zako zenye mrengo wa kimapinduzi na zilizofanyiwa tafiti.
Iwapo umepoteza mkanda wa Bunge lile, nitakusaidia kunukuu sehemu ya hotuba
yako kuhusu nini kifanyike ili kuiokoa elimu yetu:
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba elimu yetu ni kivuli hafifu cha elimu
ya kikoloni: imekosa ubora uliokuwa ndani ya elimu ya kikoloni ya wakati ule na
pia imekosa maudhui ya kiukombozi kwa sababu haionekani kuwa na malengo thabiti
yanayoangalia mustakabali wa nchi yetu. Katika
vigoda hivi viwili, elimu yetu imedondoka sakafuni.
Mheshimiwa Spika, tumekataa kukubali kwamba mfumo
mzima wa elimu yetu umevurugika baada ya kukubali kwamba turudi katika
chumba cha usanifu na kuuchora mfumo huo upya. Tumehangaika kujenga vyumba
vingi zaidi na kuelezea ujinga kwa gharama kubwa.
Mheshimiwa Spika, kinachohitajika katika mfumo wa
elimu yetu si jambo jingine bali ni mapinduzi ya elimu ambayo yataandamana
na elimu ya mapinduzi itakayozagaa katika sekta zote muhimu. Hii ni kwa
sababu, tukatae tusikatae, sekta kadhaa muhimu nazo zina taswira ileile
tunayoiona katika sekta ya elimu. Napenda kuchukua fursa hii kuangazia nini
kifanyike ili kuhakikisha kuwa serikali inatoa elimu bora na si bora elimu.
Katika hili, nisingependa kuwa nyuma kuunga mkono baadhi ya mitazamo ya
wanafalsafa walioweza kuitoa kuhakikisha kuwa sekta ya elimu nchini
inaboreshwa. Mitazamo hii ni pamoja na ifuatayo:-
Kuwatendea haki walio wengi ambao
tunajua kuwa hawataingia katika vyuo vya elimu ya juu. Hali inaonyesha kuwa ni
sehemu ndogo tu ya watoto wanaoingia shule za msingi ndio wanaopata nafasi ya
kuendelea hadi Chuo Kikuu. Tujenge mifumo ya elimu na mitaala
itakayowafanya watoto wa nchi hii wawe na manufaa kwa jamii zao; watoto wa
wakulima wafundishwe kilimo bora, watoto wa wafugaji wajifunze ufugaji bora,
n.k.
Tuwekeze kwa dhati kwa kutenga rasilimali za kutosha na kuwekeza katika tafakuri
ya pamoja katika shule za umma na kuzifanya ziwe na ubora wa hali ya juu
kiasi kwamba isiwepo haja ya wazazi kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi,
ambazo ni za gharama kubwa
zaidi.
Shule ifundishe sayansi, hisabati na lugha. Lakini pia ifundishe maadili
mema ili kujenga raia wema. Sayansi, teknolojia, hisabati na lugha ni nyenzo
muhimu katika makuzi ya kijana. Lakini iwapo nyenzo hizo hazitaambatana na
mafunzo na malezi ya uungwana ipo hatari watazitumia nyenzo hizo katika
uhalifu.
Watoto wafundishwe na watiwe shime ya kufanya tafakuri ya kiudodosi
(‘critical thinking’). Aidha, vijana wa Tanzania wafundishwe kujiamini,
kutafakari na kusema kwa sauti kile wanachokiamini. Pamoja na maadili, watoto
pia wafundishwe kupenda vitu vizuri ikiwa ni pamoja na umaridadi, michezo na
sanaa ikiwa ni pamoja na muziki na ushairi kama sehemu ya ujenzi wa jamii ya
watu wanaopenda mazingira wanayoishi maisha ya siha na furaha. Elimu
inayomfunza mtoto hisabati lakini haimfundishi namna ya kuvaa vizuri, kula kwa
staha na kuongea kwa ufasaha katika lugha anayoheshimu hadhira inaunda roboti
na si binadamu.
