17/06/2011

Kukukwaza Sitamani!

Kuna kipindi naumia
Maumivu kugugumia
Unapopatwa na udhia
Hata uanzapo kulia

Nashikwa na huzuni
Nayo majonzi moyoni
Pia raha siioni
Nikikutazama usoni

Ni mimi nakukwaza
Kujisahau kuwaza
Kutofikiria kwanza
Kudhani nakuliwaza

Ni kawaida kwa wawili
Kupishana Kiswahili
Twapendana kweli kweli
Makwazo tuyastahimili

Wewe ni mzuri mno
Unanipa penzi nono
Wanilaza kama pono
Unipapasapo kwa mikono

Kukukwaza sitamani
Si kusudi asilani
Ewe wangu mwandani
Nielewe jamani

Siku zote nakuahidi
Moyo wangu ni shahidi
Sitakuja kukukaidi
Penzi langu ufaidi

Nisogelee mwandani
Na unilaze kifuani
Ninong’oneze sikioni
Na kunibusu shingoni

3 comments:

  1. Mkuu kumbe unaimudu fani ya malenga wetu (unakikumbuka kipindi hicho huko Radio Tanzania?)

    ReplyDelete