Suala la ubora wa elimu ya walimu liwe nambari moja kwa sababu bila
walimu bora, yote mengine tunayoyafanya, kama vile ujenzi wa majumba, n.k. ni
upuuzi. Walimu watokane na wahitimu wenye ubora wa juu kuliko wengine,
watambulike kwa uwezo wao mkubwa katika masomo yao, waandaliwe vema, walipwe
mishahara mizuri na wapewe marupurupu wanayostahili…
Hebu itazame nukuu ya hotuba yako hapo juu. Hayo
yalikuwa ni mawazo yako katika Bunge Kivuli miaka miwili iliyopita. Sina hakika ni wangapi hutoa mawazo ya aina hiyo
katika Bunge uingialo ambalo ajenda yake kuu ni ‘mipasho na miposho’. Ulitaka
tujitazame kama jamii, tusiangalie tulipoangukia bali tuchunguze tulipojikwaa.
Ulisisitiza kuwa maendeleo hayapimwi kwa vitu bali ubora wa maisha ya watu.
Ulitaka tufanye tafakuri ya kina kama jamii na kufikia mwafaka wa jamii
tuitakayo. Ulisisitiza tufanye mabadiliko ya kimfumo yatakayojenga taasisi
zenye kujali maslahi ya wengi.
Naamini
utajinoa zaidi kinadharia ili usiwe mbwabwaja maneno kwa kuchukulia matatizo
yanayozalishwa na mfumo wa kinyonyaji tulioukumbatia, kuwa mtaji wako wa
kisiasa. Naamini utakinoa chama chako ili kijitaje kinadharia na kivitendo, je,
umma kinaoupigania ni umma gani? Je, umma huo utakombolewa na itikadi/dira
gani? Je, umma huo utakombolewa na nani? Je, ni miiko ipi inapaswa kutawala
maisha ya viongozi na wanachama?
Ngoja
nikutolee mfano: TANU na CCM ya mwalimu Nyerere ilichagua umma wa wanyonge
[wakulima na wafanyakazi] huku itikadi yake ya ukombozi ikiwa Ujamaa. Pamoja na
mapungufu kadhaa ya utekelezaji wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, wananchi
wetu bado wanalikumbuka Azimio la Arusha na kusema: ‘Azimio lilitujali!’ Hata
juzi machinga walipofukuzwa katika eneo la Ubungo, ambapo huuza bidhaa zao
wakati wa jioni, waliimba: ‘Kama sio juhudi zako Nyerere, na amani ingetoka
wapi?’ Wanatambua kwamba amani ni tunda la haki; amani hupatikana kwa kujenga
mfumo unaojali maslahi ya wengi. Ndivyo alivyofanya Mwalimu.
CCM ya sasa
pia ina umma wake – wawekezaji-papa na wafadhili – na itikadi yake ni
uliberali mambo-leo [soko huria]. Machinga, wakulima wadogo, wachimbaji wadogo,
mama ntiliye n.k. sio umma wa CCM. Wao ni uchafu, sio injini ya maendeleo
katika soko huria. Ndio maana hunyang’anywa ajira zao, hunyanyaswa na
kusukumwasukumwa ovyo. Huporwa hata kile kidogo walicho nacho. Hivyo
haishangazi, wakati wananchi wakilalamika kwa hali ngumu ya maisha,
watawala huwashangaa huku wakisema, ‘huko nje tunasifiwa’.
Najua unajiandaa na sherehe ya kuapishwa. Naomba
nikugawie kipande cha keki niliyopewa na Prof. Shivji wakati nikihitimu shahada
ya kwanza mwaka 2011. Ni keki isiyoisha, isiyooza, isiyopungua utamu:
Maisha sio porojo
Za siasa na Abunuwasi.
Maisha sio uhondo
Wa dhahabu na almasi
Maisha sio uhongo
Wa ufisadi na uchoyo
Wa mali na madaraka.
Maisha ni kuishi
Kuishi uhai wa walalahoi.
Maisha ni kujitolea
Mhanga wa ukombozi
Ukombozi wa kitabaka
Tabaka la wanyonywaji
Tabaka la wanyanyaswaji.
…
Nakutakia kila la heri katika utekelezaji wa
majukumu yako.
Wasalaam,
Sabatho Nyamsenda,
Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya
Siasa,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
6/4/2012.